Tetesi za Soka Ulaya Jumanne: Arsenal yafikiria kumsajili Fofana, bado yamuwania Alvarez

Chanzo cha picha, SNS
Arsenal inatathmini uwezekano wa kufanya usajili wa dakika za mwisho wa winga wa Lyon na timu ya taifa ya Ubelgiji, Malick Fofana, kabla ya dirisha la usajili kufungwa Jumanne.
Kwa mujibu wa RMC Sport, klabu hiyo ya London Kaskazini inafuatilia kwa karibu hali ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 huku ikitathmini uwezekano wa kufanikisha dili hilo katika siku za mwisho za usajili.
Wakati huo huo, Arsenal haijaondoa nia yake ya kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez. Ripoti zinaeleza kuwa viongozi wa Gunners wanaendelea kufanya kazi ya kuweka mazingira yatakayorahisisha nyota huyo wa Argentina kuhamia London.

Chanzo cha picha, Getty Images
Teamtalk inaripoti kuwa Arsenal bado ina matumaini ya kufanikisha uhamisho wa Alvarez, mwenye umri wa miaka 26, huku mawasiliano kati ya wahusika wa mchezaji huyo na klabu yakiendelea.
Kwingineko, Liverpool imekataa ofa ya pauni milioni 30 iliyowasilishwa na Nottingham Forest kwa ajili ya kiungo chipukizi Trey Nyoni. Inaelezwa kuwa mabingwa hao wa Premier League hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo mwenye matumaini makubwa katika siku hizi za mwisho za dirisha la usajili.
Wakati huo huo, Borussia Dortmund inatafakari uwezekano wa kumrudisha Jadon Sancho kwa mara nyingine katika klabu hiyo ya Bundesliga.
Ripoti za Bild zinaeleza kuwa Dortmund iko tayari kumpa fursa mpya winga huyo wa England mwenye umri wa miaka 26 ili kufufua taaluma yake. Hata hivyo, Sancho atalazimika kukubali masharti tofauti na mikataba yake ya awali, ikiwa ni pamoja na makubaliano yanayozingatia zaidi kiwango cha utendaji uwanjani pamoja na kuachana na bonasi ya kusaini mkataba.
Kwingineko, Newcastle United imepiga hatua kubwa katika harakati zake za kuimarisha kikosi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
The Athletic inaripoti kuwa klabu hiyo imefikia makubaliano na Lille kuhusu ada ya uhamisho wa kiungo wa Ubelgiji Matias Fernandez-Pardo. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano utakaomfanya kuwa sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Newcastle katika St James' Park.












