Je, Trump ataweza kumpa kila Mmarekani dola 5,000 alizoahidi?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Alex Boyd
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameahidi kumpa kila Mmarekani mwenye umri wa utu uzima dola 5,000 iwapo chama cha Republican kitashinda uchaguzi wa katikati ya muhula wa Novemba.

Hata hivyo, bado haijafahamika fedha hizo zingetoka wapi, wala kama mpango huo unaruhusiwa kisheria.

Kauli hiyo iliwafurahisha wafuasi wake katika mkutano wa chama Jumatano usiku, huku Democrats wakiuita "ahadi isiyo na msingi."

Trump pia amesema fedha hizo zitatakiwa kutumika nchini Marekani, ingawa haijafahamika jinsi matumizi hayo yatakavyofuatiliwa.

Makamu wa Rais JD Vance amesema huenda malipo hayo yakagharamiwa kutokana na mapato ya ushuru wa forodha, huku akisema Wamarekani matajiri hawatapokea fedha hizo.

Je, ahadi hiyo ni halali?

Sheria ya shirikisho ya Marekani inapiga marufuku kutoa malipo yanayolenga kushawishi mtu jinsi ya kupiga kura.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa sheria wanasema ahadi ya Trump inaweza kutafsiriwa kama mpango wa kupunguza kodi, jambo linaloruhusiwa kisheria.

Mtaalamu wa sheria, Dkt Joan Mahoney, kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, amesema anaamini ahadi hiyo ni halali, ingawa si kawaida kwa wanasiasa kuweka ahadi za aina hiyo wazi kiasi hicho.

''Kwa upande mmoja inaweza kuonekana kama rushwa ya kisiasa, lakini kwa kuwa fedha hizo zingetolewa kwa kila mtu bila kujali amempigia kura nani, huenda zisitambuliwe kama rushwa'', amesema Joan.

Hata hivyo, Laurel Rapp, Mkurugenzi wa Chatham House amesema ahadi hiyo inaonekana kuwa tofauti na ahadi za kawaida za kisiasa, kwani ni makubaliano ya moja kwa moja yanayohusisha fedha na uchaguzi.

Ingegharimu kiasi gani?

Kuna takriban Wamarekani milioni 270 wenye umri wa utu uzima. Kuwalipa kila mmoja dola 5,000 kungeigharimu serikali karibu dola trilioni 1.3.

Trump hakutoa maelezo kuhusu namna malipo hayo yangefadhiliwa.

Congress ndiyo yenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha za serikali Marekani. Hata hivyo, Trump hakusema kama angeomba Congress kuidhinisha malipo hayo.

Wataalamu wa sheria pia wanasema kuna uwezekano mdogo wa Trump kuidhinisha kiasi hicho kikubwa kupitia amri ya rais pekee.

Erica York, mchumi mwandamizi katika shirika la Tax Foundation lenye makao yake makuu jijini Washington DC, aliambia BBC kuwa angekuwa "na mshangao mkubwa" iwapo Bunge lingeidhinisha pendekezo lolote.

"Hii ingekuwa mojawapo ya njia mbaya zaidi za kutumia dola trilioni 1.3," alisema.

"Tuko kwenye mkondo usio endelevu, huku nakisi ikitarajiwa kuendelea kuongezeka zaidi na zaidi," York aliongeza.

s

Chanzo cha picha, EPA

Je, ushuru wa forodha unaweza kugharamia?

Akizungumza na shirika la utangazaji la Fox News, Makamu wa Rais Vance amesema huenda malipo hayo yakagharamiwa kwa mapato yanayotokana na ushuru wa forodha.

Hata hivyo, mapato hayo bado yako mbali sana na kiasi kinachohitajika kugharamia dola 5,000 kwa kila Mmarekani mtu mzima.

Kwa mujibu wa Bipartisan Policy Center, Marekani imekusanya karibu dola bilioni 475 kutokana na ushuru wa forodha na kodi za bidhaa tangu mwanzoni mwa mwaka 2025.

Lakini zaidi ya dola bilioni 100 zimerudishwa baada ya Mahakama ya Juu ya Marekani kubatilisha ushuru kadhaa mapema mwaka huu.

Walipoulizwa jinsi malipo hayo yangeweza kufanyika, Ikulu ya Marekani ilisema katika taarifa kwa BBC: "Watu wenye mtazamo hasi na wanaotabiri mabaya wameendelea kumtilia shaka Rais Trump."

"Kwa kuendelea kuungwa mkono na wananchi wa Marekani, Rais Trump ataendelea kuleta matokeo halisi," aliongeza msemaji Davis Ingle.

Kwa nini Trump ametoa ahadi hiyo?

Wachambuzi wa siasa wanasema ahadi hiyo inapaswa kutazamwa katika muktadha wa uchaguzi wa katikati ya muhula, ambao umesalia chini ya miezi miwili.

''Ni ahadi kubwa isiyoeleweka fedha zake zitatoka wapi, lakini uchaguzi ndio unaokaribia'', Mshauri wa zamani wa Republican na mchambuzi wa kura, Robert Moran

Laurel Rapp wa Chatham House amesema Trump anaangalia muda mfupi katika juhudi za kuhakikisha Republican wanadhibiti bunge la Marekani, Congress, katika miaka miwili ya mwisho ya muhula wake.

"Suala la fedha ndilo analoligeukia sasa kwa sababu matokeo ya tafiti za maoni hayawaendei vyema Warepublican wala hayamuendei vyema yeye binafsi," aliendelea kusema.

Je, jambo kama hili limewahi kutokea?

Trump aliwahi kupendekeza malipo ya dola 2,000 kwa Wamarekani, ambayo yangefadhiliwa na mapato ya ushuru wa forodha, lakini malipo hayo hayakuwahi kutekelezwa.

Rais wa zamani Joe Biden pia aliwahi kushutumiwa kwa kujaribu kununua kura baada ya kuahidi malipo ya dola 2,000 ya msaada wa Covid kwa Wamarekani iwapo Democrats wangeshinda uchaguzi wa Seneti huko Georgia mwaka 2021.

Mzozo kama huo uliibuka tena kabla ya uchaguzi wa urais wa 2024, wakati bilionea Elon Musk, ambaye ni mfuasi wa Trump, alipotoa motisha za fedha kwa wapiga kura waliosajiliwa katika majimbo saba yenye ushindani mkubwa.

Taarifa za ziada kutoka kwa Bernd Debusmann Jr, mwandishi wa habari wa Ikulu ya Marekani (White House)