Maswali matano muhimu kujiuzulu kwa Nchimbi

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Sammy Awami
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Taarifa za kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Dkt Emmanuel Nchimbi zimeibua mshituko mkubwa Tanzania. Hata hivyo kwa wengi, si kwa sababu hawakutarajia kwamba Nchimbi angejiuzulu, bali kwamba kwa hakika imetokea, tena kwa Nchimbi ikiwa chini ya mwaka mmoja tangu ashike wadhfa huo.
Changamoto kubwa, na hasa kwa wanahabari, imekuwa kusema kwa uhakika sababu hasa ya Nchimbi kujiuzulu. Hii ingekuwa ya muhimu sana kulipatia taifa utulivu na amani ya moyo – au kwa Kiingereza inaitwa 'closure' – ikiwa kujiuzulu kwake kunatokana na uwajibikaji, ajali mbaya ya kisiasa au sababu nyingine isiyoepukika.
Isivyo bahati, taarifa zilizotapakaa miongoni mwa umma ni tetesi pekee ambazo zimekuwa ngumu kuthibitishwa haraka aidha na vyanzo rasmi au visivyo rasmi, hata kwa makubaliano ya kutotaja majina au kutambulishwa rasmi, kama ilivyo desturi ya kawaida ya uandishi wa habari duniani kote.
Na sasa, kupitia barua inayoaminika kuwa yake, kuna maswali kadhaa yanayoibuka.
Kwanza, hatua ya kujiuzulu katika utumishi wa umma, hata kama uamuzi huo unachukuliwa na mtumishi mwenyewe, kwa kawaida hutangazwa rasmi na mamlaka ya uteuzi, ikisema mtumishi ameomba kujiuzulu na kiongozi wake ameridhia kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
Katika hili la Nchimbi, ni yeye ndie aliyetangaza kuchukua uamuzi huo na kuutangazia umma kabla hata kiongozi wake aliyeridhia kuwa mgombea mwenza wake na kuzunguka nchi nzima kuomba kura kufanya hivyo.
Mtindo huu unafananana na ule uliotumika kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Marehemu Job Ndugai. Hata hivyo, tofauti na Ndugai, nafasi ya Makamu wa Rais ina utaratibu na mlolongo unaohusisha si tu chama tawala kilichoshiriki katika kumpendekeza na kumuidhisha kushika wadhfa huo, bali pia bunge ambalo litahitajika kufanya utaratibu wa kupata mbadala wake
Kwanini Nchimbi ametangaza kujiuzulu na si Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndie angeidhinisha kujiuzulu kwake?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini tangazo hili linakuja kupitia mtandao wa kijamii, ambao si tu kwamba si nyenzo au jukwaa rasmi la kutangaza uamuzi nyeti kama huo, mara ya mwisho wa akaunti hiyo kutumika ilikuwa mwaka 2023, ikiibua maswali mengi juu ya uhalali na uhakika wa akaunti hiyo.
Kwanini Nchimbi hakutumia njia na majukwaa rasmi kutangaza uamuzi wake?
Sehemu ya maudhui ya barua ya kujiuzulu pia yanaibua maswali mengi. Katika aya ya pili ya barua yake, Nchimbi anasema mnamo tarehe 27 Agosti 2025, alimuhakikishia Rais Samia kwamba siku akiona anahitaji Makamu wa Rais mwingine, ataachia nafasi hiyo.
"Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza Ahadi yangu" inasomeka sehemu ya barua ya Nchimbi
Ndio kusema Nchimbi aliona dalili kwamba asingeweza kufika hadi mwisho wa muhula wa Rais Samia? Kwanini bado alipewa kuwa Makamu wa Rais? Ni ishara gani aliyoipata sasa Nchimbi iliyomuhakikishia kwamba Rais Samia anataka mabadiliko? Ni mabadiliko gani haya?
Barua hiyo inaonekana kuandikwa na kusainiwa tarehe 26 Agosti 2026, lakini Nchimbi anasema tarehe rasmi ya kujiuzulu kwake ni tarehe 04 Septemba. Kwanini hakujiuzulu tarehe hiyo hiyo 26 Agosti au kwanini hakusubiri aandike na kuisambaza barua yake tarehe 04 Septemba?

Chanzo cha picha, IKULU
Tunachofahamu ni kwamba kati ya wiki hii hadi tarehe hiyo 04 Septemba kuna kikao cha Kamati Kuu ya CCM ambacho kimekaa (inawezekana kabisa kilifikia maamuzi), kuna kikao cha baraza kuu kinachotarajiwa kukaa siku ya Jumatano (inawezekana kingepokea maamuzi ya Kamati Kuu) na tarehe 04 hiyo pasipo shaka pangekuwa na mchakato au hata maamuzi kabisa ya bunge kufanyika juu ya hatma ya nafasi yake ya Makamu wa Rais.
Ndio kusema Nchimbi amefanya hivi kukiwahi chama na bunge, ili aondoke kwa namna anayoitaka yeye na si kufukuzwa?
Mengi ya maswali haya inawezekana yasipatiwe majibu kabisa lakini tukio moja linalotuambia ni wakati gani mpasuko ulifikia kiwango kisichorekebishika ni lile ambalo Nchimbi alitoa witu kwa wananchi kusimama kidete na kudai Katiba mpya
"Ningeambiwa 'Makamu wa Rais hebu waambie Watanzania jambo moja tu, wakisema una jambo la kuwaambia Watanzania jambo moja tu, unapewa nafasi ya mwisho, sema jambo moja tu' nitasema pambaneni mpate Katiba mpya" alisema Nchimbi katika hafla iliyoandaliwa na shirika la watetezi wa haki za binadamu THRDC
Hotuba hii, ilitanguliwa na tukio la mbunge wa Tunguu Zanzibar Mohamed Simai Said aliyesimama bungeni na kuzungumza kwa mafumbo juu ya mtu aliyempa jina la 'Yuda', huku wasifu alioendelea kuueleza kuonesha wazi kwamba alikuwa akimzungumzia Nchimbi
Simai alimlaumu huyo 'Yuda' kwa kuvunja imani ya aliyemteua na kumshutumu kwa kuumiza safari ya kisiasa ya wanasiasa wengi, kusaliti watu wake wa karibu, lakini zaidi kukwamisha jitihada za Rais Samia katika kuleta maendeleo nchini.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya CCM zinasema wito wa Nchimbi kuhimiza Watanzania 'kupambana' kuhakikisha wanapata Katiba mpya uliwapa washirika kindakindaki wa Rais Samia ndani ya chama sababu na ujasiri wa kuibua hoja ndani ya chama ya kumuadhibu Nchimbi kwa kumvua wadhfa wake kwani aliaminika wazi kuongoza jitihada za kushindana na hata kukwamisha jitihada za kiongozi wake Rais Samia.
Kilichofuata ni historia.













