Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, uamuzi wa kesi ya Tupac unaweza kuchochea uchunguzi mpya kuhusu mauaji ya Notorious B.I.G.?
Hukumu ya hatia dhidi ya Duane "Keffe D" Davis mjini Las Vegas imehitimisha mojawapo ya kesi maarufu zaidi duniani za mauaji ambayo hayakutatuliwa.
Alipatikana na hatia ya mauaji ya mwanamuziki wa muziki wa kufoka, Tupac Shakur, aliyefariki dunia baada ya gari aina ya BMW la rangi nyeusi alilokuwa akisafiria kumiminiwa risasi katika shambulio la kufyatuliwa risasi kutoka kwenye gari lingine mwaka 1996.
"Hili ni jambo kubwa. Ilikuwa kesi ngumu. Ilikuwa kesi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu bila ufumbuzi," wakili wa zamani wa mashtaka, Neama Rahmani, aliambia BBC. "Tunazungumzia rapa bora zaidi wa wakati wote, gwiji, na hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa au kushtakiwa kwa miaka 30."
Hukumu hiyo inaleta faraja na kuhitimisha sintofahamu kwa familia ya Shakur, na imezua maswali miongoni mwa wadadisi kuhusu nini hili linaweza kumaanisha kwa kesi inayofanana nayo kwa karibu kabisa: mauaji ambayo hayajatatuliwa ya Notorious B.I.G., au Biggie Smalls, ambaye jina lake halisi lilikuwa Christopher Wallace.
Wallace, ambaye alikuwa mwenyeji wa New York, hapo awali alikuwa mmoja wa marafiki wa Shakur, lakini wawili hao wakawa mahasimu na kuwakilisha mgogoro kati ya Pwani ya Mashariki na Pwani ya Magharibi uliotawala muziki wa hip-hop katika miaka ya 1990.
Wallace aliuawa jijini Los Angeles miezi michache baada ya Shakur katika mazingira yanayofanana, akipigwa risasi na watu waliokuwa wakipita wakiwa ndani ya gari. Hakuna mtu aliyewahi kushtakiwa kwa mauaji hayo.
"Mauaji ya Tupac na mauaji ya Biggie ni matukio mawili muhimu sana katika maisha yetu," alisema Justin Tinsley, mwandishi wa habari wa Andscape (ESPN) na mwandishi wa kitabu It Was All a Dream: Biggie and the World That Made Him.
"Wanaume hao wawili walikuwa wa kipekee, wenye vipaji na ushawishi mkubwa, kila mmoja kwa namna yake," Tinsley aliiambia BBC. "Lakini haiwezekani kusimulia hadithi ya mmoja wao bila kusimulia pia hadithi ya mwenzake."
"Unapozungumzia kesi hizi, siku zote zitakuwa na uhusiano kwa sababu kuna watu wengi wanaohusika katika matukio yote mawili, wakiwemo wahusika wakuu na wale wa pembeni," alisema.
Kwa muda mrefu, wadadisi wameamini kuwa mauaji hayo mawili yalihusiana. Jina la Wallace lilitajwa wakati wa kesi ya Duane Davis. Yeye na Davis walikuwepo kwenye sherehe moja usiku ambao Wallace aliuawa, na polisi walimhoji Davis kuhusiana na tukio hilo.
Mpelelezi aliyeendesha mahojiano hayo alitoa ushahidi pia katika kesi ya mauaji ya Tupac.
Hatua muhimu iliyopelekea kutatuliwa kwa kesi ya Shakur hatimaye ilitokana na jambo moja kuu: maneno ya Davis mwenyewe.
Kupitia makala za video, vyombo vya habari, kitabu chake cha kumbukumbu, vipindi vya sauti (podcasts) na hata mahojiano ya siri na polisi, alikiri kuhusika kwake katika kifo cha Shakur.
Davis alisema alitupa bunduki kwenye kiti cha nyuma cha gari, na mpwa wake, Orlando Anderson, akaitumia kumpiga risasi Shakur, ambaye baadaye alifariki kutokana na majeraha hayo, walipolifikia gari lake wakiwa sambamba nalo huko Las Vegas mnamo tarehe 7 Septemba 1996.
Anderson alipigwa risasi na kufariki dunia mwaka 1998, baada ya hapo awali kukana kuhusika na mauaji ya Shakur.
Wakati wa kesi hiyo, hakukuwa na mashahidi walioona tukio hilo na kumthibitisha Davis kuwa ndani ya gari, hakukuwa na silaha ya mauaji iliyowasilishwa, wala ushahidi wowote wa video au picha. Timu yake ya utetezi ilifikia hatua ya kusema kuwa hakukuwa hata na uthibitisho kwamba alikuwepo Las Vegas usiku huo.
Rahmani alisema ilikuwa kesi ngumu kuendesha mashtaka. Alibainisha kuwa uvumi na dhana zilizomzunguka Davis hazikuwa jambo geni na zilikuwepo kwa miongo kadhaa, lakini uamuzi wa kumshtaki na kuendelea na kesi hiyo ulikuwa "changamoto kubwa" na hatua ya ujasiri kwa waendesha mashtaka.
"Angalia, unapokuwa mwendesha mashtaka, unatarajiwa kushinda kila wakati. Walifanya uamuzi mgumu wa kuendesha kesi ambayo watu wengi walidhani isingewezekana kushinda," alieleza. "Na walipata haki, ambapo watu wengine hawakujisumbua hata kujaribu."
Wakili wa Davis, Michael Sanft, aliwataka wajumbe wa jopo la mahakama kuzingatia swali: "Je, mna ukweli gani?" Aliwahimiza wajumbe hao, kabla ya kufikia uamuzi wa hatia, wamchukulie mteja wake kama mwongo aliyesimulia hadithi ili kuuza vitabu na kujipatia fedha.
"Hakuna ushahidi," aliwaambia wajumbe wa jopo la mahakama.
Wakati uamuzi wa hatia uliposomwa mahakamani, familia ya Shakur ilionyesha hisia kali. Baadhi walilia na kufuta machozi kwa vitambaa. Wengine walikumbatiana na kushikana mikono. Mwanafamilia mmoja alimkumbatia mmoja wa waendesha mashtaka katika kesi hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Mwendesha Mashtaka wa Wilaya ya Clark County, Steve Wolfson, aliwashukuru jaji, waendesha mashtaka na wanafamilia wa Shakur, ambao alisema walipata ahueni kubwa na kwamba "hatimaye wamepata haki."
"Mpendwa wao aliuawa," alisema. "Walisubiri miaka 30 kwa ajili ya kesi hiyo. Inaeleweka kabisa kwa nini walihisi ahueni."
Wakili wa kesi hiyo, Shaun Kent, alisema kuwa kesi hiyo ilibadilika na kukua kadiri mahojiano yalivyoendelea na kila mara Davis alipoamua kuzungumzia suala hilo.
"Hakukuwa na mashahidi wengine, isipokuwa yeye mwenyewe," Kent aliiambia BBC kabla ya kesi kuanza, akibainisha kuwa "shahidi mkuu dhidi yake ni yeye mwenyewe."
Rahmani aliamini kuwa huenda Davis asingekabiliwa na mashtaka yoyote kama angebaki kimya.
"Kwa kweli hakuweza kujizuia," Rahmani aliongeza. "Hata baada ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini, aliendelea kutoa mahojiano."
Sehemu kubwa ya kesi ya Shakur iliwalazimu wajumbe wa baraza la mahakama kurejea katika mazingira ya miaka ya 1990, kipindi cha vurugu kali za magenge yaliyokuwa yamejipenyeza ndani ya muziki wa hip-hop na kuchochea uhasama kati ya wanamuziki wa rap wa Pwani ya Mashariki na Pwani ya Magharibi.
Kilikuwa kipindi cha kutoaminiana kwa kiwango kikubwa kwa polisi na kuwepo kwa kanuni za mitaani zilizokataza kutoa taarifa kwa mamlaka.
Hata Shakur, baada ya kupigwa risasi kadhaa katika shambulio la gari kwa gari ambalo hatimaye liligharimu maisha yake, alikataa kuzungumza na mamlaka.
"Tutashughulikia wenyewe," alisema akiwa ndani ya gari la wagonjwa wakati afisa mmoja akijaribu kumhoji.
Ukimya huo ulijirudia miezi kadhaa baadaye katika tukio la kuuawa kwa Biggie Smalls kwa kupigwa risasi.
Biggie, mmoja wa wanamuziki wakubwa wa rap kutoka Pwani ya Mashariki, alikuwa akitoka katika sherehe ya baada ya hafla ya Tuzo za Muziki za Soul Train mjini Los Angeles wakati gari aina ya Chevrolet nyeusi liliposogea karibu na gari lake kwenye taa nyekundu za barabarani na kufyatua risasi mnamo tarehe 9 Machi 1997.
Tukio hilo lilitokea takriban miezi sita baada ya shambulio la risasi lililomuua Shakur, mmoja wa wanamuziki wakubwa wa rap kutoka Pwani ya Magharibi.
Wote wawili walikuwa wasanii walioteuliwa kwa Tuzo za Grammy katika viwango vya juu zaidi, wakipata mamilioni ya dola na kupata uchezaji mkubwa kwenye redio mara kwa mara. Ugomvi wao ulijitokeza pia katika mashairi ya nyimbo zao na ulisababisha vitisho pamoja na vurugu.
Ghasia zilizuka katika mitaa ya Los Angeles kufuatia mauaji ya wawili hao kwa kupigwa risasi, huku magenge ya mitaani yakijaribu kulaumiana kwa vifo vya wanamuziki hao wa rap.
Kwa miaka mingi, hakuna kati ya mauaji hayo yaliyosababisha mtu kukamatwa au kuhukumiwa, na kilichobaki ni uvumi na nadharia za njama.
"Watu watatafuta hitimisho kwa njia yoyote watakayoweza kulipata," Tinsley alisema. "Watu wamekuwa wakijaribu kuelewa kilichotokea kwa miaka 30."
Kama ilivyo kwa kifo cha Shakur, nadharia na majina mengi yamehusishwa na kifo cha Biggie huko Los Angeles, lakini Idara ya Polisi ya Los Angeles (LAPD) haijawahi kumkamata mtu yeyote kuhusiana na mauaji hayo.
"Kwa kweli hili ni doa kwa Idara ya Polisi ya Los Angeles (LAPD). Ukweli kwamba tukio hili liliweza kutokea bila mtu yeyote kukamatwa au kushtakiwa," alisema Rahmani, akibainisha kuwa mauaji ya Biggie yalifanyika barabarani katikati ya jiji la pili kwa ukubwa nchini Marekani.
"Waendesha mashtaka hawapendi kushindwa," alieleza Rahmani. "Lakini huenda hukumu hii ya hatia katika kesi ya Tupac ikawapa moyo watu huko Los Angeles kuangalia upya suala hili, kesi ambayo imekaa bila maendeleo kwa muda mrefu na sasa inakaribia kutimiza miaka 30."
Walipoulizwa kuhusu kesi hizo na iwapo hukumu ya hatia katika mauaji ya Tupac inaweza kufufua uchunguzi wa kifo cha Biggie, LAPD iliiambia BBC kwamba inafahamu kuhusu hukumu hiyo na kwamba uchunguzi wa kesi ya Biggie bado unaendelea.
"Mauaji ya Christopher Wallace bado ni kesi wazi ambayo haijatatuliwa katika Kitengo cha Wizi na Mauaji cha LAPD," alisema Luteni Elpidio Orozco, huku akiwahimiza watu wenye taarifa zozote kuwasiliana na mamlaka husika.
Ingawa kesi ya Wallace imekaa bila maendeleo kwa muda mrefu, shauku ya umma bado ipo.
"Wamekuwa wamefariki kwa muda mrefu zaidi kuliko walivyoishi," alisema Tinsley. "Lakini hadithi na taswira zinazoendelea kuwazunguka watu hawa na vifo vyao zitaendelea kuwa mada katika mazungumzo siku zote."
Kayla Epstein alichangia katika taarifa hii.