Ubingwa EPL utaamuliwa lini?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Shamoon Hafez
- Nafasi, Manchester City reporter at Hill Dickinson Stadium
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Manchester City wametoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Everton katika uwanja wa Hill Dickinson Stadium, kwenye mchezo kiporo wa Ligi kuu ya England (EPL) uliopigwa Jumatatu ya Mei 04, 2026.
Dakika 13 za hekaheka kubwa kwa Manchester City katika kipindi cha pili cha mchezo huo wa kusisimua wenye mabao sita huenda zikawa zimewaharibia City nafasi yao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England.
Mechi hiyo ya Jumatatu ilikuwa moja ya mechi bora zaidi msimu huu, na matokeo yake baada ya kumalizika kumeleta mshangao huenda yakawa na athari kubwa mwishoni mwa msimu.
Timu ya Pep Guardiola ilianza kwa kuongoza kwa bao 1-0 kupitia Jeremy Doku, lakini iikaruhusu mabao matatu ndani ya dakika 13 kupitia Thierno Barry aliyefunga mabao mawili, moja likisaidiwa na kosa la Marc Guehi na Jake O'Brien aliyefunga kwa kichwa.
Hata hivyo, Erling Haaland alipunguza pengo mara moja, na winga wa Ubelgiji Jeremy Doku akaisawazishia City kwa bao la kuvutia katika dakika za mwisho, lakini City wamepoteza alama muhimu katika mbio za ubingwa dhidi ya vinara Arsenal.
Hii ina maana kuwa hatima ya ubingwa sasa iko kabisa mikononi mwa Arsenal, lakini lini hasa ubingwa utaamuliwa?
Ni lini ubingwa EPL unaweza kuamuliwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya sare yao dhidi ya Everton, kiwango cha juu kabisa cha alama ambacho Manchester City wanaweza kufikia msimu huu ni 83.
Arsenal kwa sasa wana alama 76, hivyo wanajua kwamba ushindi katika mechi zao tatu zilizobaki utawapa ubingwa, kwa sababu watafikisha alama 85.
Pia tofauti ya mabao ya Arsenal ni bora kwa mabao manne kuliko City, jambo linalowapa faida ndogo.
Lakini yako mazingira ambayo timu ya Mikel Arteta inaweza kutwaa ubingwa mapema kabisa tena Jumatano wiki ijayo, 13 Mei.
Iwapo Arsenal wataifunga West Ham Jumapili na Manchester City wakipoteza dhidi ya Brentford siku moja kabla, kisha City wakapoteza tena dhidi ya Crystal Palace siku chache baadaye, Arsenal watakuwa mabingwa wakiwa bado na mechi mbili mkononi.
Lakini kama timu zote mbili zitaendelea kushinda, mbio hizo za ubingwa zitakwenda mpaka mwisho wa msimu.
"Mwendo huu ni pigo kubwa kwa Manchester City katika mbio za ubingwa, lakini lazima wajikusanye na waendelee," alisema mchezaji wa zamani wa Blackpool Charlie Adam kupitia BBC Radio 5 Live.
Bado kuna uwezekano wa kutokea kwa matokeo ya kushutua ama kushangaza katika mbio hizo.
Guardiola hajakata tamaa licha ya matokeo

Chanzo cha picha, Getty Images
Mechi hii iliyopigwa Hill Dickinson Stadium ilionekana kuwa ngumu kwa City kabla ya mchezo, na hatimaye ikawa hivyo, huku wakipoteza alama mbili muhimu dhidi ya timu inayowania nafasi za kucheza mashindano ya Ulaya msimu ujao.
"(sare) ni bora kuliko kupoteza," alisema Pep Guardiola kuhusu sare ya 3-3. "Inaonyesha aina ya timu tuliyocheza nayo."
"[Ubingwa] hauko mikononi mwetu tena. Awali ulikuwa mikononi kwetu, sasa haupo. Bado tuna mechi zilizobaki. Tutaona kitakachotokea."
Arsenal sasa wanajua kuwa kushinda mechi zao tatu zilizobaki kutawapa ubingwa wao wa kwanza tangu mwaka 2004.
Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry alisema kupitia Sky Sports: "Sifikirii kwamba wanaweza kukubali kupoteza alama sasa, lakini ni kweli kwamba iko mikononi mwao. Hilo ni jambo la kweli."
"Nitabaki kwenye nafasi yangu, sitasherehekea mapema. Mambo bado."
Uelekeo na mechi zilizosalia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
City wana mechi tatu za nyumbani dhidi ya Brentford, Crystal Palace na Aston Villa itakayopigwa katika siku ya mwisho ya msimu (Mei 24).
Mechi yao ya ugenini iliyosalia ni dhidi ya Bournemouth. Hii ndiyo mechi ngumu kati ya zilizosalia kwa mazingira na uwezo. Bournemouth wanaoonyesha kiwango bora, lakini pia mechi itachezwa siku tatu baada ya fainali ya FA Cup dhidi ya Chelsea.
Wakati City wakilenga kutwaa mataji matatu ya ndani, Arsenal sasa wana nafasi ya kutwaa mataji mawili, ligi kuu na ligi ya mabingwa Ulaya.
Arsenal watakabiliana na West Ham ugenini, kisha Burnley waliokwisha shuka daraja nyumbani, kabla ya mchezo wa mwisho dhidi ya Crystal Palace ugenini.
Thierry Henry alisema: "Nina wasiwasi na mchezo dhidi ya West Ham. Kama nilivyokuwa na wasiwasi kwa City leo."
Nahodha wa zamani wa England, Wayne Rooney alisema kwamba anaamini Arsenal watashinda mechi zao zote zilizobaki na kutwaa ubingwa.
Alisema: "Tumesikia mengi kuhusu Arsenal kushindwa kukabiliana na presha, lakini sasa ni tofauti. Nafikiri huu ni mwaka wao."










