Mkoba wa siri wa kubeba silaha za nyuklia

.
    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Viongozi wa Marekani, China na Urusi walipowasili katika mji wa Shenzhen, kusini mwa China, siku ya Alhamisi kwa mazungumzo ya pande tatu pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC), mtu mmoja aliyevalia sare za kijeshi za Urusi alivutia macho ya wengi akiwa amebeba mkoba mweusi wa aina ya kipekee.

Kamera ya televisheni ya taifa la Urusi ilipomkaribia afisa huyo wa jeshi la majini aliyekuwa akisafiri na Rais Vladimir Putin, mwandishi wa habari Yevgeny Popov aliuonyesha mkoba huo na kuwaambia watazamaji kuwa huo ndio mkoba wa nyuklia.

Afisa huyo alitabasamu na kuthibitisha kuwa kweli ulikuwa mkoba huo, unaojulikana kama Cheget, unaompa rais wa Urusi uwezo wa kuwasiliana moja kwa moja na mfumo wa kijeshi unaosimamia silaha za nyuklia za nchi hiyo.

Putin na ujumbe wake kuonekana na kifaa hicho cha kubebea silaha ya nyuklia kimechukuliwa kama ishara ya uwezo wa kijesho. Hata hivyo, Urusi haijatamka kwa kauli iwapo ni kweli Imebeba mkoba wa nyuklia.

Tukio hilo limeibua mjadala kama kiongozi iwe ni Rais ama Waziri Mkuu anaweza kweli kuamuru shambulio la nyuklia akiwa kwenye mkutano wa kimataifa, ndani ya ndege au hotelini.

Mkoba wa nyuklia ni nini hasa?

Z

Mkoba wa nyuklia ni kifaa maalumu cha mawasiliano kinachomuwezesha kiongozi wa nchi kuwasiliana na mfumo wa kijeshi unaosimamia silaha za nyuklia na, inapohitajika, kutuma amri ya matumizi yake.

Mifumo hiyo ilianza kuendelezwa wakati wa Vita Baridi, kipindi ambacho Marekani na iliyokuwa Muungano wa Kisovieti zilikuwa katika ushindani mkubwa wa kijeshi na nyuklia.

Wakati huo, kulikuwa na hofu kwamba shambulio la ghafla la nyuklia lingeweza kutokea ndani ya muda mfupi, hivyo viongozi walihitaji njia ya kuwasiliana na makamanda wa kijeshi hata wakiwa mbali na vituo vyao vya kazi.

Hata hivyo, tofauti na picha inayojulikana ya kiongozi kubonyeza kitufe chekundu na makombora kurushwa mara moja, mchakato huo ni mgumu zaidi.

Mkoba wenyewe haurushi makombora wala kuanzisha shambulio moja kwa moja. Ni sehemu ya mfumo mpana unaohusisha mawasiliano salama, uthibitishaji wa amri na maafisa wa kijeshi wanaohusika katika utekelezaji wake.

'Cheget' inafanya kazi vipi nchini Urusi?

Mkoba wa Urusi unajulikana kama Cheget, jina lililochukuliwa kutoka mlima ulioko katika eneo la Caucasus.

Ulianza kutumika mwaka 1983, wakati wa utawala wa Kisovieti. Kwa utaratibu wa kawaida, afisa wa jeshi la majini ndiye anayebeba mkoba wa rais.

Cheget inaunganishwa na mfumo wa mawasiliano na udhibiti wa kijeshi wa Urusi unaojulikana kama Kazbek. Kupitia mfumo huo, rais anaweza kuwasiliana na uongozi wa kijeshi na kutuma amri inayohusu matumizi ya silaha za nyuklia.

Inaripotiwa kuwa Urusi ina mikoba mitatu ya aina hiyo, inayohusishwa na rais, waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi.

Kwa mujibu wa sera ya nyuklia ya Urusi, uamuzi wa kutumia silaha hizo uko mikononi mwa rais. Hata hivyo, mkoba huo hauwezi peke yake kutekeleza shambulio. Kuna taratibu nyingine za kijeshi zinazohusika katika kupokea na kutekeleza amri.

Kwa nini viongozi husafiri na mikoba hiyo?

A
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Sababu kuu ni kuhakikisha kuwa uwezo wa kuwasiliana na kutoa amri za kijeshi haukatizwi kutokana na mahali alipo kiongozi.

Shambulio la nyuklia linaweza kutokea wakati rais yuko safarini, kwenye mkutano wa kimataifa au hata akiwa hotelini. Katika mazingira kama hayo, kutegemea mifumo iliyopo ndani ya ikulu pekee kunaweza kuwa kikwazo.

Kwa hiyo, mifumo ya aina ya Cheget imeundwa kuhakikisha kuwa kiongozi anaendelea kuwa na mawasiliano na uongozi wa kijeshi wakati wote.

Pia, uwepo wa uwezo huo una umuhimu katika mkakati wa kuzuia mashambulizi ya adui. Mantiki yake ni kwamba nchi inayojua adui wake bado inaweza kujibu shambulio la nyuklia kwa kusitisha kuanzisha shambulio hilo.

Hii ndiyo dhana ya kuzuia mashambulizi kwa tishio la kulipiza kisasi, inayojulikana kama nuclear deterrence.

Kwa maana hiyo, kuonekana kwa afisa aliyebeba Cheget akiwa na Putin nchini China si jambo la kawaida tu la kiusalama. Pia wataalam wa masuala ya usalama wa kimataifa wanaeleza ni jazanda ya uwezo wa Urusi wa nyuklia wakati viongozi wa mataifa makubwa wanajadili mustakabali wa usalama wa dunia.

Je, mataifa mengine yana mikoba kama hiyo?

d

Kwanza, nchi ili iwe na mkoba wa kubebea silaha ya nyuklia lazima iwe inamiliki silaha zenyewe nchini Mwake.

Na pia kuna nchi ambazo zina silaha za nyuklia lakini mfumo wake wa kurusha au kuzuia shambulizi nyuklia haubebwi kwa mkoba.

Si Urusi tu ina mikoba ya siri ya kubeba silaha za nyuklia hata Marekani pia ina mfumo unaofanana unaojulikana kama nuclear football. Ni mkoba maalumu unaosafiri na rais wa Marekani na kumwezesha kuwasiliana na mfumo wa amri za kijeshi kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia.

Hata hivyo, si mataifa yote yenye silaha hizo ambayo yameweka wazi ikiwa viongozi wake husafiri na vifaa vinavyofanana.

Kwa mfano, nchini Uingereza, mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya silaha za nyuklia yako kwa Waziri mkuu. Kila waziri mkuu mpya huandika barua nne zinazojulikana kama Letters of Last Resort, ambazo hupewa makamanda wa manowari nne za nyuklia. Barua hizo zinaelekeza hatua za kuchukua iwapo shambulio la nyuklia litaharibu serikali ya Uingereza na kukatiza mawasiliano na uongozi wake.

Nchini Ufaransa, mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha matumizi ya silaha hizo yako kwa rais.

China nayo inasema inafuata sera ya kutotumia silaha za nyuklia kwanza, ikimaanisha kuwa haitazianzisha dhidi ya nchi nyingine isipokuwa ikiwa imefanyiwa shambulio la nyuklia. Hata hivyo, haijulikani wazi iwapo Rais Xi Jinping husafiri na mkoba maalumu wa nyuklia.

India inasema mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya silaha hizo yako kwa Baraza lake la Kisiasa la Mamlaka ya Amri ya Nyuklia, linaloongozwa na waziri mkuu.

Pakistan na Korea Kaskazini pia zinamiliki silaha za nyuklia, huku Israel ikiaminika kuwa nazo, ingawa haijathibitisha rasmi. Taarifa kuhusu vifaa vinavyotumiwa na viongozi wa mataifa hayo kuwasiliana na mifumo yao ya kijeshi ni chache.

Afrika imechukua msimamo gani kuhusu silaha za nyuklia?

Mkoba wa siri wa kubeba silaha za nyuklia huenda ukawa ni jambo la kushangaza haswa tukirejea hapa barani Afrika.

Ni vigumu serikali barani Afrika kuwa na mikoba ya aina hiyo kutokana na azimio la pamoja la kupiga marufuku nchi yoyote kutengeneza silaha za nyuklia.

Mwaka 1964, viongozi wa iliyokuwa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) walipitisha tamko la kutaka Afrika iwe eneo lisilo na silaha za nyuklia.

Msimamo huo ulifikiwa kupitia Mkataba wa Pelindaba, ulioanza kutumika mwaka 2009.

Chini ya mkataba huo, nchi wanachama zimekubali kutotengeneza, kupata, kumiliki, kuhifadhi au kudhibiti silaha za nyuklia. Pia zimekubali kutofanyia majaribio au kuruhusu kuwekwa kwa silaha hizo katika maeneo yao.

Mkataba huo ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia na kuendeleza lengo la dunia isiyo na silaha hizo.

Hata hivyo, wakati Afrika ikisisitiza msimamo huo, mataifa makubwa yenye silaha za nyuklia yanaendelea kuwa na mifumo ya kijeshi inayowawezesha viongozi wao kuwasiliana na kutoa maamuzi kuhusu matumizi yake.

Kwa hiyo, mkoba wa Cheget si kifaa cha kawaida cha kusafiria. Ni sehemu ya mfumo unaoonyesha jinsi maamuzi kuhusu silaha zenye uwezo wa kusababisha maafa makubwa yanavyoweza kufanywa hata wakati viongozi wako maelfu ya kilomita kutoka vituo vyao vya kijeshi.

Mjadala wa nyuklia

q

Mkutano wa Xi Jinping, Donald Trump na Vladimiri Puti umesheheni kuhusu mustakabali wa silaha za nyuklia duniani.

Kwa sasa, Iran iko katika mzozo na marekani na Israel ikidaiwa kumiliki na kurutubisha urani unaohitajika kutengeneza silaha za nyuklia. Upande wa Israel wanaamini iran kumiliki silaha za nyuklia ni hatari kwa usalama dhidi ya nchi yo huku Iran ikiendelea kusisitiza kuwa haimiliki nyuklia.

Rais wa Marekani Donald Trump na wenzake wa Urusi na China, Vladimir Putin na Xi Jinping, wametoa tamko la pamoja la amani baada ya kufanya mazungumzo ya kihistoria yaliyowakutanisha viongozi hao watatu.

Viongozi hao walikutana kwa muda wa dakika 90 katika mji wa Shenzhen, kusini mashariki mwa China, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC).

Ingawa viongozi hao wamewahi kukutana katika mazungumzo ya ana kwa ana, hii ni mara ya kwanza kwao kukutana katika mazungumzo ya pamoja ya pande tatu.

Katika tamko lao, walisema kuwa vita vya nyuklia haviwezi kushinda na havipaswi kamwe kupiganwa. Pia walieleza kuwa nchi zao zina mpango wa kuongeza uzalishaji na usambazaji wa mafuta ya petroli.

Marekani ina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa silaha za nyuklia za China. Wasiwasi huo umeongezeka pia tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, ambapo Rais Putin aliweka vikosi vya nyuklia vya Urusi katika hali maalumu ya tahadhari, akasitisha ushiriki wa nchi hiyo katika mkataba wa New START wa kudhibiti silaha za nyuklia na kufanya mabadiliko katika mwongozo wake wa matumizi ya silaha hizo.