Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Iran imepoteza udhibiti wa makundi yanayoitii Mashariki ya Kati?
Kulikuwa na mivutano mingi iliyokumba Iraq, Yemen, Syria na Lebanon kwa muda wa miezi kadhaa kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7 iliyopita yaliyofanywa na Hamas dhidi ya Israel na vita vilivyofuata katika Ukanda wa Gaza.
Mivutano hii imezidisha hofu ya kuenea kwa vita katika eneo la Mashariki ya Kati.
Majeshi ya nchi zozote za Kiarabu hayakuwa sehemu ya mivutano hii. Badala yake, suala hilo lilihusishwa na wanamgambo na makundi yenye silaha yaliyo na mafungamano na Iran ambayo yalitoa taarifa za kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza, au kutishia kushambulia maeneo ya Israel au Marekani ili kushinikiza kukomesha vita.
Maendeleo haya yameibua maswali kuhusu undani wa uhusiano kati ya Iran na makundi haya. Wakati baadhi ya watu wakiamini kwamba Tehran imepoteza "udhibiti" juu ya makundi hayo, wengine wanasisitiza kuwa ushawishi mkubwa wa Tehran juu ya makundi hayo haujapungua, wakati baadhi wakisema kuwa makundi hayo, licha ya msaada wa Iran kwa ajili yao, wana Itikadi moja inayonufaika na kiwango fulani cha uhuru.
"Mhimili wa upinzani"
Iran daima imekuwa mdau muhimu katika eneo, lakini mikakati yake ilibadilika sana baada ya Mapinduzi ya Kiislamu yaliyompindua Shah mwaka 1979. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980, imekuwa ikitaka kuimarisha uhusiano wake na makundi yenye silaha katika eneo hilo, wengi wakiwa ni Shia, na wanaoegemea utawala wa Rais wa zamani wa Syria Hafez al-Assad.
Lakini ushawishi wa kikanda wa Iran ulipanuka kwa kiasi kikubwa kufuatia uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003, ambao ulimpindua adui mkuu wa Iran, hayati Rais wa Iraq Saddam Hussein, pamoja na bei ya juu ya mafuta.
Barbara Slavin, msomi katika Taasisi ya Utafiti ya Stimson ambaye ameandika vitabu na tafiti nyingi kuhusu Iran na Mashariki ya Kati, anasema, "Malengo ya Iran kimsingi ni ya kujihami. Inataka kuwa na uwezo wa kutetea utawala wake dhidi ya kuingiliwa na mataifa ya kigeni, na kuwa na sauti katika maamuzi ya kikanda." Inazuia au kupunguza hatua zozote zinazoenda kinyume na maslahi ya Iran.”
Muungano kati ya Iran na makundi yanayoipinga Israel na ushawishi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, kama vile kundi la Hamas, Hezbollah ya Lebanon, wanamgambo wa Iraq, kundi la Houthi nchini Yemen, pamoja na utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad sasa wanaitwa “mhimili wa upinzani”.
Uhusiano mgumu na Hamas
Katika wiki zilizofuata shambulio la Oktoba 7, wataalam na waangalizi walikuwa na maoni tofauti kuhusu kama Iran ilikuwa na ufahamu kuhusu mpango wa Hamas. Jarida la Marekani Wall Street Journal lilidai kuwa mamia ya wanachama wa Hamas walipata mafunzo maalum nchini Iran katika wiki chache kabla ya shambulio hilo, na kwamba Iran ilisaidia kupanga hilo, madai ambayo yalikanushwa na Tehran, ambayo ilithibitisha kuwa haikuwa na jukumu lolote katika shambulio hilo. Vyanzo vya kijasusi vya Marekani pia vilionyesha kuwa shambulio hilo liliishangaza Iran.
Lakini Tehran haikukataa kutoa msaada wa kijeshi kwa Hamas. Akizungumza na NBC News mwezi uliopita, Amir Saeed Ivani, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisema: "Kuhusiana na Palestina, tunawatumia silaha na kuwapa mafunzo."
Kufuatia Mapinduzi ya Kiislamu, sera za kigeni za Iran kwa Israel na Wapalestina zilibadilika. Baada ya kuwepo ushirikiano wa kiusalama kati ya Shah Mohammad Reza Pahlavi na Israel, Tehran ilianza kuzungumzia uungaji mkono wake kwa a Palestina na kuiona Israel kama " upande inaoikalia kwa mabavu" na "adui wa Uislamu," na kuiona kuwa ni "shetani mdogo" na Marekani, ambayo kwa maoni yake iliwakilisha “shetani mkubwa”.
Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina wakati huo, Yasser Arafat, alikuwa mtu wa kwanza wa kimataifa kuitembelea Iran baada ya mapinduzi na kukutana na kiongozi wake, Ayatollah Khomeini.
Kulikuwa na muungano dhaifu kati ya Tehran na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina, uliogubikwa na tofauti za kiitikadi kati ya tabia ya kidini ya Jamhuri ya Kiislamu na mielekeo ya kilimwengu ya Jumuiya hiyo, na vile vile uhusiano kati ya baadhi ya vipengele vya Jumuiya hiyo na utawala wa marehemu rais Saddam Hussein Saddam Hussein. Tehran ilisitisha uungaji mkono wake kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina baada ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Amani ya Oslo mwaka 1993, ambayo ilipinga vikali.
Kwa upande mwingine, Tehran ilijipata katika vuguvugu la Kiislamu la Hamas, ambalo liliundwa mwaka 1987, kama anayeweza kuwa mshirika wa siku za usoni, licha ya tofauti za kiitikadi kati ya utawala wa Kishia wa Iran na vuguvugu la Palestina linalofuata madhehebu ya Sunni, na uhusiano kati yao ulizidi kuimarika zaidi.
Lakini uhusiano huo ulidorora kufuatia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria mwaka 2011, kwa vile Hamas ilikataa kumuunga mkono Rais Bashar al-Assad, mshirika wa karibu wa Tehran, na msaada wa kijeshi wa Iran kwa harakati hiyo ulipungua na misaada ya kifedha kusimamishwa.
Maelewano kati ya pande hizo mbili yalirejea tena polepole, na yaliimarishwa baada ya Washington kujiondoa kutoka kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran mnamo 2018, na nchi kadhaa za Kiarabu zikaelekea kurekebisha uhusiano wao na Israeli.
Uhusiano na Hezbollah
Slavin anaamini kuwa, moja ya sababu za uhusiano mkubwa kati ya kundi la Hezbollah na Iran ni uhusiano wa karibu uliojengeka kati ya Mashia wa Lebanon na wapinzani wa Iran waliokimbilia Lebanon kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Kufuatia uvamizi wa Israel dhidi ya Lebanon mwaka 1982 na kuikalia kwa mabavu kusini mwa nchi hiyo, kuundwa kwa Hizbullah, au "Upinzani wa Kiislamu" kama ilivyokuwa ikijulikana wakati huo, ilitangazwa, chombo cha kisiasa cha Shia. Tangu kuasisiwa kwake, kundi hilo limemchukulia Kiongozi Mkuu wa Irani kuwa "mamlaka yake ya kisheria," na kilikuwa moja ya vikundi vya kwanza vyenye silaha kupokea msaada wa kifedha na kijeshi wa Iran katika eneo hilo. Katika miongo minne iliyofuata, pande zote mbili zilibaki kuwa wafuasi wenye nguvu.
Maafisa wa Iran na Hezbollah wamezungumza mara kwa mara kuwa pande hizo mbili zinashauriana kuhusu maamuzi muhimu zaidi ya kijeshi na kisiasa. Wale wanaofahamu masuala ya Iran wanaamini kwamba Wairani huwa wanashauriana na Katibu Mkuu wa kundi hilo, Hassan Nasrallah, na wanaamini tathmini yake ya mambo katika eneo hilo, hasa kuhusu mzozo na Israel.
Uhusiano mkubwa kati ya Hezbollah na Hamas ulishuhudia kipindi cha baridi, kama ilivyotokea kati ya Iran na Hamas, kufuatia kuhusika kwa Hezbollah katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria pamoja na jeshi la Syria, ambalo lilikosolewa na Hamas, ambayo iliunga mkono upinzani. Hata hivyo, maafisa wa Hamas walithibitisha katika miezi michache kabla ya shambulio la Oktoba 7 kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili umeanza kurejea katika hali ya kawaida.
Makabiliano kati ya Hezbollah na Israel yameongezeka baada ya shambulio la Oktoba 7 na vita ambavyo Israel inasema inaendesha dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, hasa katika kipindi cha wiki chache zilizopita, jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa hofu ya kutokea kwa vita vipya kati ya pande hizo mbili.
Nasrallah alipongeza shambulio la Hamas dhidi ya Israel, akisema kwamba "lilianzisha awamu mpya ya mzozo kati ya Israel na watu wa Palestina," na kuzitaka serikali za Kiarabu na Kiislamu kujitahidi kusimamisha mapigano.
Wanamgambo wa Iraq na kuvuka "mstari mwekundu"
Iran imekuwa na uhusiano wa karibu na makundi yenye silaha ya Kishia ya Iraq kwa muda mrefu, huku Tehran ikiwaunga mkono wapinzani wa Kishia wa Iraq waliokimbilia humo mwanzoni mwa miaka ya 1980. Kufuatia uvamizi wa Marekani uliompindua Saddam Hussein mwaka 2003, Iran ilianzisha uhusiano wa karibu na serikali ya Baghdad na idadi kubwa ya wanamgambo wa Kishia wenye silaha ambao baadaye waliiunda Iraq.
Baada ya shambulio la Oktoba 7, uhusiano huu uliibuka tena, na majeshi ya Marekani nchini Iraq yakikabiliwa na mashambulizi kadhaa ya wanamgambo wa Iraq na makundi yenye silaha ambayo yalipinga uwepo wa Marekani nchini humo.
Washington ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya makundi ya Iraq, ikiwa ni pamoja na "Popular Mobilization Forces" na "Harakat al-Nujaba" chini ya bendera yake, ambayo Katibu Mkuu Akram al-Kaabi anachukuliwa kuwa mmoja wa wapinzani mashuhuri wa uwepo wa Amerika nchini Iraq. Kufuatia mauaji ya wanachama wa Hashd katika uvamizi wa Marekani mwezi Novemba mwaka jana, Al-Kaabi alitoa wito wa "kutangaza vita dhidi ya Marekani" na kuondoa majeshi yake kutoka Iraq.
Wachambuzi wanaamini kuwa kuna "mstari mwekundu" ambao haujatangazwa katika sheria za mzozo wa Iran na Marekani, ambayo ni kwamba Iran au wanamgambo wanaoshirikiana nayo hawapaswi kuua raia wa Marekani. Hata wakati Qasem Soleimani, kiongozi mashuhuri wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, aliuawa katika shambulio lililofanywa na ndege isiyo na rubani ya Marekani, jibu la Iran ambalo lililenga kambi ya Wamarekani huko Iraq halikusababisha kupoteza maisha kwa Wamarekani.
Lakini mstari huu mwekundu ulivukwa mwishoni mwa Januari wakati shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani cha "Tower 22" huko Jordan, karibu na mpaka na Syria, na kusababisha kifo cha askari watatu wa Marekani na wengine 34 kujeruhiwa.
Jibu la Marekani lilikuja kwa kuanzisha mashambulizi dhidi ya "vituo vya Iran" nchini Syria na Iraq.
Houthi na uhusiano mwingine "mgumu"
Mizizi ya kimafundisho ya vuguvugu la Ansar Allah Houthi inarejea kwenye fundisho la Uislamu wa Kishia Zaidi, ambalo linatofautiana na fundisho la Twelver doctrine lililoenea nchini Iran.
Kiongozi wa kwanza wa kundi hilo, Hussein Badr al-Din al-Houthi, aliathiriwa na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, fikra ya uongozi wa kisiasa wenye uhalali wa kidini, na upinzani dhidi ya ukoloni na Uzayuni.
Harakati hiyo inapitisha baadhi ya kauli mbiu za mapinduzi ya Iran, kama vile "Kifo kwa Amerika" na "Kifo kwa Israeli.
Vuguvugu hilo liligeuka kuwa kundi lenye silaha mwaka 2004, ambalo pia lilishuhudia mauaji ya Hussein al-Houthi, na kaka yake mdogo, Abdul Malik, akamrithi katika uongozi. Harakati hiyo ilipigana vita vingi na serikali ya Rais wa zamani Ali Abdullah Saleh, na Wahouthi waliimarisha nafasi na ushawishi wao nchini humo baada ya kuanguka kwa Saleh mwaka 2012, na wafuasi wake wakageuka kuwaunga mkono kijeshi.
Licha ya uhusiano mkubwa kati ya Iran na Houthi, na Tehran kuimarisha uwezo wao wa kijeshi, ambayo ni pamoja na makombora ya masafa marefu, makombora ya kukinga meli, na ndege zisizo na rubani, wachunguzi wa mambo wanabainisha kuwa uhusiano huo unatofautiana na uhusiano wa Iran na Hezbollah, kwa mfano, kutokana na kuwepo kwa tofauti za kimadhehebu, na ikizingatiwa kwamba Wahouthi, kwa maoni yao, hawatafuti kuchukua jukumu, lakini badala ya kuzingatia hali yao ya ndani.
Kwa hakika, Wahouthi wamekuwa sehemu ya vita, wakianzisha mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya meli za kibiashara na kijeshi za Magharibi tangu katikati ya mwezi wa Novemba, wakisema kwamba mashambulizi hayo yanalenga kuwaunga mkono Wapalestina.
Mashambulizi haya yalitatiza usafiri wa meli katika maji ya Bahari Nyekundu na Mfereji wa Suez, na kusababisha baadhi ya makampuni kuelekeza meli na makontena yao kwenye njia ndefu na ya gharama zaidi ya Cape of Good Hope.
Marekani na Uingereza zilijibu kwa kuanzisha mashambulizi mwezi uliopita dhidi ya Houthi katika maeneo wanayodhibiti magharibi mwa Yemen.
Qassem Soleimani na kiunganisha kilichopotea
Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba mauaji ya Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, ambaye anasifiwa kwa kuanzisha na kusimamia “Mhimili wa Mapambano,” yaliathiri pakubwa uwezo wa uratibu na uhamasishaji wa Iran na wanamgambo wa Mhimili wa Mashariki ya Kati. Soleimani alikuwa na uhusiano wa karibu na wanamgambo hawa na uzoefu mkubwa katika kanda.
"Wairani wanasema kuwa uratibu kati ya wanachama wa Mhimili wa Upinzani ulikuwa na nguvu zaidi wakati Qasem Soleimani alipokuwa hai, na hilo linaonekana kuwa sawa , ikizingatiwa kwamba Soleimani alizungumza Kiarabu fasaha na kimsingi ndiye aliyeunda mhimili huo," Slavin anasema. "Mrithi wake [Ismail Qaani] ni zaidi ya mtaalamu wa Afghanistan." "Uzoefu wake katika ulimwengu wa Kiarabu unamaanisha kuwa wanachama wa mhimili huo wanaweza kuchukua hatua kwa uhuru zaidi, na inakuwa vigumu kwa mamlaka yoyote kuwadhibiti.
Lakini Michael Knights anaamini kwamba kila wanamgambo au kikundi "kina uhusiano tofauti kidogo na Kikosi cha Quds, na hakuna hata mmoja wao anayeweza kuchukua hatua kwa uhuru kwa njia zinazodhuru usalama wa Iran. Vikundi vyote vinaelewa nini wanapaswa kufanya na nini hawapaswi kufanya. Iran ina malengo ya kiitikadi na mkataba wa ulinzi." Inashiriki na wanachama wa mhimili wa upinzani, na kwa hivyo ni nadra sana kwa masilahi ya Iran kutofautiana na masilahi ya Hezbollah, wanamgambo wa Iraq au Houthi.
Licha ya mitazamo tofauti kuhusu ukubwa wa ushawishi wa Iran miongoni mwa wanamgambo wanaoitii au wanaofungamana nayo katika Mashariki ya Kati, kunakaribia makubaliano kwamba haitaki kupanua wigo wa vita au kuingia katika mzozo wa moja kwa moja na Marekani na Israel - jambo ambalo Tehran imethibitisha kwa zaidi ya tukio moja.
Lakini wakati huo huo, inaweza kupata ugumu kukatisha tamaa vikundi vya "Axis of Resistance" kuanzisha mashambulizi dhidi ya Amerika au Israel kwa sababu hiyo ingekinzana na misimamo yao iliyotangazwa na dhana ya "upinzani." Kila kundi pia hujikuta wakati mwingine linalazimika kuchukua hatua ndani ya muktadha wa hali ya nchi yake na hali ya ndani.
Mawazo haya yote yanaongeza hali ya kutokuwa na uhakika juu ya mustakabali wa hali katika eneo hilo, katika kipindi ambacho afisa wa Marekani alisema katika taarifa kwamba "labda kilikuwa kipindi ngumu zaidi ambacho eneo hilo limeshuhudia.
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi