Ukimya wa Al Qaeda juu ya vita vya Iran, Marekani na Israel una maana gani?

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Al-Qaeda imekuwa kimya sana kuhusu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilivyoanza Februari 28. Hili si jambo la kawaida, kwani al-Qaeda na wafuasi wake kwa kawaida wamekuwa wakijihusisha na matukio makubwa ya Mashariki ya Kati.

Hasa wakati ambapo migogoro kama hiyo inajadiliwa ndani ya makundi yenye msimamo mkali.

Mwaka huu, kauli moja tu ilitoka kwa uongozi mkuu wa Al-Qaeda, Februari 4, wakati ambapo Marekani ilikuwa ikiongeza uwepo wake wa kijeshi Mashariki ya Kati, kufuatia mvutano na Iran.

Taarifa yake ilitoa wito wa kufanyika mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani na Israel, na mashirika mengi yenye msimamo mkali yaliiona taarifa hiyo kama ya kuuunga mkono Iran kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Lakini hakujawa na kauli nyingine zaidi ya hiyo. Kundi hilo kwa sasa liko katika hali ngumu. Kiongozi wake, Saif al-Adl, na washirika wake wa karibu wanaaminika kuishi Iran kwa mujibu wa FBI.

Baada ya mashambulizi ya 9/11, viongozi wengi muhimu wa Al-Qaeda na familia zao walikimbia Afghanistan na Pakistani na kwenda Iran.

Kwa upande mwingine, al-Qaeda huenda inakwepa kuikera Iran, ndiyo maana haijajiunga waziwazi na makundi yenye msimamo mkali ambayo kwa kawaida huonya juu ya kuunga mkono Iran yenye Washia wengi.

Makundi kadhaa kama yenye mismamo mikali yamewataka Waislamu wa Sunni kwa kauli moja kutojihusisha na upande wowote.

Pia shirika hilo huenda limechukua mkakati wa kuepuka kutoa matamshi zaidi dhidi ya Marekani au Israeli, kama lilivyofanya Februari 4.

Kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kuonekana kama kuiunga mkono Iran kwa njia isiyo ya moja kwa moja, jambo ambalo linaweza kuharibu sifa yake miongoni mwa wafuasi wake.

Kwa upande wa itikadi, Washia wa Iran wanachukuliwa kuwa maadui wa jadi wa Waislamu wa Sunni.

Al-Qaeda walikuwa kimya wakati wa vita vya siku 12 vya Marekani na Israel dhidi ya Iran Juni 2025.

Kwa upande mwingine, ISIS, ambayo inaonekana kama mpinzani wa Al Qaeda, haijakaa kimya na imekosoa vikali pande zote mbili.

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu lilisema wito wa Al-Qaeda wa kufanya 'jihad' dhidi ya Marekani uliotolewa Februari 4 ni 'uthibitisho' kwamba Al-Qaeda inazidi kuwa 'mshirika dhaifu wa Iran.

Ukimya wa viongozi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Al-Qaeda pia imekuwa kimya kwa muda mrefu kuhusu uongozi wake, na ukimya wake kuhusu mzozo nchini Iran pia unahusiana na hili.

Al-Qaeda haijamtaja kiongozi wake mkuu kwa umma tangu Julai 2022. Hii ilikuwa wakati Marekani ilipotangaza kuuawa kwa Ayman Al-Zawahiri, kiongozi wa kundi hilo wakati huo, ambaye aliuawa katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Ingawa kuna ripoti za ndani kuwa naibu kiongozi wa kundi hilo, Mmisri Saif al-Adl, amechukua uongozi wa kundi hilo.

Hata hivyo, al-Qaeda haijawahi kuthibitisha au kukataa rasmi ripoti hizi, ingawa makundi ya jihadi na wafuasi wao wamekiri kwamba Ayman al-Zawahiri amekufa na Saif al-Adl amechukua uongozi.

Inawezekana kwamba Al-Qaeda walichagua ukimya huu ili wasiiweke Taliban ambayo ni mshirika, katika hali ngumu.

Wakati huo huo, pia inataka kujibu swali gumu la kama viongozi wake wapya wanaishi Iran, kwani makundi ya kijihadi ya kiSunni yanaiona Iran kama adui mkubwa.

Hapo awali, vyanzo vya ndani vya Al-Qaeda pia vilithibitisha kwamba baadhi ya viongozi wakuu wa shirika hilo wako Iran.

Tangu mwaka 2022, kundi linalojiita Islamic State limekuwa likiishutumu Al-Qaeda kwa kuwa chini ya Iran na kutaja uwepo wa Saif al-Adl nchini Iran kama ushahidi.

Wafuasi wa Al-Qaeda wamejaribu kutoa maelezo tofauti kujibu kadhaa hiyo, wakidokeza kwamba fedha za shirika hilo ni chache na Saif al-Adl alikuwa chini ya kifungo cha nyumbani au alizuiliwa kuondoka Iran.

Licha ya tofauti za kiitikadi na Iran, baadhi ya wanachama ndani ya al-Qaeda wanaweza kuhalalisha uhusiano wa kimkakati na Iran.

Hamas ilifanya vivyo hivyo, na asili yake imetokana na Udugu wa Kiislamu.

Utata

Mwaka huu, ni kauli moja tu ndio imetoka kwa kiongozi mkuu wa Al-Qaeda, ikiwataka Waislamu kuchukua hatua dhidi ya uwepo wa wanajeshi wa Marekani huko Mashariki ya Kati.

Lakini matawi ya kikanda ya shirika hilo hayakutoa taarifa yoyote kuhusu vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

Hata Al-Qaeda katika Rasi ya Arabia (AQAP), tawi la Yemen la Al-Qaeda, ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kusukuma Jihadi Duniani kote katika miaka ya hivi karibuni halijazungumza.

Ni tawi la Asia Kusini pekee lililotoa maoni yake kuhusu jambo hili, katika makala iliyochapishwa katika jarida la AQIS la 'Nawa'i Ghazwat-ul-Hind' Machi 8, ambayo ilionyesha hisia za chini za kuipendelea Iran.

Mara nyingi Al-Qaeda hutoa matamko kwa matukio makukubwa yanayotokea katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa mfano, Al-Qaeda imetoa taarifa ya wazi kuhusu mzozo huko Gaza, huku kundi la Islamic State likionekana kutotoa tamko lolote. Baadhi ya kauli za Al Qaeda kuhusu mzozo wa Gaza zinaunga mkono Hamas.

Kufuatia salamu za rambirambi kwa vifo vya viongozi wa Hamas, kundi linalojiita Dola la Kiislamu liliishutumu Al-Qaeda kwa kushawishiwa na Iran.

Kwa kuzingatia hali hii nyeti, al-Qaeda kwa ujumla imeepuka kuisifu Hamas yote hadharani, badala yake hulenga kuzungumzia 'Mujahidina' wa Palestina au tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Izz ad-Din al-Qassam.

Al-Qaeda na washirika wake walikuwa kimya wakati wa vita vya siku 12 kati ya Marekani na Israeli kuhusu Iran Juni 2025, lakini wakati huu ukimya unaongezeka.

Makundi mengi yenye msimamo mkali yamesisitiza kwamba kuiunga mkono Iran si sahihi. Hata hivyo, kuna makundi ya Kiislamu yanayozungumza kuiunga mkono Iran, lakini idadi yao ni ndogo.

Makundi yanayounga mkono Al Qaeda

ol

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Osama bin laden na al Zawahiri

Machi 1, siku mbili baada ya vita kuanza, kundi la kijihadi liliibuka likijiita 'Ajnad Bayt al-Maqdis' (Askari wa Jerusalem). Inaaminika kundi hilo linafanya kazi nchini Syria na limetangaza utiifu kwa al-Qaeda.

Kundi hilo limesema kuibuka kwake kumetokana na ombi la al-Qaeda, kupitia ujumbe wa Februari 4.

Baadaye, kundi hilo jipya lilidai kufanya mashambulizi manne madogo dhidi ya vikosi vya Marekani na Israel ndani na karibu na Syria.

Hadi leo, al-Qaeda haijakubali kauli za Ajnad Bayt al-Maqdis na haijatambua au kuunga mkono tamko lake la utii.

Wafuasi wa kundi linalojiita Islamic State wamelikataa kundi hilo, wakilielezea kama kundi linaloungwa mkono na Iran.

Baadhi ya wafuasi wanasema ikiwa kundi hilo linaunga mkono au lina uhusiano na al-Qaeda, itaimarisha madai yao kwamba al-Qaeda sasa inatekeleza maagizo ya Iran.

Tuhuma hizi ziliimarishwa zaidi baada ya makundi ya Washia wanaounga mkono Irani yaliyopo nchini Syria pia kudai kuhusika na baadhi ya mashambulizi yaliyodaiwa na kundi hili jipya.