Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nchi ambayo kuwa na mnyama kipenzi kunaweza kukuweka jela hivi karibuni
"Ananiangalia kwa macho yake mazuri yasiyo na hatia. Anataka nimtoe nje tukatembee, lakini siwezi kuthubutu. Tutakamatwa."
Mahsa, mfugaji mbwa kutoka Tehran, anaashiria wimbi jipya la kukamatwa kwa watu wanaofuga wanyama na kuzuiliwa kwa wanyama wao katika jiji hili.
Polisi katika mji mkuu wa Iran hivi karibuni wametangaza kwamba mbwa wanaotembea katika bustani za jiji hilo ni "uhalifu".
Marufuku hiyo ilihalalishwa kama hatua ya "kulinda usalama wa umma".
Faini
Kwa mujibu wa kanuni ya sheria mpya iliyopendekezwa, umiliki wa wanyama utakuwa chini ya kibali kilichotolewa na kamati maalum.
Sheria hiyo pia inapendekeza faini ya chini ya dola 800 za kimarekani kwa "kuagiza, kununua na kuuza, usafirishaji na ufugaji" wa aina mbalimbali za wanyama, ikiwa ni pamoja na wanyama wa kawaida wa nyumbani kama vile paka, kasa na sungura.
Mijadala kuhusu mswada huu ilianza zaidi ya muongo mmoja uliopita wakati kundi la Wabunge wa Iran lilipojaribu kuhimiza sheria ya kuwachukua mbwa wote na kuwapeleka kwenye mbuga za wanyama au kuwaacha jangwani," Dkt Payam Mohebi, rais wa Chama cha Wataalamu wa Mifugo wa Iran anayepingamswada huo, aliiambia BBC.
"Kwa miaka mingi, wamebadilisha hili mara kadhaa na hata kujadili adhabu ya viboko kwa wamiliki wa mbwa. Lakini mpango wao haukufika popote," Dkt Mohebi aliongeza.
Ishara ya Maisha ya mjini ya Iran
Ufugaji wa mbwa umekuwa jambo la kawaida katika maeneo ya vijijini nchini Iran, lakini wanyama hao pia wakawa ishara ya maisha ya mijini katika Karne ya 20.
Iran ilikuwa mojawapo ya nchi za kwanza katika eneo la Mashariki ya Kati kupitisha sheria za ustawi wa wanyama mwaka wa 1948, na serikali ilifadhili taasisi ya kwanza ya kuimarisha haki za wanyama.
Hata familia ya kifalme ya nchi ilikuwa na mbwa wao.
Lakini mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 yalibadilisha nyanja nyingi za maisha kwa raia wa Irani na mbwa.
Wanyama hao wanachukuliwa kuwa najisi katika utamaduni wa Kiislamu.
Kwa utawala mpya, mbwa pia wakawa ishara ya utamaduni wa "magharibi" ambayo mamlaka ilitaka kudhibiti.
"Hakujawa na udhibiti thabiti kuhusu umiliki wa mbwa," Dkt Ashkan Shemirani, daktari wa mifugo anayeishi Tehran, aliiambia BBC.
"Vikosi vya polisi vinakamata watu kwa kuwatembeza mbwa wao au hata kuwabeba kwenye magari yao kulingana na tafsiri yao ya kile kinachoweza kuonekana kama ishara za ughaibuni."
Jela za mbwa
"Hata walibuni gereza la wanyama, na tulisikia hadithi nyingi za kutisha kutoka huko," aliongeza.
"Wanyama hao walifugwa kwa siku nyingi katika maeneo ya wazi bila chakula wala maji bora huku wamiliki wa mbwa wakibiliwa na kila aina ya matatizo ya kisheria."
Matatizo ya kiuchumi ya Iran kufuatia miaka ya vikwazo vya nchi za Magharibi pia yamechangia kubuniwa kwa mswada huo mpya.
Mamlaka imepiga marufuku uagizaji wa chakula cha mifugo kutoka nje kwa zaidi ya miaka mitatu kama sehemu ya harakati za kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni nchini humo.
Katika mazingira yaliyotawaliwa na chapa za bidhaa za kigeni, hali hiyo ilimaanisha kupanda kwa bei, hasa baada ya kuanzishwa kwa soko la kisiri.
"Tunategemea sana watu wanaosafirisha chakula kinyemela," mmiliki wa kliniki ya mifugo katika jiji la Mashhad aliambia BBC.
"Bei sasa ni mara tano kuliko ilivyokuwa miezi michache iliyopita."
Mmiliki wa biashara anadai kuwa chakula kinachozalishwa nchini hakijafikia kiwango kinachihitajika.
Viwanda hutumia nyama ya bei nafuu au samaki, hata viungo vilivyoisha muda wake.
Shida ya paka
Lakini sheria mpya sio tu inalenga mbwa. Paka pia wamejumuishwa kwenye orodha ya wanyama - hata mamba wanatajwa.
Iran inajulikana kama mahali pa kuzaliwa kwa paka wa Uajemi, mojawapo ya mifugo maarufu zaidi duniani.
"Je, unaweza kuamini kwamba sasa paka za Kiajemi haziko salama katika nchi yao?" daktari wa mifugo anayeishi Tehran aliiambia BBC.
"Hakuna mantiki nyuma ya sheria hii. Watu wenye msimamo mkali wanataka kuonyesha ngumi za chuma kwa watu," waliongeza.
Dkt Mohebi, Rais wa Chama cha Madaktari wa Mifugo wa Iran, anaita sheria inayopendekezwa kuwa "ya aibu".