Simulizi ya kijana aliyempeleka kuku wake mgonjwa hospitalini ilivyobadili maisha yake

.

Chanzo cha picha, Omar Chan

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Kijana mwenye umri wa miaka 12 kutoka Ethiopia amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kuchukua hatua isiyo ya kawaida ya kumpeleka kuku wake mgonjwa katika hospitali inayotibu binadamu ili apatiwe matibabu.

Markos Abaaye, ambaye hivi karibuni alihamia mji wa Denbecha kutoka kijijini kwa ajili ya kuendelea na masomo, alisafiri akiwa na kuku aliyekuwa amepewa na familia yake. Kuku huyo alikuwa wa thamani kubwa kwake, kiasi kwamba alimchukulia kama sehemu ya familia.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kufika mjini, kuku huyo alianza kuugua. Markos alijaribu kila alichoweza kumsaidia, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya. Akiwa hana suluhisho jingine, aliamua kumpeleka hospitali.

"Nilidhani hospitali ni mahali ambapo viumbe wote wagonjwa wanaweza kutibiwa," Markos alinukuliwa akisema.

Tukio hilo lilitokea katika Hospitali ya Denbecha, ambako muuguzi Omar Chan alimwona kijana huyo akiwa amembeba kuku wake kwa huzuni kubwa usoni.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo, watu wengi waliokuwepo hospitalini walishangazwa na kitendo hicho, huku baadhi wakijaribu kumcheka. Lakini yeye aliona jambo tofauti.

"Niliona huruma kubwa kwenye uso wa mtoto huyo. Alikuwa na wasiwasi wa kweli kuhusu afya ya kuku wake. Hakukuwa na mzaha katika alichokuwa akifanya," alisema.

Muuguzi huyo alirekodi video fupi akizungumza na Markos kuhusu sababu ya kumleta kuku hospitalini. Katika video hiyo, kijana huyo alieleza kuwa kuku wake alikuwa akilia na kuonyesha dalili za maumivu, jambo lililomfanya kuamini kuwa anahitaji matibabu ya haraka.

Baada ya kufafanuliwa kuwa hospitali hiyo hutibu binadamu pekee, Markos alielekezwa kwenda kwa wataalamu wa mifugo.

.

Chanzo cha picha, Omar Chan

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Video hiyo iliposambazwa kwenye mtandao wa TikTok, maelfu ya watu waliguswa na upendo na huruma aliyoonyesha kwa mnyama wake. Ndani ya muda mfupi, simulizi yake ikawa maarufu nchini Ethiopia na nje ya mipaka yake.

Baba yake mlezi, Ato Kelemework Amogene, alisema familia ilishangazwa na umaarufu huo kwani hawakujua hata kwamba Markos alikuwa amekwenda hospitalini.

"Hakutuambia alikokwenda. Tulisikia habari hizo siku kadhaa baadaye kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii," alisema.

Aliongeza kuwa Markos amekuwa na mapenzi makubwa kwa kuku tangu akiwa mdogo. Akiwa kijijini, alikuwa akiwatunza sio kuku wake pekee, bali hata wa majirani. Wakati mwingine aliwalisha na kuwahudumia alipobaini kuwa walikuwa wagonjwa.

"Anawapenda sana. Hata chakula chake wakati mwingine anakigawanya ili wale pamoja naye," alisema.

Umaarufu wa Markos uligeuka kuwa baraka baada ya makampuni na watu kadhaa kumzawadia zawadi mbalimbali, ikiwemo kuku ambapo kampuni ya Trust Agro ilimzawadia vifaranga vya kuku 100 kutokana na moyo wake wa kujali wanyama.

Mbali na zawadi hiyo, taasisi hiyo iliahidi kugharamia malazi, chakula na mafunzo maalumu ya ufugaji wa kuku kwa kijana huyo ili kumsaidia kupata maarifa zaidi kuhusu afya, lishe na tabia za ndege hao.

Mwanzilishi wa taasisi hiyo, Dk. Abunu Andarge, alisema kitendo cha Markos kinaonyesha umuhimu wa kuwafundisha watoto huruma kwa viumbe hai.

"Chochote ambacho watu wanaweza kusema kuhusu tukio hili, sisi tumeona moyo wa kipekee wa mtoto anayejali maisha ya kiumbe mwingine. Huo ni mfano mzuri kwa jamii," alisema.

Leo, Markos anaendelea na masomo yake huku akiwa na matumaini ya kuwa mfugaji bora siku zijazo. Na ingawa kuku aliyempeleka hospitalini amepona, simulizi yake imeacha somo kubwa kwa wengi: kwamba huruma kwa viumbe hai inaweza kubadili maisha kwa njia ambayo mtu hakutarajia.