Marekani na Israel zinajiandaa kushambulia tena Iran -ripoti
Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na CBS, Rais wa Marekani Donald Trump bado hajatoa amri ya mwisho ya kuanzishwa kwa mashambulizi hayo.
Muhtasari
- Mwanajeshi wa Israel ajeruhiwa katika mapigano na Hezbollah
- Uhispania yalaani matamshi ya 'ubinafsi' wa baadhi ya nchi za EU kuhusu wahamiaji wanaovukia Ceuta
- Mamlaka za Tigray zatangaza kuzuka kwa mapigano mapya Magharibi mwa jimbo hilo
- Viongozi wa Afrika wataka muda wa vikosi vya AU Somalia uongezwe
- UEFA yafurahia FIFA kuachana na mpango wa kuuza hisa za Kombe la Dunia
- Askofu Mkuu wa Canterbury awasili Cameroon kwa ziara ya kichungaji
- Maafisa tisa wa Ukraine wauawa katika shambulizi la Urusi mjini Kyiv
- Kifaa kisichojulikana chagonga meli ya mafuta karibu na Oman
- FIFA yafuta mpango tata wa uwekezaji wa Kombe la Dunia
- Marekani na Israel zinajiandaa kushambulia tena Iran - ripoti
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi
Mwanajeshi wa Israel ajeruhiwa katika mapigano na Hezbollah

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Israel limetangaza kuwa mmoja wa wanajeshi wake alijeruhiwa jana usiku wakati wa "makabiliano ya karibu" na vikosi vya Hezbollah kusini mwa Lebanon, licha ya kusitishwa kwa mapigano.
Jeshi la Israel lilitangaza katika taarifa kwamba mtu aliyejeruhiwa ni afisa wa jeshi.
AFP mjini Beirut inasema iliwasiliana na Hezbollah ili kupata maoni yake kuhusu habari hizo, lakini kundi hilo halikutoa maoni yoyote.
Hezbollah haijadai kuhusika na mashambulizi yoyote kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.
Uhispania yalaani matamshi ya 'ubinafsi' wa baadhi ya nchi za EU kuhusu wahamiaji wanaovukia Ceuta

Chanzo cha picha, Reuters
Uhispania imelaani mwitikio wa "ubinafsi, unaochochea mgawanyiko na usio halali" wa baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kufuatia wimbi la wahamiaji 60,000 walioingia Ceuta wakitokea Morocco.
Maafisa wanasema karibu watu wote waliofika eneo hilo la ng'ambo mnamo tarehe 30 Julai wamesharejea, huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uhispania, Fernando Grande-Marlaska, akisema Jumamosi kuwa idadi ya vifo imefikia takribani 67.
Haya yanajiri baada ya Italia kusitisha kwa muda makubaliano ya Visa ya Schengen ya EU—ambayo huruhusu usafiri bila vizuizi vya mipaka—kuhusiana na Uhispania, huku Waziri Mkuu Giorgia Meloni akielezea matukio hayo kuwa ya "kushtua".
Finland na Denmark ziliunga mkono hatua hiyo ya Italia, huku Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czech, Andrej Babiš, akitoa wito wa kusimamishwa kwa muda uanachama wa Uhispania katika eneo la Schengen.
Katika barua kwa Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez alisema ana "wasiwasi mkubwa" kuhusu baadhi ya serikali za Ulaya.
Alisema serikali ya Uhispania ilikuwa imerejesha kikamilifu udhibiti wa mpaka na kuzuia "harakati zozote zisizoidhinishwa za kuendelea na safari kuelekea bara la Ulaya" ndani ya muda usiozidi saa 48.
Ingawa nchi nyingi zilionyesha "uungaji mkono na mshikamano", Sánchez alisema serikali nyingine za Ulaya zilichagua kuishambulia Uhispania, "zikichochewa na chuki, habari za uongo, ujinga, au maslahi ya kisiasa", na akabainisha kuwa Ceuta si sehemu ya eneo la Schengen.
"Umoja wa Ulaya hauwezi kumudu aina hii ya mwitikio wa ubinafsi, unaochochea mgawanyiko na usio halali," alisema.
Soma pia:
Mamlaka za Tigray zatangaza kuzuka kwa mapigano mapya Magharibi mwa jimbo hilo

Chanzo cha picha, GET
Mamlaka za eneo la Tigray nchini Ethiopia zimetangaza kuwa mapigano yamezuka katika eneo la Magharibi mwa Tigray, zikidai kuwa Vikosi vya Ulinzi vya Taifa vya Ethiopia (ENDF) vimeanzisha mashambulizi mapya ya kijeshi.
Katika taarifa iliyotolewa leo, serikali ya Tigray ilidai kuwa vikosi vya serikali kuu vilianzisha "vita vya wazi tangu alfajiri ya leo" kuelekea eneo la Shererina, katika Ukanda wa Magharibi mwa Tigray. Taarifa hiyo ilisema mashambulizi hayo ni mwendelezo wa kile ilichokiita kuzingirwa, vizuizi na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya eneo hilo.
Chama cha TPLF pia kiliishutumu serikali ya Ethiopia kwa kukiuka Makubaliano ya Amani ya Pretoria yaliyomaliza vita vya Tigray vya mwaka 2020 hadi 2022, kikidai kuwa huduma za kijamii zimezuiwa pamoja na usambazaji wa mafuta, fedha taslimu, huduma za benki na mgao wa bajeti.
Juhudi za kupata maoni kutoka kwa Vikosi vya Ulinzi vya Taifa vya Ethiopia na kitengo cha mawasiliano cha serikali hazikufanikiwa.
Mvutano huu unafuatia miezi kadhaa ya hali ya sintofahamu kati ya serikali ya shirikisho na TPLF, ambayo imekuwa ikiishutumu Addis Ababa kwa kuwapeleka wanajeshi katika mipaka ya Tigray na kujiandaa kwa mzozo mpya.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, hivi karibuni aliishutumu TPLF kwa kushirikiana na Eritrea na Sudan ili kuleta hali ya kutokuwa na utulivu nchini.
Kiongozi wa TPLF, Debretsion Gebremichael, alisema katika mkutano wa hadhara mjini Mekelle tarehe 19 Julai kuwa Tigray ina washirika wanaotaka kuiondoa serikali ya sasa madarakani, ingawa hakutaja ni washirika wa ndani au wa nje.
Katika taarifa ya leo, TPLF imewataka wakaazi wa Tigray waliopo ndani na nje ya nchi, vikosi vya usalama, asasi za kiraia na taasisi za dini kujiandaa kwa mapigano.
Pia imewataka raia kuchukua tahadhari na kuziomba jumuiya za kimataifa kutambua athari zinazoweza kujitokeza iwapo vita vitarejea katika eneo hilo.
Viongozi wa Afrika wataka muda wa vikosi vya AU Somalia uongezwe
Viongozi wa nchi zinazochangia wanajeshi katika vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM) wametaka muda wa operesheni hiyo uongezwe, licha ya Marekani kusitisha uungaji mkono wake wa kisiasa na kifedha.
Marekani imetangaza kuwa itasitisha ufadhili kwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOS), inayotoa huduma muhimu za vifaa na usafiri kwa AUSSOM, mwishoni mwa mwaka huu.
Katika mkutano uliofanyika Kampala, Uganda, viongozi walisisitiza haja ya kuwepo kwa mpango wa miaka miwili wa kuondoa AUSSOM hatua kwa hatua huku majukumu ya usalama yakikabidhiwa kwa vikosi vya Somalia.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema uwezekano wa vikosi hivyo kuendelea ni mdogo kutokana na msimamo wa Marekani.
Wameonya kuwa kuondoka kwa haraka kwa vikosi vya AU kunaweza kusababisha hali kama iliyotokea Afghanistan mwaka 2021, ambapo kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kulifuatiwa na kuanguka kwa serikali.
Somalia imekuwa ikikabiliana na waasi wa Al-Shabaab kwa takriban miongo miwili.
UEFA yafurahia FIFA kuachana na mpango wa kuuza hisa za Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, PA Media
Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limekaribisha uamuzi wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) wa kuachana na mpango wa kuuza hisa katika mashindano yake, yakiwemo Kombe la Dunia, kwa wawekezaji binafsi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, UEFA ilisema:
"UEFA inakaribisha uamuzi wa FIFA wa kuondoa mpango wake wa kuuza hisa katika mashindano yake, ikiwemo Kombe la Dunia, kwa sekta binafsi."
UEFA pia ilisema katika siku na wiki zijazo itafanya kazi kwa karibu na vyama wanachama wake pamoja na mashirikisho mengine ya mabara kutathmini jinsi mpango huo ulivyofikia hatua hiyo na kuweka utaratibu wa kuhakikisha hatua kama hizo haziwezi kuharakishwa bila mashauriano katika siku zijazo.
Maelezo zaidi:
Askofu Mkuu wa Canterbury awasili Cameroon kwa ziara ya kichungaji

Chanzo cha picha, MINAT
Askofu Mkuu wa Canterbury, Dame Sarah Mullally, amewasili nchini Cameroon kwa hatua ya pili ya ziara yake ya mataifa mawili barani Afrika.
Hapo jana alipokelewa na viongozi wa serikali ya Cameroon, maafisa wa Kanisa la Anglikana pamoja na Kamishna Mkuu wa Uingereza nchini humo.
Akiwasili katika uwanja wa ndege wa Yaoundé, alisema anafurahia kutembelea taifa hilo la Afrika ya Kati katika ziara yake ya siku kumi barani humo.
"Ni heshima kubwa kwangu kuwa hapa Cameroon. Hii ni mara yangu ya kwanza kutembelea Afrika kama Askofu Mkuu wa Canterbury," aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza kuwa yuko nchini humo kwa ziara ya kichungaji ya kuomba, kuabudu pamoja na Kanisa la Anglikana, kutembea bega kwa bega na waumini wake, na kuwatia moyo katika huduma yao.
Kabla ya kuwasili nchini humo, Dame Sarah alikuwa Ghana kwa siku tano ambapo alikutana na waumini wa Kanisa la Anglikana na kuimarisha uhusiano wao na Kanisa la England.
Akiwa huko pia alithibitisha tena dhamira ya kanisa hilo ya kutenga pauni milioni 100 katika mfuko wa kushughulikia athari za kihistoria za ushiriki wa Kanisa la England katika biashara ya utumwa kupitia Bahari ya Atlantiki.
Katika ziara yake ya siku tano nchini Cameroon, atatembelea miji minne, ikiwemo Buea na Limbe katika eneo la Kusini Magharibi linalozungumza Kiingereza, ambako mgogoro wa mapigano umeendelea kwa karibu muongo mmoja.
"Katika kipindi hiki cha migogoro mikubwa duniani na mateso yanayoendelea hapa Cameroon, nimekuja nikiwa na ujumbe wa Injili," alisema, akieleza kuwa ujumbe huo ni wa amani.
Akiwa Buea, atatembelea taasisi inayotoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga. Uhusiano wake na taaluma ya uuguzi unatokana na kazi yake ya awali kama muuguzi katika Huduma ya Afya ya Taifa ya Uingereza (NHS), ambako alipandishwa vyeo hadi kushika nafasi za juu.Siku ya Jumapili, Askofu Mkuu huyo mwenye umri wa miaka 64 atahubiri katika Bishopscourt jijini Douala, makao makuu ya Dayosisi ya Cameroon. Pia atatembelea makanisa mbalimbali na kukutana na viongozi wa dini katika jiji hilo.
Atakaporejea Yaoundé siku ya Jumatatu, atatembelea taasisi nyingine za kidini na kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali kabla ya kuondoka nchini Cameroon siku ya Jumanne.
Maafisa tisa wa Ukraine wauawa katika shambulizi la Urusi mjini Kyiv

Chanzo cha picha, Reuters
Takribani watu tisa wameuawa katika mashambulizi ya makombora ya balistiki ya Urusi dhidi ya Ukraine, kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo mapema Jumamosi.
Watu wengine 23 walijeruhiwa katika shambulio hilo dhidi ya mji mkuu, Kyiv, kulingana na Huduma yaDharura ya Ukraine.
Moscow imeongeza mashambulizi ya makombora ya balistiki maafa dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, jambo lililomfanya Rais Volodymyr Zelensky kusema kuwa mifumo ya kuzuia makombora inahitajika kwa dharura.
Mashambulizi hayo yalifanyika siku mbili baada ya kombora la kurushwa kutoka kwa 'meli' linalodhaniwa kuwa la Urusi kuangukia nchini Poland wakati wa shambulio kubwa dhidi ya Ukraine lililoua angalau watu wanane, wakiwemo wanafamilia sita wa familia moja katika kijiji kilicho karibu na Kryvyih Rih.
Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, alisema mji mkuu huo ulishambuliwa kwa makombora ya balistiki, huku shirika la habari la AFP likiripoti milipuko zaidi ya 10.
Moto ulizuka katika maeneo mbalimbali ya jiji na kukatika kwa umeme kuliripotiwa katika baadhi ya maeneo.
Klitschko alisema jengo la makazi katika eneo la Shevchenkivskyi liliharibiwa kwa kiasi, na kuacha watu wakiwa wamenaswa ndani.
Huduma za dharura zilisema angalau watu saba waliuawa katika shambulio katika wilaya ya Darnytskyi. Watu wengine 14 walijeruhiwa, wakiwemo watoto wawili, iliripoti huduma hiyo.
Kifaa kisichojulikana kilichorushwa kutoka angani chagonga meli ya mafuta karibu na Oman

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Operesheni za Biashara ya Baharini la Uingereza (UKMTO) limetangaza kuwa meli ya mafuta imegongwa na kifaa kilichorushwa ambacho hakikutambuliwa, umbali wa kilomita 20 kaskazini-mashariki mwa Lima, Oman.
Kulingana na afisa usalama wa mmiliki wa meli hiyo, mgongano huo uliharibu chumba cha injini na meli hiyo haiwezi tena kuongozwa wala kuendelea na safari yake. Walinzi wa pwani katika eneo hilo wamearifiwa na mamlaka zinafanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo.
Hakuna ripoti zozote za majeruhi au madhara kwa mazingira kufikia sasa. UKMTO imezitaka meli zinazopita eneo hilo kuwa waangalifu na kuripoti shughuli yoyote ya kutiliwa shaka.
Tukio hili linakuja wakati ambapo mvutano wa masuala ya baharini umeongezeka katika maji yanayozunguka Iran na Oman; katika wiki za hivi karibuni, meli kadhaa za kibiashara zimeshambuliwa katika Ghuba ya Oman na karibu na Lango la Bahari la Hormuz.
Wakati huo huo Iran imeweka vikwazo vya usafiri katika Lango la Bahari la Hormuz, huku Marekani ikituma vikosi vyake vya majini katika eneo hilo, ikisema inachukua hatua kulinda uhuru wa usafiri wa baharini.
Bado haijabainika ni nani aliyehusika na shambulio dhidi ya meli hiyo ya mafuta.
Soma zaidi hapa:
FIFA yafuta mpango tata wa uwekezaji wa Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino, anasema amefuta mpango uliozua utata wa kuuza hisa katika mashindano makuu ya shirikisho hilo, kufuatia upinzani mkubwa.
Raia huyo wa Uswizi alisema ni wazi kuwa mradi huo "umesababisha migawanyiko" ambayo "haiendani tena na maslahi" ya lengo lake la awali.
Raia huyo wa Uswizi aliongeza: "Kwa sababu hiyo, mpango huu hautaendelezwa."
Infantino alikuwa ameahidi kutoa dola milioni 40 kwa vyama vyote 211 wanachama iwapo vingeliunga mkono pendekezo la kuanzisha kampuni tanzu ya biashara kusimamia mashindano yake makubwa, ikiwemo Kombe la Dunia, na kuruhusu wawekezaji wa nje kununua hisa katika kampuni hiyo.
Rais wa Shirikisho la Soka la Asia (AFC), Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa amekaribisha hatua ya kufutwa kwa mpango huo.
"Mustakabali wa soka duniani lazima uamuliwe kupitia mashauriano, majadiliano ya pamoja na heshima kwa mifumo iliyowekwa ya uongozi wa mchezo wetu," alisema Sheikh Salman.
Vyama 55 wanachama wa soka barani Ulaya, UEFA, vilipiga kura Alhamisi wiki hii kususia Kombe la Dunia ikiwa mpango huo ungelitekelezwa.
Soma zaidi:
Marekani na Israel zinajiandaa kushambulia tena miundombinu ya nishati ya Iran - ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
CBS News, mshirika wa habari wa BBC linaripoti Marekani na Israel zinapanga operesheni dhidi ya miundombinu ya nishati Iran, na huenda mashambulizi hayo yakatekelezwa mapema wiki ijayo.
Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na CBS, Rais wa Marekani Donald Trump bado hajatoa amri ya mwisho ya kuanzishwa kwa mashambulizi hayo.
Mtandao huo ulisema kuwa operesheni hii itakuwa mojawapo ya mashambulizi makali zaidi kufanywa dhidi ya Iran katika vita vya Marekani na Israel.
Kituo hicho kilibainisha kuwa kulikuwa na majadiliano kuhusu kukomesha mashambulizi kabla ya masoko ya fedha kufunguliwa siku ya Jumatatu.
Baadaye, mwandishi wa Axios alimnukuu afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani akisema kuwa "Rais Trump anafikiria kuamuru kupigwa kwa mitambo ya nishati ya Iran katika siku zijazo, lakini bado hajatoa amri ya mwisho ya kuitekeleza."
Soma pia:
Natumai hujambo.




















