Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asitisha mpango wa kulinda meli Hormuz, ataja mazungumzo na Iran

Rais wa Marekani, Donald Trump alisema operesheni ya “Project Freedom”, iliyoanza siku chache zilizopita, itasimamishwa kwa “makubaliano ya pande zote” kwa sababu “maendeleo makubwa” yamepatikana kuelekea makubaliano na Iran.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Trump: Vita vya Iran na mzingiro wa Marekani vitaisha kwa makubaliano, la sivyo mashambulizi yataongezeka

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema vita dhidi ya Iran pamoja na mzingiro wa Marekani vinaweza kumalizika kupitia makubaliano, lakini ameonya kuwa mashambulizi yatazidi iwapo Tehran haitakubali.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema iwapo Iran “itakubali kutoa kile ambacho tayari kimekubaliwa” jambo alilolitaja kuwa “dhana kubwa” basi Operesheni Epic Fury itasitishwa.

    Trump ameongeza kuwa mzingiro wa Marekani pia “utairuhusu Mlango wa Hormuz kufunguliwa kwa wote, ikiwemo Iran.”

    Hata hivyo, ameonya kuwa iwapo Iran haitakubali makubaliano, mashambulizi yatarejea tena “kwa kiwango cha juu zaidi na nguvu kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa awali.”

    Kauli hiyo inaashiria msimamo mkali wa Washington huku ikiacha wazi uwezekano wa suluhisho la kidiplomasia ikiwa pande hizo mbili zitafikia makubaliano.

    Soma zaidi:

  2. Kupitia Hormuz bado ni hatari licha ya kusitishwa kwa “Freedom Project” - Mtaalam

    Mpango wa “Freedom Project” wa Marekani, uliotangazwa kwa mbwembwe kubwa na kusitishwa chini ya saa 48 baadaye, haukuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa suluhisho la kuondoa mkwamo katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Rais Donald Trump aliueleza mpango huo kama “hatua ya kibinadamu” ya kusaidia kuwaokoa takriban mabaharia 20,000 waliokwama katika Ghuba ya Uajemi kutokana na mzingiro wa pande mbili kutoka Marekani na Iran.

    Hata hivyo, Iran iliutafsiri mpango huo kama ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Aprili 8 na kushambulia msafara wa kwanza wa meli mbili za kibiashara za Marekani zilizokuwa zikisindikizwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani.

    Jeshi la Marekani limesema helikopta zake ziliharibu boti sita za kasi za Iran kujibu shambulio hilo, madai ambayo Iran imeyakanusha.

    Kupitisha meli mbili pekee katika mlango huo ni hatua ndogo sana kulinganisha na mahitaji halisi.

    Katika nyakati za kawaida kabla ya vita hivi, takriban meli 140 zilikuwa zikipita katika mlango huo kila siku.

    Hata Jeshi kubwa la Wanamaji la Marekani halina uwezo wa kusindikiza idadi hiyo yote ya meli, hivyo operesheni hiyo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya uratibu na uangalizi wa karibu.

    Hata hivyo, bado ukweli unabaki kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran linaendelea kuwa na droni, makombora, mabomu ya majini na boti za kasi za kutosha kutishia meli yoyote inayopita karibu na pwani yake.

    Kwa hiyo, bila makubaliano na Tehran, Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa njia hatari kwa usafiri wa majini.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Pakistan yapokea kwa matumaini kusitishwa kwa mpango wa Marekani wa kuongoza meli kupitia Hormuz

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amepongeza uamuzi wa Rais Donald Trump wa kusitisha operesheni ya Marekani ya kuongoza meli kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran katika mazungumzo ya amani, imesema imeupokea uamuzi huo kwa matumaini.

    Sharif amesema ana “shukrani kwa Rais Donald Trump kwa uongozi wake wa kishujaa na tangazo lake la wakati muafaka.”

    Ingawa Trump katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii aliitaja Pakistan “na mataifa mengine”, Sharif amesema ombi hilo pia lilitolewa na Saudi Arabia.

    Amesema Pakistan ina matumaini kuwa kile alichokiita “mwelekeo wa sasa” kitafungua njia ya kufikiwa kwa makubaliano ya kudumu.

    Hadi sasa, hakuna dalili za wazi kuwa Pakistan inajiandaa kuwa mwenyeji wa duru nyingine ya mazungumzo.

    Trump alisema kusitishwa kwa operesheni hiyo kunalenga kutoa nafasi ya kuona “iwapo makubaliano yanaweza kukamilishwa na kutiwa saini” kati ya Marekani na Iran.

    Kwa upande wake, Iran imeeleza kusitishwa kwa mpango huo ''Freedom Project'' kama ushindi.

    Soma zaidi:

  4. Iran yasema itakubali tu makubaliano ya “haki” na Marekani

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, yuko Beijing ambako amekutana na mwenzake wa China, Wang Yi.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Araqchi amesema Iran itakubali tu “makubaliano ya haki na ya kina” katika mazungumzo na Marekani yanayolenga kumaliza vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

    Akinukuu vyombo vya habari vya Iran, Reuters imeripoti kuwa baada ya mkutano wake na Wang Yi, Araqchi alisema: “Katika mazungumzo, tutafanya kila tuwezalo kulinda haki na maslahi yetu halali.”

    Kwa mujibu wa shirika la Associated Press, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alimwambia mwenzake wa Iran kuwa China “ina wasiwasi mkubwa” kuhusu vita ambavyo vimeendelea kwa zaidi ya miezi miwili na kwamba “usitishaji kamili wa mapigano” hauwezi kuepukika katika mazingira ya sasa.

    Hii ni ziara ya kwanza ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini China tangu Marekani na Israel zilipoanzisha vita dhidi ya Iran tarehe 28 Februari.

    Kwa mujibu wa AP, katika mkutano huo Wang Yi alisema: “Tunaamini usitishaji kamili wa mapigano unahitajika haraka, kurejea kwa mapigano hakukubaliki, na ni muhimu sana kudumisha dhamira ya mazungumzo na diplomasia.”

    Soma zaidi:

  5. Wanawake wanaohusishwa na kundi la wanamgambo kurejeshwa nyumbani

    Serikali ya Australia imethibitisha kuwa raia wake 13 waliokuwa wakihusishwa na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la Islamic State (ISIS) wanarejea kutoka Syria.

    Katika taarifa, Waziri wa Mambo ya Ndani Tony Burke amesema serikali haitatoa msaada wa moja kwa moja kwa kundi hilo linalojumuisha wanawake wanne na watoto tisa.

    Mkuu wa Polisi wa Shirikisho, Krissy Barrett, amesema baadhi ya wanawake hao watakamatwa na kufunguliwa mashtaka watakapowasili Alhamisi, akiongeza kuwa mipango ya kuwarejesha imekuwa ikiandaliwa tangu mwaka 2015.

    Barrett amesema pia watoto hao wataandaliwa programu za kuwasaidia kujiunga upya na jamii, pamoja na kupatiwa huduma za ushauri nasaha.

    Soma zaidi:

  6. Watu wanne wakamatwa kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi Tanzania

    Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watu wanne wakihusishwa na tukio la mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM, James Rogers Temba.

    Mwili wake ulikutwa unaelea kwenye maji yaliyokuwa yanatiririka katika mto Msimbazi eneo la Kipawa wilaya ya Ilala tarehe 30.04.2026 ukiwa hauna kichwa.

    waliokamatwa ni Steven Rogers Chaka, Mbungu ambaye ni Afisa maabara, mkazi wa Kilimanjaro, Anna Frank Lema miaka, mfanyabiashara na mkazi wa Tabata Chang'ombe, Twalib Khamis mkazi wa Kigogo kati na Michael John mkazi wa kigogo kati.

    Polisi wamesema kuwa vipo pia baadhi ya vielelezo ambavyo vinachunguzwa kuhusiana na tukio hilo.

    Jeshi limewataka wananchi kuwa watulivu ili kila anayehusika kulingana na ushahidi achukuliwe hatua za kisheria.

  7. Kampuni ya Ufaransa imesema kuwa meli yake ilishambuliwa katika mlango bahari wa Hormuz

    Kampuni ya usafirishaji ya Ufaransa, CMA CGM, imesema kuwa moja ya meli zake, San Antonio, ilishambuliwa Jumanne wakati ikipitia mlango bahari wa Hormuz, na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kujeruhiwa pamoja na uharibifu wa meli.

    Kampuni hiyo imesema wafanyakazi waliojeruhiwa wamehamishwa na wanapatiwa matibabu.

    “CMA CGM inafuatilia kwa karibu hali hii na inaendelea kushirikiana kikamilifu na wafanyakazi wa meli,” ilisema katika taarifa.

    Ingawa kampuni haikubainisha nani alifanya shambulio hilo, Iran imesema itashambulia meli yoyote itakayopita katika mlango bahari huo bila ruhusa yake.

    Kumekuwa na mashambulizi 26 dhidi ya meli katika Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa vita vya Iran, kulingana na mamlaka ya masuala ya baharini UK Maritime Trade Operations (UKMTO).

    Inasema kuwa tangu tarehe 28 Februari, imepokea taarifa za matukio 46 “ndani na karibu” na Ghuba, Ghuba ya Oman na mlango bahari wa Hormuz.

    Unaweza kusoma;

  8. Mtanzania afariki baada ya meli kushambuliwa mlango bahari wa Hormuz

    Baharia wa Kitanzania amepoteza maisha wakati akihudumu katika meli ya kuvuta iitwayo VOLANS, Shirika la uwakala wa Meli Tanzania, TASAC limeeleza.

    Kifo cha baharia huyo kwa jina Mchama Maregesi Mongu, kilitokea tarehe 3 mwezi Mei mwaka 2026.

    Meli hiyo iliyobeba bandera ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ilikuwa safarini kutokea UAE kuelekea nchini Oman.

    Chombo hicho kilishambuliwa na bomu wakati kikivuka kwenye mlango bahari wa Hormuz uliopo kati ya nchi za Iran na Oman.

    Katika taarifa yake, TASAC imesema kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafuatilia kwa karibu taarifa za tukio hilo ili waweze kuurudisha mwili wa marehemu nchini Tanzania, mara tu utakapopatikana.

    ''TASAC inaungana na IMO kusisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya mabaharia wanapokuwa baharini, hususani katika maeneo yanayohusisha haki ya kupita kwa amani kama inavyolindwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa sheria ya bahari'' Ilisema taarifa hiyo.

    Unaweza kusoma;

  9. Serikali ya Australia imesema baadhi ya familia zinazohusishwa na wanamgambo wa IS zinarejea Australia

    Kundi la wanawake na watoto 13 wenye uhusiano na Islamic State (IS) limekata tiketi za kurejea nchini Australia, serikali imesema.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Tony Burke, alisema serikali “haitatoa msaada wowote” kwa wanawake wanne na watoto tisa ambao wameishi kwa miaka kadhaa katika kambi ya wakimbizi nchini Syria.

    Kundi hilo ni sehemu ya watu 34 wanaodhaniwa kuwa wake, wajane na watoto wa wapiganaji wa IS.

    Kamishna wa Polisi Australia (AFP), Krissy Barrett, alisema baadhi ya watu watakamatwa na kufunguliwa mashtaka watakapowasili nchini Australia.

    Kundi kubwa liliondoka kambini mwezi Februari lakini lilirejea kwa “sababu za kiufundi,” huku serikali ikikataa kuwarejesha rasmi.

    Burke alisema hawa ni watu walioungana na kundi hatari la kigaidi na kuweka watoto wao katika mazingira mabaya, na akaongeza kuwa yeyote aliyefanya uhalifu atachukuliwa hatua kali za kisheria.

    Serikali iligundua kurejea kwao mara tu walipokata tiketi za ndege, ambapo mfumo wa tahadhari ulitoa taarifa hiyo mara moja.

  10. Polisi asimulia jinsi walivyofanya operesheni hatari ya kutoa mabaki ya mtu ndani ya mamba

    Afisa wa polisi, Johan Potgieter, amesimulia tukio la kushangaza ambapo alishushwa kutoka kwenye helikopta hadi kwenye mto uliojaa mamba nchini Afrika Kusini ili kusaidia kutoa mabaki ya binadamu.

    Kapteni huyo alikuwa amepewa jukumu la kumkamata mamba aliyeshukiwa kumla mfanyabiashara aliyesombwa na maji ya mafuriko.

    Tukio hilo lilitokea katika mto Komati, ambapo gari la mtu huyo lilikwama alipokuwa akijaribu kuvuka daraja la chini lililofurika.

    Potgieter alisema kuwa mamba huyo alikuwa amelala kwenye kisiwa kidogo katikati ya mto, na njia pekee ya kumfikia ilikuwa kwa njia ya anga. Katika operesheni hiyo, droni na helikopta zilitumika kuwatafuta wanyama hao hadi walipofika eneo hilo.

    Mamba aliyeshukiwa alipigwa risasi na maafisa wengine kabla ya Potgieter kufika. Awali walidhani amekufa, lakini baadaye waligundua bado alikuwa hai na alikuwa ameogelea umbali mfupi kuelekea juu ya mto.

    Baadaye, mabaki ya binadamu yalipatikana ndani ya mamba huyo mwenye urefu wa mita 4.5 na uzito wa kilo 500, na vipimo vya DNA vinaendelea kufanywa kuthibitisha utambulisho wa marehemu.

  11. Mashambulizi ya Urusi yaua zaidi ya watu 20 kabla ya usitishaji mapigano

    Mashambulizi ya Urusi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 20 kote Ukraine siku ya Jumanne, kabla ya kusitishwa kwa mapigano kulikotangazwa na pande zote mbili, Urusi na Ukraine

    Mamlaka za Zaporizhzhia zilisema watu 12 waliuawa katika shambulio la anga la Urusi, huku Rais Volodymyr Zelensky akilielezea kama “shambulio la kigaidi lisilo na huruma”. Pia alisema watu watano waliuawa Kramatorsk na wanne Dnipro.

    Kwa upande wa Urusi, mamlaka katika Chuvash Republic zilisema watu wawili waliuawa na 32 kujeruhiwa katika shambulio la droni.

    Siku ya Jumatatu, Urusi na Ukraine zilitangaza kusitisha mapigano kabla ya kumbukumbu za ushindi wa Vita vya pili vya Dunia, ambapo Urusi huadhimisha ushindi dhidi ya Ujerumani ya Nazi.

    Urusi ilisema itasitisha mapigano tarehe 8 na 9 Mei, na ikaonya kuhusu “shambulio kubwa la makombora” dhidi ya Kyiv ikiwa Ukraine itavunja makubaliano hayo.

    Hata hivyo, Kyiv ilitangaza kusitisha mapigano kuanzia usiku wa manane tarehe 6 Mei bila muda maalum wa mwisho, na kusema itachukua hatua zinazolingana na vitendo vya Urusi.

    Hadi sasa, kusitishwa kwa mapigano kunaonekana kuwa kwa upande mmoja tu, kwani hakuna makubaliano ya pamoja kuhusu masharti, muda, au ufuatiliaji wake.

    Mkuu wa wafanyakazi wa Zelensky, Kyrylo Budanov, alisema ikiwa Urusi itafuata hatua hiyo, Ukraine itaendelea kuheshimu kusitishwa kwa mapigano, na kuongeza kuwa “hatua inayofuata iko mikononi mwa Urusi.”

    Unaweza kusoma;

  12. Meli ya kitalii,iliyokumbwa na mlipuko wa Hantavirus yatarajiwa kuelekea visiwa vya Canary

    Meli ya kitalii ya Uholanzi, MV Hondius, ambayo imekumbwa na mlipuko wa Hantavirus, inatarajiwa kuelekea Visiwa vya Canary nchini Hispania, kulingana na taarifa ya serikali.

    Wizara ya afya ya Hispania imesema maafisa wanachunguza ni abiria gani wanahitaji kuhamishwa haraka kutoka Cape Verde, ambako meli hiyo ilikuwa imetia nanga.

    Abiria waliobaki wataendelea na safari kuelekea visiwa vya Canary, ambapo wanatarajiwa kufika ndani ya siku tatu hadi nne, ingawa bandari kamili ya kuwasili bado haijaamuliwa. Kampuni ya safari, Oceanwide Expeditions, imesema mpango ni kuelekea “Gran Canaria au Tenerife”.

    Watu watatu waliokuwa ndani ya meli hiyo wamefariki tangu ilipoondoka Argentina karibu mwezi mmoja uliopita kwa safari yake ya kuvuka Bahari ya Atlantiki.

    Wafanyakazi wawili, akiwemo daktari wa meli, wanahitaji matibabu ya haraka na wanasubiri kuhamishwa. Mtu mwingine anayehusishwa na raia wa Ujerumani aliyefariki pia anatarajiwa kuhamishwa.

    Katika taarifa yake, wizara ilisema daktari huyo, ambaye yuko katika hali mbaya, anatarajiwa kupelekwa katika Visiwa vya Canary Jumanne kwa ndege ya hospitali.

    Iliongeza kuwa WHO imeeleza kuwa Cape Verde “haiwezi kutekeleza operesheni hiyo”.

    “Visiwa vya Canary ndivyo vilivyo karibu zaidi vyenye uwezo unaohitajika. Hispania ina wajibu wa kimaadili na kisheria kusaidia watu hawa, miongoni mwao wakiwemo raia kadhaa wa Hispania,” ilisema taarifa hiyo.

    Unaweza kusoma;

  13. Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Marekani itasitisha kwa muda operesheni ya kusindikiza meli kupitia Mlango bahari wa Hormuz

    Operesheni ya Marekani ya kusindikiza meli zilizokwama katika Mlango bahari wa Hormuz itasitishwa kwa “muda mfupi”, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza Jumanne jioni.

    Trump alisema operesheni ya “Project Freedom”, iliyoanza siku chache zilizopita, itasimamishwa kwa “makubaliano ya pande zote” kwa sababu “maendeleo makubwa” yamepatikana kuelekea makubaliano na Iran.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilielezea hatua hiyo kama ushindi, vikidai kuwa Trump “alirudi nyuma” baada ya kushindwa mara kwa mara kufungua njia hiyo muhimu kwa usafirishaji wa kimataifa.

    Tangazo la Trump lilikuja wakati Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, alisema kuwa operesheni ya awali ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, “Operation Epic Fury”, imekamilika baada ya kufikia malengo yake.

    Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema alifanya uamuzi huo “kutokana na ombi la Pakistan”, ambayo imekuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran. Hata hivyo, aliongeza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya bandari za Iran vitaendelea.

    Tangazo hilo linaweza kuwashangaza baadhi ya watu, kwani linapingana na kauli za awali za viongozi wa Marekani akiwemo Rubio, waziri wa ulinzi Pete Hegseth, na mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi Dan Caine, ambao walisisitiza kuwa operesheni hiyo ingeendelea kuhakikisha uhuru wa usafirishaji katika eneo hilo.

    Rubio alisema: “Tunapendelea njia ya amani. Kile ambacho rais anapendelea ni kufikia makubaliano.”

    Kwa sasa, hatua itakayofuata haijulikani wazi. Serikali ya Marekani ilikuwa imesisitiza kuwa “Project Freedom” ni kampeni tofauti na vikwazo vya kiuchumi, ambavyo vina lengo la kuishinikiza Iran.

    Unaweza kusoma;

  14. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo