Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ameishutumu Marekani kwa kudai kuwa inataka kumaliza vita huku ikiendelea kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Qalibaf, ambaye pia ni mmoja wa viongozi wakuu wa mazungumzo ya Iran na Marekani, aliandika kwenye mtandao wa X:
"Marekani inaendelea kupeleka vifaa vipya vya kijeshi katika eneo hili huku ikidai inataka kusitisha vita. Wamedhani uwezo wetu wa kijasusi ni mdogo kuliko wao. Sasa tunaelewa kikamilifu mbinu hizi za Marekani na tumejiandaa ipasavyo. Vitendo ndivyo vinavyopaswa kuthibitisha kauli, si kuvipinga."
Kauli zake zimekuja wakati vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vikiripoti kuwa Washington inaongeza nguvu zake za kijeshi katika eneo hilo, hatua inayotafsiriwa kama maandalizi ya uwezekano wa vita vikubwa zaidi na Iran.
The New York Times, likinukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutajwa majina, liliripoti kuwa Marekani inapeleka ndege zaidi za kivita aina ya F 16, F 35 pamoja na ndege za kujaza mafuta angani katika Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake, The Washington Post limemnukuu afisa mmoja wa Marekani akisema Washington inajiandaa kwa uwezekano wa vita kupanuka dhidi ya Iran.
Afisa huyo, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema operesheni za Marekani zinaweza kukabiliwa na vikwazo kutokana na kupungua kwa mifumo ya ulinzi wa anga, akiba ya silaha za masafa marefu, pamoja na changamoto za kupeleka wanajeshi na ndege zaidi katika eneo hilo.
"Tunakabiliwa na upungufu unaotishia kuathiri usalama wa operesheni zetu, na sidhani kama Ikulu ya White House inalielewa kikamilifu suala hili," alisema.
Haya yanajiri wakati Iran na Marekani zikiendelea kushambuliana, huku pande zote mbili pia zikionyesha utayari wa kutafuta suluhu kupitia njia ya diplomasia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baqaei, amethibitisha kuwa Tehran imepokea mapendekezo kutoka kwa nchi zinazopatanisha ili kupunguza mvutano, lakini hakufichua maudhui yake.
Amesema mbali na hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Iran, juhudi za kidiplomasia pia zinaendelea.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Washington iko tayari kufikia suluhu ya kidiplomasia, lakini akasisitiza kuwa mabadiliko hayo yatategemea pia mwelekeo wa Iran.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran anatarajiwa kuzuru Pakistan, nchi inayotajwa kuwa mmoja wa wapatanishi wakuu katika juhudi za kupunguza mvutano kati ya Tehran na Washington.