Moja kwa moja, Mmoja wa viongozi wakuu wa ISIS auawa na majeshi ya Marekani na Nigeria

Rais wa Nigeria Bola Tinubu amethibitisha kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Islamic State (ISIS) katika oparesheni ya pamoja na Marekani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Kufikia hapo tunafika mwisho wa taarifa zetu za moja kwa moja

  2. Zaidi ya watoto 50 watekwa nyara nchini Nigeria

    Picha ya mtu akiwa amebeba bunduki

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya mtu akiwa amebeba bunduki

    Watu waliojihami wamewateka nyara Zaidi ya Watoto 50 kutoka shule tatu katika mji mmoja kaskazini mashariki mwa Nigeria.

    Wengi wa Watoto waliotekwa nyara ni kati ya umri wa miaka miwili hadi mitano.

    Walioshuhudia tukio hilo eneo la Mussa, katika jimbo la Borno, alisema washukiwa hao waliwatumia Watoto kujikinga wakati wanatoroka wakitumia pikipiki, na kuzuia maafisa wa polisi kuwafyatulia risasi.

    Hakuna kundi ambalo limekiri kuhusika na shambulio hilo.

    Utekaji nyara huo ulitokea katika Shule ya Sekondari ya Mussa, Shule ya Msingi ya Mussa Central, na Shule ya Msingi ya State Universal Basic Education Board.

    Utekaji nyara huo unasemekana kufanana na mashambulio ya awali yaliyotekelezwa na kundi la Boko Haram na kundi la Islamic State West Africa Province (ISWAP).

    Nigeria imekuwa ikakabiliana na visa vya utekaji nyara unaofanywa na makundi mbalimbali ya wahalifu.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Waziri wa usalama wa ndani wa Pakistan azuru Iran

    Waziri huyo pia alizuru Tehran mwezi uliopita

    Chanzo cha picha, IRAN

    Maelezo ya picha, Waziri huyo pia alizuru Tehran mwezi uliopita

    Shirika la habari la IRNA nchini Iran, limeripoti kuwa Waziri wa usalama wa Ndani wa Pakistan yuko mjini Tehran katika “ziara ambayo haikutangazwa rasmi.”

    Kulingana na IRNA, Waziri huyo Mohsen Naqvi, anatarajiwa kukutana na baadhi ya maafisa wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

    Pakistan bado inasimamia juhudi za upatanishi kipindi hiki cha usitishaji mapigano uliopo sasa kati ya Iran na Marekani.

    Mazungumzo ya kupatikana kwa amani kati ya wawaklishi wa Iran na Marekani bado hayajazaa matunda.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Kundi la Hamas lathibitisha kuuawa kwa kamanda wake na Israel

    Msafara wa mazishi Gaza

    Chanzo cha picha, AFP Via Getty

    Maelezo ya picha, Msafara wa mazishi Gaza

    Kundi la Hamas na jeshi la Israel wamethibitisha kuuawa kwa Izz al-Din Haddad, kamanda wa kijeshi wa kundi la Hamas, katika shambulio lililotekelezwa na Israel mjini Gaza jana jioni.

    Israel imesema kamanda huyo alikuwa miongoni mwa wapiganaji walioshiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7, mwaka 2023.

    Mazishi ya Izz al-Din Haddad yamefanyika leo mjini Gaza.

    Baadhi ya wanafamilia wa Haddad pia waliuawa katika shambulio hilo la anga lililotekelezwa na Israel.

    Mashirika ya kutoa misaada mjini Gaza yamesema kuwa watu wasiopungua saba waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

    Ingawa usitishaji mapigano eneo la Gaza uliafikiwa tangu mwezi Oktoba, serikali ya Israel imesema bado ina mamlaka ya kuwalenga wapiganaji wa Hamas.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Israel yatangaza wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Hezbollah

    Israel yaendelea kuishambulia Lebanon

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Israel yaendelea kuishambulia Lebanon

    Jeshi la Israel limesema limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo walioko wapiganaji wa Hezbollah kusini mwa Lebanon.

    Jeshi la Israel awali lilitoa ilani ya kuwahamisha wakazi wa maeneo ya kusini mwa Lebanon.

    Mashambulizi hayo mapya yamejiri siku moja tu baada ya wawakilishi wa Israel na Lebanon kukutana mjini Washington na kukubaliana kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 45.

    Awali, maafisa wa Lebanon waliishutumu Israel kwa kulenga vituo vya matibabu na wahudumu wa afya

    Wizara ya Afya ya Lebanon ilitangaza kuwa Israel ilishambulia kituo cha kutoa msaada na kuwaua watu sita, wakiwemo wahudumu watatu wa afya.

    Israel imekanusha kuwalenga wanaotoa misaada na vituo vya afya.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Bei ya nauli yapanda maradufu nchini Kenya

    Picha ya matatu

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya matatu

    Wahudumu wa magari ya uchukuzi maarufu matatu, nchini Kenya, wametangaza mgomo wa kitaifa utakaoanza siku ya Jumatatu, wakilalamikia ongezeko la bei ya mafuta.

    Wahudumu hao pia wameongeza bei ya nauli kwa 50%

    Chama cha Wamiliki wa Matatu kimesema sekta hiyo imeathirika pakubwa na gharama za juu za mafuta, na kuonya kuwa watasitisha shughuli za uchukuzi iwapo serikali ya Kenya haitaangazia malalamiko yao.

    Ongezeko la nauli kwa 50% ilianzwa kutekelezwa mara moja hapo jana, huku wakenya wengi wakilalamikia gharama ya juu ya usafiri.

    Nyongeza ya nauli imejiri siku mbili tu baada ya Mamlaka ya udhibiti wa nishati nchini Kenya EPRA kuongeza bei ya mafuta.

    Mjini Nairobi, bei ya petroli kwa sasa ni Sh214.25 (dola 1.65) na dizeli Sh242.92 (dola 1.88)

    Pia unaweza kusoma:

  7. Kiongozi mmoja wa kundi la ISIS auawa nchini Nigeria

    Picha ya Donald Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa majeshi ya Marekani na Nigeria yamemuua kiongozi wa pili kwa cheo katika kundi la kigaidi la Islamic State (ISIS) katika operesheni ya pamoja.

    Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema kuwa “Abu Bilal al-Minouki hataweza tena kuwadhuru watu wa Afrika wala kupanga mashambulizi dhidi ya Wamarekani.”

    Aliongezea kuwa Al-Minouki alikuwa “mtu hatari zaidi duniani”

    Al-Minouki alikuwa amewekewa vikwazo na Marekani mwaka wa 2023 kutokana na uhusiano wake na kundi la Islamic State.

    Pia unaweza kusoma:

  8. "Hatutavumulia tena vita ambavyo havituhusu" - Lebanon

    Waziri mkuu wa Lebanon

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Waziri mkuu wa Lebanon

    Waziri Mkuu wa Lebanon Nawaf Salam amesema kuwa nchi yake haiwezi tena kuvumilia “vita vya kiholela” vinavyopiganwa kwa maslahi ya watu wengine, na ametoa wito kwa jumuiya ya Kiarabu na kimataifa kuiunga mkono Lebanon katika mazungumzo yake na Israel.

    Kiongozi huyo ameitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa duru ya hivi karibuni ya mazungumzo na kuongezwa kwa muda wa usitishaji mapigano kwa siku 45.

    Akiishtumu Hezbollah kwa kujiingiza katika vita vya eneo hilo la Mashariki ya Kati, kwa kuinga mkono Iran, Waziri huyo mkuu alisema “Lebanon imekumbwa na matukio haya ya kiholela na imetosha” na kusisitiza kuwa jeshi la Lebanon ndiyo pekee kikosi cha usalama nchini humo.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Trump: kusitishwa kwa mpango wa nyuklia wa Iran kwa muda wa miaka 20 kunatosha

    Trump akizungumza na wanahabari baada ya mkutano wake mjini Beijing

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Trump akizungumza na wanahabari baada ya mkutano wake mjini Beijing

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema atakubali pendekezo la Iran kusitisha mpango wake wa nyuklia kwa muda wa miaka 20.

    Hii inaonekana kama kubadilisha msimamo wake wa awali wa kutaka Iran isitishe kabisa mpango wake wa nyuklia.

    Trump alisisitiza kuwa lazima iwe “miaka 20 ya kweli.” Awali alikuwa akitaka Iran isitishe kabisa urutubishaji wa uranium—hatua muhimu katika kutengeneza silaha za nyuklia.

    Rais huyo aliongezea kuwa uvumilivu wake kwa Iran unaisha, huku kukiwa hakuna dalili za mafanikio katika mazungumzo yanayoendelea.

    Vikosi vya Israel na Marekani vilianza mashambulizi ya anga dhidi ya Iran tarehe 28 mwezi Februari.

    Bado usitishaji mapigano uliopo tangu mwezi uliopita unaendelea kutekelezwa ili kutoa nafasi ya mazungumzo kufanyika.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Trump aionya Taiwan dhidi ya kutangaza uhuru wake

    Picha ya Rais Xi na Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Picha ya Rais Xi na Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ametoa onyo kwa Taiwan dhidi ya kutangaza rasmi uhuru wake kutoka China.

    “Nisingependa kuona mtu akijitangazia uhuru,” alisema rais huyo wa Marekani katika mahojiano na Fox News hapo jana, baada ya kukamilisha mkutano wake wa siku mbili na Rais wa China Xi Jinping mjini Beijing.

    Rais wa Taiwan Lai Ching-te awali alisema kuwa Taiwan haihitaji kutangaza uhuru wake kutoka China kwa sababu tayari inajiona kama taifa huru.

    Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikiiunga mkono Taiwan, ikiwa ni pamoja na kuipa silaha za kujilinda, lakini mara nyingi haijakuwa ikipaza sauti kuhusu uhusiano huo ili kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na China.

    Msimamo wa Washington kwa muda mrefu ni kwamba haiungi mkono uhuru wa Taiwan, huku uhusiano wa Washington na Beijing ukitegemea pakubwa kukubali kuwa kuna serikali moja tu ya China.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Idadi ya vifo kutokana na ugonjwa wa Ebola vyaongezeka nchini DRC

    Watu zaidi ya 2300 walifariki nchini DRC kati ya 2018 na 2020 kutokana na Ebola

    Chanzo cha picha, AFP via Getty

    Maelezo ya picha, Watu zaidi ya 2300 walifariki nchini DRC kati ya 2018 na 2020 kutokana na Ebola

    Kituo cha Afrika cha kuzuia na kudhibiti magonjwa (Africa CDC) limetangaza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika wilaya ya Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Takriban visa 246 na vifo 80 vimeripotiwa, hasa katika miji ya uchimbaji dhahabu ya Mongwalu na Rwampara, kulingana na taarifa za kituo hicho.

    Mamlaka nchini Uganda pia wamethibitisha kisa kimoja cha Ebola kilichoingia nchini humo kutoka DR Congo siku ya Ijumaa, huku wizara ya afya ya nchi hiyo ikisema kuwa mwanaume mwenye umri wa miaka mwenye umri wa miaka 59 aliyefariki siku ya Alhamisi alipatikana na virusi vya Ebola.

    Hakuna tiba iliyothibitishwa kutibu ugonjwa wa Ebola. Kulingana na shirika la afya duniani (WHO) 50% ya watu ambao hupatikana na ugonjwa huu hufariki.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Israel na Lebanon zakubaliana kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 45.

    Bendera ya Israel na Lebanon

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bendera ya Israel na Lebanon

    Lebanon imekaribisha makubaliano na Israel ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano kwa siku 45, ambao ulikuwa unatarajiwa kumalizika siku ya Jumapili,baada ya mazungumzo yaliyofanyika Marekani mwezi Aprili.

    Hata hivyo, vikosi vya Israel vilishambulia miji na vijiji vya kusini mwa Lebanon, na kuua angalau watu 12 siku ya Ijumaa, wakiwemo wahudumu watatu wa afya.

    Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani, Tommy Pigott, alisema kuwa “Tunatumai mazungumzo haya yatachangia katika kupatikana kwa amani ya kudumu kati ya nchi hizo mbili, kutambuliwa kikamilifu kwa mamlaka na mipaka ya kila upande, pamoja na kuimarishwa kwa usalama katika mpaka wa mataifa hayo.”

    Pia unaweza kusoma:

  13. Hamjambo, na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja leo siku ya Jumamosi