Robert Pattinson athibitishwa kuwa James Bond mpya
Muigizaji wa filamu za Batman, Robert Pattinson, amethibitishwa kuwa mwigizaji mpya atakayeigiza nafasi ya jasusi maarufu James Bond katika filamu zijazo za 007.
Pattinson atakuwa muigizaji wa saba kupewa nafasi hiyo katika mfululizo rasmi wa filamu za James Bond.
Katika taarifa yake iliyoripotiwa na jarida la Variety, Pattinson amesema kupewa nafasi ya kuigiza mhusika huyo ni heshima kubwa zaidi katika maisha yake.
"James Bond ni mmoja wa wahusika mashuhuri zaidi katika historia ya filamu, na kukabidhiwa nafasi ya 007 ni heshima ya maisha yangu," amesema.
Ameongeza kuwa anawashukuru mkurugenzi wa filamu hiyo, Denis Villeneuve, pamoja na timu ya Amazon MGM Studios kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo, akisema ana furaha kubwa kuanza kazi hiyo na timu hiyo.
Steven Knight, aliyetengeneza tamthilia maarufu ya Peaky Blinders, ndiye anayeandika mswada wa filamu hiyo mpya, huku Villeneuve akitarajiwa kuiongoza.
Tangazo la Pattinson limeambatana na picha yake akiwa katika mwonekano wa James Bond, amevalia suti rasmi na kushika bunduki. Video iliyotolewa kuthibitisha uteuzi wake inaishia kwa maneno: "James Bond atarejea".
Mwezi Mei, Amazon MGM Studios ilitangaza kuwa mchakato wa kumpata mwigizaji mpya wa James Bond ulikuwa umeanza baada ya kampuni hiyo kuchukua udhibiti wa haki za utayarishaji wa filamu hizo.