Viongozi wa kundi la 'Cockroach' wakamatwa Delhi

Chanzo cha picha, Reuters
Mamia ya waandamanaji wamekamatwa jijini Delhi wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na kundi la vijana la Cockroach Janta Party (CJP) wakidai mageuzi ya uchaguzi nchini India.
Kundi hilo limesema mwanzilishi wake, Abhijeet Dipke, pamoja na viongozi wengine walitiwa mbaroni mara baada ya kuwasili Delhi. Polisi walikuwa wametuma maelfu ya maafisa wa usalama na kufunga baadhi ya barabara kabla ya maandamano hayo.
CJP, ambalo halijasajiliwa kama chama cha siasa, linataka mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi na kujiuzulu kwa Kamishna Mkuu wa Uchaguzi, Gyanesh Kumar, likidai kuwepo kwa dosari katika orodha za wapiga kura. Tume ya Uchaguzi imekanusha madai hayo na kusema zoezi la kusasisha daftari la wapiga kura ni la kawaida.
Kundi la CJP pamoja na vyama vya upinzani vinamshutumu Kamishna Mkuu wa Uchaguzi, Gyanesh Kumar, kwa kuipendelea chama tawala cha BJP katika mchakato wa usasishaji wa daftari la wapiga kura. Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya India na BJP zimekanusha tuhuma hizo.
Akizungumza kabla ya kuwasili Delhi kwa maandamano hayo, mwanzilishi wa CJP, Abhijeet Dipke, alisema kundi hilo halitatishwa na vitisho vya kukamatwa au kufungwa jela.
"Wanaodhani wanaweza kutuzuia kwa vitisho vya jela wamekosea," alisema Dipke.
Mwanzilishi wa CJP, Abhijeet Dipke, pamoja na viongozi wengine wawili wa kundi hilo, Saurav Das na Ashutosh Ranka, walizuiliwa walipokuwa wakisafiri kwa ndege kutoka Mumbai kwenda Delhi siku ya Jumamosi.
CJP ilidai kuwa viongozi hao watatu wamepelekwa eneo lisilojulikana.
Polisi jijini Delhi hawajatoa tamko rasmi kuhusiana na kuzuiliwa kwao.





























