Tanzania kupata ufadhili - Shirika la Fedha Duniani
IMF imesema inatarajia uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.9 mwaka huu
Muhtasari
- Serikali yatupilia mbali matokeo ya uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kivita
- Wizara ya afya yasema mashambulizi ya Israel dhidi ya magari kusini mwa Lebanon yaua watu 12
- Mfalme Charles afungua Bunge la Uingereza
- Idadi ya wanaoendelea kuhama makazi yao kwa migogoro yaendelea kuongezeka - Ripoti
- Iran yazitahadharisha Marekani na Israel, yasema iko tayari kwa mashambulizi mapya
- Tanzania kupata ufadhili - Shirika la Fedha Duniani
- Trump aiongeza Somalia kwenye orodha ya nchi zinazokabiliwa na vitisho vya usalama
- Ghana kuwahamisha raia 300 kutoka Afrika Kusini
- Afungwa jela baada ya kuiba muziki wa Beyoncé ambao haujatolewa
- Kidonge kipya chatajwa kusaidia kudhibiti uzito wa mwili baada ya kuacha sindano
- Mourinho afanya mazungumzo ya kuwa kocha mpya wa Real Madrid
- Mfumo wa Trump wa 'Golden Dome' kugharimu dola trilioni 1.2 huku ukitiliwa shaka uwezo wake
- Iran yafanya mazoezi ya kijeshi kwa siri
- Pentagon: Gharama ya vita kati ya Marekani na Iran yafikia karibu dola bilioni 29
- Reuters: Saudi Arabia ilifanya mashambulizi ya siri dhidi ya Iran wakati wa vita
- Trump : Lazima tufikie makubaliano na Iran au itaangamizwa kabisa
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Serikali yatupilia mbali matokeo ya uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kivita

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Serikali ya kijeshi nchini Sudan imekataa tamko la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Africa (AU) lililotaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu madai ya uhalifu wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Maafisa wanasema kuwa si misheni iliyotumwa kwa uchunguzi ya Umoja wa Mataifa wala tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Afrika hakuna mwenye mamlaka ya kisheria kufanya uchunguzi huo.
Tamko hilo linataka kusitishwa kwa mapigano na ufikiaji usio na kikomo wa kibinadamu kwa Sudan. Lakini Khartoum imetupilia mbali matokeo yake, ambayo inasema yanakuja tu kutokana na kutembelea kambi za wakimbizi na mahojiano kwa njia ya mtandaoni, na si misheni za maeneo yaliyoathirika moja kwa moja.
Sudan imekataa kushirikiana na timu ya Umoja wa Mataifa tangu ilipoanzishwa miaka mitatu iliyopita.
Jeshi na mpinzani wake, vikosi vya Rapid Support Forces, wameshutumiwa kwa uhalifu wa kivita na ukiukwaji mwingine katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka minne.
Soma zaidi:
Iran yazitahadharisha Marekani na Israel, yasema iko tayari kwa mashambulizi mapya

Chanzo cha picha, CBS
Iran imesema iko tayari kujibu mashambulizi mapya kutoka Marekani au Israel huku mazungumzo ya amani yakionekana kukwama, kwa mujibu wa CBS.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika eneo la Tehran, Brigedia Jenerali Hassan Hassanzadeh, aliyesema mazoezi ya kijeshi yaliyofanyika karibu na mji mkuu wa Iran yameonyesha uwezo mkubwa wa vikosi vyao kukabiliana na tishio lolote kwa muda mfupi.
Mazoezi hayo ya siku tano yaliyopewa jina la “Martyr Commander” yalihusisha vikosi maalum na makomandoo wa IRGC, yakilenga kujiandaa dhidi ya operesheni za maadui pamoja na mbinu za mapambano katika mazingira tofauti.
“Hii inaonyesha tuko katika kiwango cha juu cha utayari wa kukabiliana na adui wa Marekani na Wazayuni wakati wowote na mahali popote,” alisema Hassanzadeh.
Tamko hilo limekuja wakati mvutano kati ya Iran, Marekani na Israel ukiendelea kuongezeka, huku juhudi za kidiplomasia zikionekana kutopata mafanikio ya haraka.
Kwa mujibu wa CBS, hatua hiyo pia inafuatia wasiwasi wa Iran kuhusu uwezekano wa mashambulizi mapya dhidi ya miundombinu yake ya kijeshi na nyuklia.
Wizara ya afya yasema mashambulizi ya Israel dhidi ya magari kusini mwa Lebanon yaua watu 12

Chanzo cha picha, EPA
Wizara ya afya ya Lebanon inasema watu wasiopungua 12 wameuawa katika mashambulizi saba tofauti ya anga ya Israeli dhidi ya magari kusini mwa Beirut, Lebanon huku vita kati ya Israeli na kundi la Hezbollah vikiendelea licha ya kusitishwa kwa mapigano.
Maafisa wa Lebanon wanasema mashambulizi hayo yalilenga msafara wa magari uliokuwa katika barabara kuu karibu na pwani.
Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya serikali ya Israel na Lebanon, Jeshi la Israeli limeendelea kufanya mashambulizi hasa kusini mwa Lebanon.
Jeshi la Israel halijasema lolote kuhusiana na tukio hilo lakini lilisema vikosi vya Israel vilishambulia miundombinu ya Hezbollah katika maeneo kadhaa ya kusini.
Wapiganaji wa Hezbollah pia walirusha ndege zisizo na rubani ambazo zililipuka karibu na eneo ambalo wanajeshi wa Israeli walikuwa wakifanya kazi kusini mwa Lebanon, iliongeza, bila kuripoti majeruhi wowote.
Siku ya Jumanne, wahudumu wawili wa dharura kutoka huduma ya dharura ya Ulinzi wa Raia inayoendeshwa na serikali walikuwa miongoni mwa watu 13 waliouawa katika mashambulizi kusini mwa Lebanon , kulingana na wizara ya afya ya Lebanon.
Inasema zaidi ya watu 400 wameuawa kote nchini huko tangu kutangazwa kwa usitishaji mapigano na Rais wa Marekani Donald Trump karibu mwezi mmoja uliopita.
Mfalme Charles afungua Bunge la Uingereza

Chanzo cha picha, Reuters
Mfalme Charles wa Uingereza ameongoza ufunguzi wa Bunge la Uingereza huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu hatma ya waziri huyo mkuu, ambaye anakabiliwa na shinikizo za kujiuzulu.
Mfalme aliweka ajenda zitakazopewa kipaumbele na serikali ya Sir Keir ikiwa ni utamaduni ambao umekuwa ukifanyika kwa miaka mingi iliyopita, ilidhamiriwa kutoa mwelekeo kwa mzozo unaokumba chama tawala cha Labour, kuhusiana na ikiwa Waziri Mkuu anapaswa kujiuzulu kufuatia matokeo mabaya katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Zaidi ya miswada 35 iliwasilishwa.
Muda mfupi kabla ya hotuba hiyo, vyombo vya habari nchini Uingereza viliripoti kuwa washirika wa waziri wa afya Wes Streeting walisema kuwa anajiandaa kujiuzulu, ili kuongeza shinikizo kwa waziri mkuu kujiuzulu.
Licha ya hotuba hiyo kusomwa na Mfalme Charles, hotuba hiyo iliandikwa na serikali ya sasa ambayo inaitumia kuangazia sheria inazozipendekeza katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Katika hotuba hiyo Starmer ameahidi kuongeza juhudi ili kuifanya Uingereza kuwa yenye nguvu na usawa zaidi.
Miongoni mwa masuala mengine ni pamoja na kuimarisha uhusiano wa Uingereza na Muungano wa Ulaya mbali na kuitaifisha kampuni ya chama ya uingereza.
Aidha serikali imeahidi kufanya mageuzi katika mfumo wa uhamiaji na kupunguza umri wa kupiga kura hadi miaka kumi na sita.
Hata hivyo kuna wasi wasi kuwa huenda Waziri Mkuu Keir Starmer akaondolewa kabla ya kutekeleza agenda hii ya serikali.
Chini ya sheria za chama cha Labour Streeting atahitaji uungwaji mkono wa wabunge 81 au asilimia 20 ya wabunge ili kuanzisha mchakato wa kutaka kumuondoa Starmer.
Starmer hata hivyo amekariri kuwa yuko tayari kupambana na pingamizi ya aina yoyote.
Idadi ya wanaoendelea kuhama makazi yao kwa migogoro yaendelea kuongezeka - Ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Migogoro na vita zimesababisha watu wengi zaidi kuhama ndani ya nchi zao mwaka jana kuliko majanga ya asili na yale yaliyosababishwa na binadamu kwa mara ya kwanza katika historia.
Kituo cha Ufuatiliaji wa Uhamisho wa Ndani na Baraza la Wakimbizi la Norway wanasema katika ripoti yao ya kila mwaka kuhusu hali hii kwamba mwishoni mwa mwaka wa 2025, watu milioni 82.2 walikuwa wakiishi katika makazi ya wakimbizi ulimwenguni kote.
Idadi hiyo inakaribia idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa mnamo mwaka wa 2024.
Mkurugenzi wa IDMC, Tracy Lucas, ameliambia shirika la AFP, kuwa "Idadi inasalia katika viwango vya juu vya kihistoria," na wanatoa wito ili liweze kuangaziwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo katika kipindi cha mwaka jana, wakimbizi wapya milioni 65.8 waliripotiwa, ikiwa ni pamoja na idadi ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao mara nyingi.
Migogoro na ghasia zilisababisha milioni 32.3 kati ya watu hao waliokimbia makazi yao, ikiwa ni asilimia 60 kutoka mwaka uliopita, huku milioni 29.9 wakikimbia dhoruba, mafuriko na majanga mengine.
"Hatujawahi kurekodi idadi kubwa kama hii ya watu waliohama kutokana na migogoro," alisema Lucas.
Ripoti hiyo ilieleza kwa kina jinsi migogoro inayoibuka, inayoongezeka na iliyokita mizizi katika maeneo kama vile Iran na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iliwalazimu watu kukimbia mara kwa mara ndani ya nchi zao.
Uhamisho kama huo unasalia kujilimbikizia sana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni kwamba huku zikikumbwa na hali ya kukosekana kwa utulivu iliyozidi mwaka jana, Iran na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pekee zilichangia theluthi mbili ya wakimbizi wapya wa ndani wanaotokana na mzozo, wakiwa takriban milioni 10 kila mmoja.
Sudan iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ilikuwa na wakimbizi wa ndani wengi zaidi kwa mwaka wa tatu mfululizo, na zaidi ya milioni tisa, ikifuatiwa na Colombia, Syria, Yemen na Afghanistan.
Huku vita vipya vinavyoendelea mwaka huu vikiongeza, mizozo mingi iliyokita mizizi kote ulimwenguni, watu wengi zaidi kuhama kutokana na ghasia kunaweza kutarajiwa.
"Familia nyingi zinarejea kwenye nyumba zilizoharibiwa na huduma zinazotoweka au haziwezi kurejea kabisa," Egeland alisema.
Pia unaweza kusoma:
Tanzania kupata ufadhili - Shirika la Fedha Duniani

Chanzo cha picha, BOT
Shirika la Fedha Duniani IMF limesema kuwa limefikia makubaliano na serikali ya Tanzania yatakayowezesha kupatikana kwa ufadhili wa dola milioni 375.5, huku nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikikabiliana na athari za vita dhidi ya Iran.
Jopo la maafisa wa ngazi ya juu wa shirika la fedha duniani IMF, likiongozwa na Nicolas Blancher, lilifanya ziara rasmi nchini Tanzania, na kufanya mazungumzo kuhusu awamu ya sita na saba ya ufadhili wa shirika hilo kwa Tanzania.
Kufuatia ziara hiyo jopo hilo limependekeza ufadhili wa dola milioni 375.5 kwa Tanzania.
Pendekezo hilo sasa linasubiri idhinisho kutoka kwa kamati kuu ya utendeji ya shirika hilo kabla ya fedha hizo kutolewa, na kufikisha jumla ya ufadhili wa shirika hilo kwa Tanzania kufikia dola milioni elfu moja na hamsini na mbili.
Kwa taarifa, IMF imesema kuwa malengo ya miradi yake nchini Tanzania yamaafikiwa.
Ripoti hiyo imesema ukuaji wa uchumi nchini Tanzania umesalia kuwa dhabiti huko mfumuko wa bei nao ukisalia kuwa chini na imara.
Aidha IMF imesema kuwa Tanzania ina hazina ya kutosha ya fedha za kigeni mbali na kuwa bajeti ya elimu na afya imeongezeka pakubwa.
Hata hivyo taifa la Tanzania limekumbwa na matatizo ya kiuchumi tangu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran Kuanza.
Bei ya Mafuta imepanda na kumekuwa na upungufu mkubwa wa pembejeo kama vile mbolea ya kilimo.
Blancher, ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuruhusu ongezeko la bei za mafuta kwenda kwa bei za ndani na kwa kuruhusu kiwango cha ubadilishaji wa fedha za kigeni kuamuliwa na mahitaji na upatikanaji.
IMF imesema inatarajia uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.9 mwaka huu huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kupanda hadi asilimia 4.7.
IMF hata hivyo imeonya kuwa kupanda kwa bei ya mafuta na mbolea na kutatizwa kwa usafiri wa anga na usambazaji wa bidhaa dunia huenda ikawa na athari kubwa kwa ukulima, utalii na sekta ya usafiri na hivyo kuchangia pakubwa mfumuko wa bei ya bidhaa.
Pia unaweza kusoma:
Ghana kuwahamisha raia 300 kutoka Afrika Kusini

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ghana inasema itawahamisha raia 300 kutoka Afrika Kusini kufuatia wimbi la maandamano dhidi ya raia wa kigeni hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Nje Samuel Okudzeto Ablakwa alisema katika chapisho kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne kwamba rais wa Ghana alikuwa ametoa idhini ya "kuhamishwa kwao mara moja".
Alisema Waghana "wenye dhiki" walijiandikisha katika ubalozi wa nchi hiyo huko Pretoria ili kuokolewa kutokana na ushauri kutoka kwa wizara ya mambo ya nje "kufuatia wimbi la hivi karibuni la mashambulizi ya chuki dhidi ya raia wa kigeni".
Wiki iliyopita, mamlaka ya Afrika Kusini yalikanusha kwamba mtu yeyote alikuwa ameshambuliwa, ikisema video zilizosambazwa sana zilikuwa bandia.
Siku ya Jumatatu, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema "maandamano na vitendo vya uhalifu vilivyoelekezwa kwa raia wa kigeni" hivi karibuni havionyeshi sera ya serikali, akivielezea kama "vitendo vya uhalifu visivyo na uhusiano wowote na serikali".
Aliongeza kuwa Afrika Kusini "itadhibiti uhamiaji, kulinda mipaka yetu na kutekeleza sheria zetu".
Maelfu ya Waafrika Kusini walijiunga na maandamano dhidi ya uhamiaji haramu, wakidai kufukuzwa kwa raia wengi wa kigeni wasio na vibali. Waandamanaji wanasema uhamiaji haramu umeathiri ajira za wakazi, makazi na kuchangia uhalifu.
Siku ya Jumanne, ubalozi wa Ghana nchini Afrika Kusini uliwashauri raia kuwa waangalifu sana na kuweka kipaumbele usalama wao kwa kuepuka mikusanyiko ya umma na kufunga maduka au biashara zao katika jiji la bandari la Durban kabla ya maandamano yaliyopangwa Jumatano.
Pia unaweza kusoma:
Trump aiongeza Somalia kwenye orodha ya nchi zinazokabiliwa na vitisho vya usalama

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Marekani imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuenea kwa makundi ya wanamgambo wenye msimamo mkali yanayofanya kazi Afrika Magharibi, hasa katika eneo la Sahel na Ziwa Chad.
Utawala wa Trump umeonya kwamba wanamgambo hao wanapata nguvu Afrika Magharibi baada ya kudai kushindwa nchini Iraq na Syria.
Marekani imetoa kauli hii katika ripoti iliyotolewa kuhusu mkakati wake mpya wa kupambana na ugaidi kwa mwaka 2026.
Katika ripoti hiyo, utawala wa Trump ulitambua Afrika Magharibi, eneo la Sahel, na Ziwa Chad, ambalo linapakana na kaskazini mwa Nigeria, kama kitovu cha wapiganaji wenye msimamo mkali ambao, Marekani inadai, wameshindwa Mashariki ya Kati na wamehamia Afrika.
Eneo la Afrika linakabiliana na tatizo la makundi ya waasi, ambalo linahusisha udhaifu wa serikali za Afrika.
Wataalamu wa usalama kama vile Dkt. Kabiru Adamu walisema kwamba ripoti hii inapingana na miongozo iliyoandikwa hapo awali:
"Hii inajumuisha maneno mengi ya kisiasa, kwa mfano, ikiwa ni pamoja na madai ya rais wa sasa kwamba alipoingia madarakani aliangamiza IS na makundi ya Al-Qaeda nchini Iraq na Syria."
"Trump alibainisha maeneo sita barani Afrika ambapo alisema makundi haya yamerejea, ikiwa ni pamoja na Afrika Magharibi, eneo la Sahel, Ziwa Chad, Msumbiji, Sudan, na Somalia," alisema Dkt. Kabiru Adamu.
Mojawapo ya malengo ya mkakati mpya wa kupambana na ugaidi uliotangazwa na Marekani ni kuzuia kuenea kwa makundi ya kigaidi yanayolenga kushambulia Marekani, pamoja na kuzingatia kuwalinda Wakristo ambao alisema wanakabiliwa na "hatari," hasa nchini Nigeria.
Soma zaidi:
Afungwa jela baada ya kuiba muziki wa Beyoncé ambao haujatolewa

Chanzo cha picha, EPA
Mwanamume aliyevunja gari na kuiba kifaa cha kuhifadhi habari yaani hard drive yenye muziki wa Beyoncé ambao haujatolewa amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
Kelvin Evans, mwenye umri wa miaka 41, alikiri mashtaka ikiwemo kuingia kwenye gari kwa njia ya uhalifu mwaka jana huko Atlanta, Georgia. Jaji alimhukumu kifungo cha miaka mitatu zaidi cha kufuatiliwa tabia.
Inaonekana bila mpangilio, Evans alivamia Jeep Wagoneer iliyokodishwa na mcheza densi na mpiga ngoma wa Beyoncé mnamo tarehe 8 Julai 2025, wakati ziara ya Cowboy Carter ya mwimbaji huyo ilipokuwa ikifanyika Atlanta.
Wawili hao walirudi na kukuta dirisha la nyuma la gari limevunjwa na mizigo yao imetoweka. Wachunguzi hawajapata diski hiyo au vitu vingine vilivyoibiwa.
Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Fulton County ilithibitisha kwa BBC kwamba Evans alifikia makubaliano ya kukiri mashtaka mahakamani Jumanne kabla ya kesi yake kuanza wiki hii.
Wakili wake alimwambia jaji kwamba mteja wake "alikuwa na matumaini ya kufanikiwa kimaisha siku zijazo kihalali na kuwa sehemu ya jamii kama sisi wengine".
Kama sehemu ya hukumu yake, Evans ameamriwa kukaa mbali na waathiriwa pamoja na maegesho ya magari ambapo wizi huo ulifanyika.
Amekuwa gerezani tangu alipokamatwa mwezi Agosti mwaka jana.
Korea Kusini yadokeza kushiriki kulinda usalama wa baharini katika Mlango wa Hormuz

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini, Ahn Gyu-bak amesema Seoul inazingatia hatua za taratibu za kushiriki katika kulinda usalama wa njia za usafirishaji wa majini katika Mlango wa Hormuz, lakini haitajihusisha moja kwa moja kijeshi.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Korea Kusini mjini Washington Jumatano, Ahn alisema pia aliwasilisha msimamo huo katika mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth Jumatatu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini, Ahn alisema:
“Tutatekeleza wajibu wetu kama mwanachama anayewajibika wa jumuiya ya kimataifa katika kuhakikisha usalama wa baharini katika Mlango wa Hormuz, na hatua kwa hatua tutatafakari namna tunavyoweza kushirikiana.”
Alisema hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kutoa uungaji mkono wa kisiasa, kupeleka wafanyakazi, kubadilishana taarifa pamoja na kutoa rasilimali za kijeshi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa hakukuwa na mazungumzo ya kina kuhusu kuongeza ushiriki wa wanajeshi wa Korea Kusini katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Trump azua mjadala baada ya kuiita Venezuela “Jimbo la 51” la Marekani

Chanzo cha picha, Truth social
Rais wa Marekani Donald Trump ameibua mjadala mpya baada ya kuchapisha ramani ya Venezuela iliyoambatanishwa na bendera ya Marekani na maneno “State 51” kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Jumanne usiku.
Trump, ambaye yuko njiani kuelekea China kwa mkutano na Rais Xi Jinping, alichapisha picha hiyo siku moja baada ya ripota wa Fox News kusema kuwa rais huyo alimweleza kwa simu kwamba alikuwa “anafikiria” kuifanya Venezuela kuwa jimbo la 51 la Marekani.
Kauli na picha hiyo zimezua mjadala mkubwa kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa Trump aliwahi pia kutoa kauli zinazofanana kuhusu Canada na Greenland, hatua zilizokosolewa vikali na serikali pamoja na wananchi wa maeneo hayo.
Nollywood yaomboleza Alex Ekubo baada ya mwigizaji kufariki akiwa na miaka 40

Chanzo cha picha, Alex Ekubo/Facebook
Mwigizaji maarufu wa filamu za Nollywood Alex Ekubo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 40, tukio ambalo limeacha tasnia ya filamu ya Nigeria katika majonzi makubwa huku wenzake wakimkumbuka kwa heshima na hisia kali kupitia mitandao ya kijamii.
Habari za kifo chake zilithibitishwa Jumanne na baadhi ya watu wake wa karibu pamoja na waigizaji wenzake akiwemo Funke Akindele, Bolanle Ninalowo na Godwin Nnadiekwe.
Akizungumzia msiba huo kupitia Instagram yake, Funke Akindele aliandika maneno ya huzuni akisema alijaribu kumtafuta ili waweze kuonana tena lakini hakufanikiwa, akimtakia pumziko la amani na kumkumbuka kama “rafiki yake wa karibu” aliyeitwa kwa upendo “Ore mi”.
Kwa upande wake, Bolanle Ninalowo aliandika ujumbe wa rambirambi akimuombea marehemu apumzike kwa amani na kuwatakia faraja familia yake pamoja na mashabiki wote.
Naye Godwin Nnadiekwe alieleza kuguswa sana na taarifa hiyo akisema ni vigumu kuamini kifo cha rafiki na msanii mwenza, akisema Nollywood imepoteza kipaji cha kipekee.
Kwa mujibu wake, msiba huo umemuumiza sana hadi kushindwa kupata maneno ya kueleza, akibainisha kuwa marehemu tayari alikuwa ameacha wosia, jambo lililoongeza uzito wa huzuni hiyo.
Alex Ekubo alijulikana sana kama mmoja wa waigizaji mahiri na wanaopendwa zaidi katika Nollywood, akiwa amejipatia umaarufu kupitia filamu za mapenzi, vichekesho na vipindi vya televisheni vilivyovutia watazamaji ndani na nje ya Nigeria.
Ronaldo akosa ushindi, Al Nassr na Al Hilal wagawana pointi katika mbio za ubingwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Al Nassr na Al Hilal zimekutana katika mchezo uliotarajiwa kuamua hatima ya ubingwa wa ligi ya Saudi Pro League.
Jorge Jesus alianza vibaya mchezo huo baada ya kikosi chake kuzidiwa nguvu katika kipindi cha kwanza na upande wa Simone Inzaghi.
Licha ya shinikizo hiyo, bao la Mohamed Simakan lilibadilisha mwelekeo wa mchezo na kuipa Al Nassr matumaini makubwa ya karibu na ubingwa wa kwanza kwa Cristiano Ronaldo akiwa na klabu hiyo.
Katika kipindi cha kwanza, Al Hilal walitawala kwa muda mrefu wakitumia shinikizo na mpira wa pamoja uliopangwa vizuri, hatua iliyowalazimisha Al Nassr kujihami zaidi. Hata hivyo, Karim Benzema na N'Golo Kanno walikosa nafasi muhimu ambazo zingebadilisha matokeo mapema.
Baada ya bao la Simakan, Al Hilal walirudi nyuma kwa kiasi kikubwa huku Al Nassr wakianza kudhibiti mchezo.
Timu ya Jorge Jesus iliendelea kuhimili mashambulizi lakini bado haikupoteza ushindani, huku Sadio Mane akiongoza safu ya ushambuliaji kwa kiwango cha juu.
Kipindi cha pili kilishuhudia mabadiliko ya kasi, Al Nassr wakijaribu kuongeza mashambulizi na kulazimisha mchezo wa kasi zaidi.
Hali hiyo ilizifanya timu zote kugawana umiliki wa mpira, lakini Ronaldo hakuonekana sana uwanjani, huku Joao Felix akionyesha kiwango bora kwa upande wa ushambuliaji.
Wakati mchezo ukielekea kumalizika, kosa la kipa Bento Krepski liliiwezesha Al Hilal kusawazisha katika sekunde za mwisho za dakika za nyongeza (90+8), na kuhitimisha mchezo kwa sare iliyoweka mbio za ubingwa wazi zaidi.
Soma zaidi:
Kidonge kipya chatajwa kusaidia kudhibiti uzito wa mwili baada ya kuacha sindano

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti mpya umeonyesha kuwa kidonge kipya cha matumizi ya kila siku kinaweza kusaidia watu waliotumia sindano za kupunguza uzito kuendelea kuwa na mwili mwembamba hata baada ya kuacha matibabu hayo.
Dawa hiyo tayari inapatikana Marekani na huenda ikaanza kutumika Uingereza hivi karibuni.
Katika majaribio yaliyofanywa, wagonjwa waliotumia kidonge hicho kinachoitwa Orforglipron kila siku kwa mwaka mmoja walifanikiwa kuepuka kurejea kwa uzito mkubwa waliokuwa wameupunguza awali.
Kuongeza uzito wa mwili ni moja ya changamoto zinazowakabili watu wengi wanapoacha sindano za GLP 1 za kupunguza uzito.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Nature Medicine ulifadhiliwa na kampuni ya Eli Lilly ambayo pia hutengeneza sindano ya kupunguza uzito ya Mounjaro.
Wataalamu wanasema bado kuna haja ya kufanya tafiti zaidi ili kubaini mtu anatakiwa kutumia dawa hiyo kwa muda gani, huku baadhi wakisema huenda matibabu yakahitajika kwa muda mrefu au hata maisha yote.
Daktari Marie Spreckley, mtaalamu wa tafiti za kudhibiti uzito katika Chuo Kikuu cha University of Cambridge ambaye hakushiriki katika utafiti huo, amesema watu wengi wanaweza kuona ni rahisi zaidi kutumia kidonge kuliko kujidunga sindano.
Hata hivyo, ameonya kuwa bado haijulikani matokeo hayo yataendelea kwa muda gani kwa matumizi ya muda mrefu.
“Utafiti huu unaonyesha kuwa unene kupita kiasi ni tatizo sugu ambalo linaweza kurejea tena, na mara nyingi huhitaji matibabu na msaada wa kuendelea,” alisema.
Soma Pia:
Mourinho afanya mazungumzo ya kuwa kocha mpya wa Real Madrid

Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha raia wa Ureno Jose Mourinho yuko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kurejea kuinoa Real Madrid, miaka 13 baada ya kuondoka kwa mara ya kwanza katika dimba la Santiago Bernabeu.
Mourinho mwenye umri wa miaka 63 ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kuchukua mikoba ya ukocha, na kwa sasa ndiye mgombea pekee ambaye Real Madrid inaendelea kufanya naye mazungumzo rasmi.
Iwapo makubaliano yatafikiwa, atamrithi Alvaro Arbeloa ambaye alichukua nafasi hiyo mwezi Januari baada ya kuondoka kwa Xabi Alonso.
Rais wa Real Madrid Florentino Perez alianza kufikiria uwezekano wa Mourinho kurejea siku mbili baada ya kuondoka kwa Xabi Alonso, kupitia mawasiliano ya awali na wawakilishi wa kocha huyo wa Ureno.
Kwa sasa Mourinho ni kocha wa Benfica baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili Septemba mwaka jana. Hata hivyo, jana alikwepa kuzungumzia mustakabali wake.
“Kuna mechi dhidi ya Estoril, na kuanzia Jumatatu nitaweza kujibu maswali kuhusu mustakabali wangu na wa Benfica,” alisema Mourinho.
Mechi ya Jumamosi dhidi ya Estoril Praia utakuwa wa mwisho kwa Benfica msimu huu.
Kuanzia Jumapili, Real Madrid itakuwa na nafasi ya kukamilisha dili hilo kwa gharama nafuu kutokana na kipengele cha mkataba kinachomruhusu Mourinho kuondoka kwa ada ya euro milioni tatu ndani ya siku 10 baada ya mechi ya mwisho ya msimu.
Katika kipindi chake cha kwanza Real Madrid kati ya mwaka 2010 na 2013, Mourinho aliiongoza klabu hiyo kutwaa taji la La Liga, Copa del Rey pamoja na Spanish Super Cup.
Baada ya kuondoka Madrid, alirejea Chelsea na kushinda taji lake la tatu la Ligi Kuu England pamoja na Kombe la EFL msimu wa 2014 hadi 2015.
Mwaka 2016 alijiunga na Manchester United ambapo alitwaa Europa League, EFL Cup na Community Shield kabla ya kutimuliwa mwaka 2018 kutokana na matokeo mabaya.
Mourinho pia amewahi kuzinoa Tottenham Hotspur, AS Roma ambako alitwaa ligi ya Europa Conference mwaka 2022, pamoja na Fenerbahce kabla ya kujiunga na Benfica mwaka jana.
Wakati huo huo, Real Madrid imemaliza msimu wa 2025 hadi 2026 bila taji lolote, huku mahasimu wao Barcelona wakitwaa ubingwa wa La Liga baada ya ushindi wa mabao 2 kwa 0 katika El Clasico na kumaliza kwa tofauti ya pointi 14.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid iliondolewa robo fainali baada ya kufungwa kwa jumla ya mabao 6 kwa 4 na mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich.
Soma pia:
Mfumo wa Trump wa ‘Golden Dome’ kugharimu dola trilioni 1.2 huku ukitiliwa shaka uwezo wake

Chanzo cha picha, Getty Images
Mfumo wa kisasa wa ulinzi wa makombora wa Rais wa Marekani Donald Trump unaojulikana kama “Golden Dome” unatarajiwa kugharimu takriban dola trilioni 1.2 za Marekani sawa na pauni bilioni 882 katika kipindi cha miaka 20 ya kuubuni, kuujenga na kuendesha, kwa mujibu wa makadirio ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge la Marekani.
Kiasi hicho ni kikubwa zaidi kuliko makadirio ya awali ya dola bilioni 175 zilizokuwa zimetengwa kwa mradi huo.
Hata hivyo, mfumo huo uliobuniwa kuilinda Marekani dhidi ya makombora ya balistiki na makombora kutoka kwa meli za kivita huenda usiwe na uwezo wa kuhimili mashambulizi makubwa ya moja kwa moja.
Ripoti mpya ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge imeonya kuwa “Golden Dome” inaweza kuzidiwa nguvu katika shambulizi kamili kutoka Urusi au China.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa gharama za ununuzi pekee zitazidi dola trilioni moja, ikijumuisha mifumo ya kuzuia makombora pamoja na teknolojia za anga za juu za kutoa tahadhari na kufuatilia makombora.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mashaka kuhusu uwezo wa Marekani kujenga mfumo wa ulinzi wenye uwezo wa kulinda eneo kubwa kiasi hicho la kijiografia.
Maafisa wa Marekani pia wameonya kuwa mifumo iliyopo sasa haijaendana na maendeleo ya silaha za kisasa zinazomilikiwa na mataifa hasimu.
Licha ya gharama kubwa zinazotarajiwa, Ofisi ya Bajeti ya Bunge ilisema mfumo huo “unaweza kuzidiwa uwezo na mashambulizi makubwa yatakayofanywa na taifa lenye nguvu sawa au linalokaribia kiwango hicho.”
Amri ya kiutendaji iliyoagiza kuundwa kwa mfumo huo, ambao awali uliitwa “Iron Dome for America”, ilieleza kuwa tishio la silaha za kizazi kipya limekuwa “kubwa na tata zaidi” kadri muda unavyopita, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa Marekani.
Mwezi uliopita, SpaceX na Lockheed Martin zilipata kandarasi zenye thamani ya hadi dola bilioni 3.2 kwa ajili ya kuunda mifumo ya majaribio ya anga ya kuzuia makombora kwa mradi huo.
Soma zaidi:
Iran yafanya mazoezi ya kijeshi kwa siri

Chanzo cha picha, Getty Images
Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran kimetekeleza mazoezi ya kijeshi ambayo hayakutangazwa rasmi, yaliyopewa jina la “Mashahidi wa Makamanda”.
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa mazoezi hayo yalilenga kupima uwezo wa vikosi vya kijeshi katika kukabiliana na adui pamoja na kutathmini mikakati ya operesheni za kivita.
Kwa mujibu wa Hassan Hassanzadeh, mbinu zote za kiutendaji na operesheni za vikosi maalumu pamoja na maafisa wake zilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa mazoezi hayo.
Alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa mapambano na kuongeza utayari wa kijeshi dhidi ya hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa na adui.
Soma zaidi:
Pentagon: Gharama ya vita kati ya Marekani na Iran yafikia karibu dola bilioni 29
Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imetangaza Jumanne kuwa makadirio ya hivi karibuni ya gharama ya vita dhidi ya Iran yamefikia karibu dola bilioni 29 za Marekani.
Takwimu hiyo mpya, iliyotolewa wakati wa kikao cha kujadili bajeti katika Bunge la Marekani, ni takriban dola bilioni 4 zaidi ya makadirio yaliyotolewa wiki mbili zilizopita na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth.
Pete Hegseth pamoja na Jenerali Dan Caine walikuwa wakifafanua ombi la bajeti ya dola trilioni 1.5 kwa mwaka 2027 walipoulizwa kueleza gharama ya vita dhidi ya Iran.
“Wakati wa ushuhuda huo, gharama ilikuwa dola bilioni 25,” alisema Jules Hurst, afisa mkuu wa fedha wa Pentagon ambaye pia alikuwepo katika kikao hicho, akirejelea makadirio ambayo Waziri wa Ulinzi aliwasilisha kwa Bunge Aprili 29.
Pia unaweza kusoma:
Reuters: Saudi Arabia ilifanya mashambulizi ya siri dhidi ya Iran wakati wa vita

Chanzo cha picha, @modgovksa/X
Baada ya kuripotiwa jana kuwa UAE ilifanya mashambulizi ya siri ya anga dhidi ya Iran, shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba Saudi Arabia pia ilitekeleza mashambulizi kadhaa ambayo hayakutangazwa rasmi dhidi ya Iran, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake wakati wa vita vya Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa maafisa wawili wa Magharibi wenye ufahamu wa suala hilo pamoja na maafisa wawili wa Iran, mashambulizi hayo ndiyo mara ya kwanza kwa Saudi Arabia kujulikana kuchukua hatua ya moja kwa moja ya kijeshi ndani ya ardhi ya Iran, hali inayotafsiriwa kuwa ishara ya Riyadh kuonyesha uthubutu zaidi katika kujilinda dhidi ya mpinzani wake mkuu wa kikanda.
Reuters imesema katika ripoti yake maalumu kuwa mashambulizi hayo, ambayo hayajawahi kuripotiwa hapo awali, yalifanywa na jeshi la anga la Saudi Arabia na huenda yalitekelezwa mwishoni mwa mwezi Machi.
“Hayakuwa mashambulizi ya kawaida, bali yalikuwa ya kulipiza kisasi baada ya Saudi Arabia kushambuliwa,” mmoja wa maafisa hao wa Magharibi aliliambia Reuters.
Hata hivyo, Reuters imesema haikuweza kuthibitisha maeneo mahsusi yaliyolengwa katika mashambulizi hayo.
Afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia hakuzungumzia moja kwa moja madai hayo alipoulizwa na Reuters kutoa maoni, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran nayo ikikataa kujibu ombi la shirika hilo la habari.
Saudi Arabia, ambayo kwa muda mrefu imekuwa na ushirikiano wa karibu wa kijeshi na Marekani, imekuwa ikitegemea ulinzi wa Marekani dhidi ya vitisho vya kikanda. Hata hivyo, vita vya wiki 10 vilivyoikumba Mashariki ya Kati vimeonekana kuiacha nchi hiyo katika mazingira hatarishi baada ya baadhi ya mashambulizi kupenya mifumo ya ulinzi inayoungwa mkono na Marekani.
Jana, gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu ulifanya mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya mafuta ya Iran katika Ghuba ya Uajemi katika saa za mwanzo za tangazo la usitishaji mapigano kati ya Iran na Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi hayo yalijumuisha angalau shambulizi moja dhidi ya vituo vya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran katika Kisiwa cha Lavan.
Soma zaidi:
