Wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza watekwa nyara na kutishiwa kuondolewa figo zao

Chanzo cha picha, Kurdish Regional Government
Zaidi ya wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza msimu uliopita wa kiangazi walitekwa nyara, kuteswa na kutishiwa kuondolewa viungo vyao kwa nguvu, BBC imebaini.
Wanaume hao vijana, wote kutoka Kurdistan ya Iraq, walikamatwa nchini Libya na kundi la wanamgambo ambao walidai fidia ya dola 5,000 kutoka kwa kila familia ya watu hao, na wakatishia kuwatoa figo ikiwa malipo hayatafanyika haraka.
Tumezungumza na baadhi ya mateka ambao waliachiliwa baadaye, na pia kuona ushahidi wa picha unaoonesha kuwa upasuaji wa kulazimishwa huenda ulifanyika.
Waliokuwa mateka walionesha ushahidi wa mateso, na walisema walikuwa wakishikiliwa katika mazingira duni sana, huku karibu watu 180 wakiwa kwenye seli moja.
Mateka mmoja ameripotiwa kufariki, na bado haijulikani ni wangapi wanaoendelea kushikiliwa.
Wanamgambo hao walipaswa kuwa wanawaongoza wahamiaji kupitia Libya hadi pwani ya Bahari ya Mediterania. Hata hivyo, mgogoro wa malipo ulizuka kati yao na msafirishaji haramu wa watu wa Kurd wa Iraq, Noah Aaron, ambaye alipanga safari hiyo ya wahamiaji.
Aaron kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 10 jela nchini Ufaransa kwa makosa tofauti ya utakatishaji fedha na usafirishaji haramu wa watu.
Maelezo kuhusu utekaji nyara huo yaliibuka wakati wa uchunguzi wa hivi karibuni wa BBC kuhusu msafirishaji mwingine wa watu, Kardo Jaf, ambao ulisababisha kukamatwa kwake mwezi uliopita.
Inaaminika kuwa wasafirishaji hao wawili walikuwa wakifanya kazi pamoja hapo awali. Wote wawili wanatoka katika mji wa Ranya huko Kurdistan ya Iraq, eneo ambalo limeelezwa kuwa “limejaa mitandao hai ya usafirishaji haramu,” kulingana na ripoti ya taasisi ya utafiti ya Uingereza, Chatham House.
Mwezi Februari, timu ya uchunguzi ya BBC ilikuwa ikifanya utafiti kuhusu Jaf mjini Ranya, wakati ilipofikiwa na mwanaume mmoja wa eneo hilo aliyesema kuwa mtoto wake alikuwa miongoni mwa vijana waliowekwa mateka.
Unaweza kusoma;















