Zuio la Marekani dhidi ya bandari za Iran linaanza kutekelezwa huku Trump akitishia kushambulia ‘meli za mashambulizi’

Iran inasema ''haitababaishwa na vitisho vya Marekani'' ikiongeza kuwa mazingumzo ya Islamabad yalifeli kutokana na ''Washington kubadili misimamo''.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Beldeen Waliaula

  1. Kufikia hapo, ndipo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Mashambulizi ya makombora yaripotiwa kaskazini mwa Israel kutoka Lebanon

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Watu wawili wamejeruhiwa na wanapokea matibabu katika mji wa Nahariya kaskazini mwa Israel, baada ya shambulio la anga lililolenga mji huo.

    Shirika la habari la kitaifa nchini Lebanon lilisema kuwa kundi la Hezbollah lilitangaza kutekeleza mashambulizi ya anga katika kambi ya kijeshi ya Liman, kaskazini mwa mji wa Nahariya.

    Jeshi la Israel IDF limesema limedungua zaidi ya makombora 10, yaliyorushwa kutoka Lebanon wakilenga vikosi vya Israel vilivyoko kusini mwa Lebanon

    Jeshi la Israel limesema limepanua maeneo ya oparesheni yake kusini mwa Lebanon.

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mashambulizi bado yanaendelea nchini Lebanon, licha ya usitishaji mapigano kati ya Marekani na Iran, makubaliano ambayo Israel imesisitiza hayajumuishi kundi la Hezbollah.

    Kulingana na wizara ya Afya ya Lebanon zaidi wa watu 2089 ikiwemo Watoto 16 wameuawa kuanzia tarehe 2 mwezi Machi.

    Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu ICRC, limeshtumu vikali mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya nchini Lebanon.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Meli zashauriwa kujiandaa kukutana na kizuizi cha kijeshi cha Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meli zinapaswa kujiandaa kukutana na kizuizi cha kijeshi, Shirika la Uendeshaji wa Biashara za Baharini la Uingereza (UKMTO) limeonya katika iliyotoa.

    Taarifa hiyo kwa mabaharia inahimiza meli zote zilizoko eneo hilo “kudumisha uangalizi wa hali ya juu,” huku mwongozo wa kina zaidi ukitarajiwa kutolewa baadaye.

    UKMTO inawahimiza wote wanaosafiri kupitia eneo la Ghuba, Ghuba ya Oman, na Bahari ya Arabia mashariki mwa Mlango wa Hormuz kutarajia uwepo wa kijeshi na uwezekano wa kusimamishwa au kukaguliwa.

    “Kizuizi hiki cha kijeshi kinatumika bila ubaguzi kwa meli za bendera yoyote zinazohusika na bandari za Iran au vituo vya mafuta"

    Shirika hilo pia limesema kuwa ufafanuzi zaidi unatarajiwa kutolewa kupitia ilani zijazo kadri taarifa zaidi zitakavyopatikana.

  4. Waziri mkuu wa Pakistan asema bado wanaendelea na juhudi za kutatua mgogoro kati ya Marekani na Iran

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amesema juhudi bado zinaendela za kutatua mgogoro kati ya Marekani na Iran.

    Hii inajiri baada ya mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili yaliyofanyika mjini Islamabad nchini Pakistan kukosa kuafikia makubaliano.

    “Usitishaji mapigano bado unaendelea, juhudi za kutatua masuala yaliyosalia bado zinaendelea” Sharif ameliambia baraza lake la mawaziri kulingana na shirika la habari la AFP.

  5. Tutaangamiza 'meli za mashambulizi' za Iran- Trump

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wakati kizuizi cha kijeshi cha Marekani dhidi ya Iran ikianza kutekelezwa, Trump ameonya kushambulia meli za Iran.

    “Meli za Iran za mashambulizi zitaangamizwa ikiwa zitakaribia kizuizi cha kijeshi cha Marekani,” Donald Trump amesema katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social.

    “Jeshi la majini la Iran liko chini ya bahari, tumelimeharibu kabisa, tumezamisha meli 158. Tulichokosa kushambulia ni idadi ndogo ya kile wanachokiita ‘meli za mashambulizi ya haraka’, kwa sababu hatukuziona kama tishio kubwa,”Aliandka Trump.

    “Onyo: Ikiwa meli yoyote kati ya hizi itakaribia kizuizi chetu, itaangamizwa mara moja, kwa kutumia mfumo ule ule wa ‘kuua’ tunaotumia dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya”

    Itakumbukwa kuwa utawala wa Trump awali ulitekeleza mashambulizi dhidi ya boti zinazosafirisha dawa za kulevya katika bahari ya Carribbean na Pacific.

    Pia unaweza kusoma :

  6. Meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani na meli zingine mbili za kivita zaonekana Ghuba ya Oman

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    BBC Verify imekuwa ikikagua picha za setilaiti ili kubainisha ni meli gani za kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani ziko eneo la Mashariki ya Kati, baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa kizuizi cha kijeshi dhidi ya meli na bandari za Iran itaanza kutekelezwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.

    Picha za setilaiti za siku ya Jumamosi zinaonyesha meli ya kubeba ndege za kivita ya USS Abraham Lincoln ikiwa katika ukingo wa mashariki wa Ghuba ya Oman, takriban kilomita 200 kusini mwa pwani ya Iran.

    Hii ni mara ya kwanza kwa meli hiyo inayotumia nishati ya nyuklia kuonekana karibu na ghuba hiyo tangu vita hivyo kuanza.

    Meli nyingine mbili za kivita zimeonekana kwenye picha hizo za setilaiti na zina ukubwa na umbo unaofanana na meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani aina ya “guided-missile destroyers”.

    Inaaminika kuwa zinaweza kuwa sehemu ya kikundi cha meli ya USS Lincoln ambazo hutumika kutekeleza mashambulizi na kudungua makombora.

    Pia unaweza kusoma :

  7. Israel inaunga mkono kizuizi cha kijeshi katika bandari za Iran

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema Israel inaiunga mkono kizuizi cha kijeshi katika bandari za Iran.

    Akiwahutubia mawaziri kupitia njia ya video Waziri huyo mkuu alisema “Rais Trump ameamua kuweka kizuizi hicho na tunamuunga mkono”

    Netanyahu pia alisema alizungumza na naibu rais wa Marekani JD Vance siku ya Jumapili baada ya kutibuka kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani. Waziri huyo mkuu anasema Vance alimwambia kuwa “Kizuizi kikuu ni Iran kuendelea na mpango wake nyuklia”

    Waziri huyo mkuu pia alitupilia mbali semi kuwa kuna “utofauti” uliojitokeza kati yao na Marekani.

    Pia unaweza kusoma :

  8. Britney Spears ajipeleka kituo cha matibabu cha uraibu wa dawa za kulevya

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Nyota wa muziki aina ya pop nchini Marekani Britney Spears, amepelekwa katika kituo cha matibabu cha uraibu wa pombe na matumizi ya dawa za kulevya, mwezi mmoja tu baada ya kukamatwa akiendesha gari akiwa akiwa mlevi.

    Mwanamuziki huyo alijipeleka mwenyewe kwenye kituo cha matibabu ya uraibu wa pombe siku ya Jumapili, hii ni kulingana na mwakilishi wake.

    Baada ya kukamatwa tarehe 4 mwezi Machi, mwakilishi wa msanii huyo alisema tukio hilo “halina kisingizio lolote” na kusema jamaa za msanii huyo watakuja na njia “ya kuhakikisha msanii huyo anarejelea ubora wake na anastawi tena”

    Hii inakuja wiki tatu tu kabla ya msanii huyo mwenye umri wa miaka 44 kufikishwa mahakamani huko Carlifonia kwa shtaka la kuendesha gari akiwa mlevi.

    Mwakilishi wake aliiambia BBC kuwa“Britney atachukua hatua sahihi na kuheshimu sheria, na tunatumai huu unaweza kuwa mwanzo wa kuleta mabadiliko katika maisha yake.”

    Spears ni mmoja wa wasanii wa muziki wa pop waliofanikiwa zaidi,akiwa na nyimbo maarufu kama Baby One More Time, Toxic, Everytime, Gimme More, Womanizer, na Stronger.

    Kwa miaka 13 hadi mwaka 2021, Spears alikuwa chini ya “ulezi wa kisheria”, mfumo wa kisheria uliodhibiti fedha zake na maisha yake binafsi chini ya usimamizi wa baba yake.

    Pia unaweza kusoma :

  9. Mchezaji wa soka wa Ghana auawa baada ya basi lao kushambuliwa

    .

    Chanzo cha picha, Anadolu Agency via Getty Images

    Mchezaji wa soka nchini Ghana, Dominic Frimpong, ameaga dunia baada ya watu waliojihami kufyatulia risasi basi lililokuwa limeibeba timu yake ya Berukum Chelsea wakitoka kucheza mechi moja.

    Shirikisho la soka la Ghana (GFA) limesema limeshtushwa na tukio hilo na kutuma rambirambi zao kwa familia ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20.

    “Dominic alikuwa mchezaji chipukizi mwenye kipaji ambaye alikuwa anajituma na kuienzi mpira”

    Kulingana na timu ya Berekum Chelsea, basi ya timu hiyo ilikuwa ikirejea baada ya kushiriki mechi za ligi kuu ya Ghana siku ya Jumapili, kabla ya kushambuliwa na watu waliojihami na bunduki na wamevalia barakoa zilizoficha nyuso zao.

    “Wanaume hao walianza kufyatulia risasi basi, dereva wetu alijaribu kulitorosha gari. Wachezaji na wafanyikazi wengine walikimbilia kwenye misitu iliyokuwa karibu na kujificha” Uongozi wa timu hiyo ulitoa taarifa.

    Washukiwa bado hawajakamatwa huku uchunguzi ukiendelea.

    Pia unaweza kusoma :

  10. Jumuiya ya kimataifa yatoa hisia mseto kuhusu hali Mashariki ya Kati

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mataifa tofauti yametoa hisia zao kuhusu tishio la Trump kudhibiti bandari za Iran na kufunga mlango bahari wa Hormuz.

    Hispania- Waziri wa Ulinzi Margarita Robles amesema mapendekezo ya kusitisha vita hivyo “haina maana.”

    China imehimiza pande zote mbili “kuwa watulivu na kujizuia” na kuongeza kuwa, kuhakikisha mlango bahari wa Hormuz unasalia wazi ni ndilo lengo la jamii ya kimataifa.

    Asean- Kundi la mataifa 11 kusini mashariki mwa bara Asia, ambao wanategemea pakubwa mafuta kutoka Mashariki ya Kati wanataka mapendekezo ya kusitisha mapigano “kutekelezwa kikamilifu” na kuhakikisha usalama na uhuru wa baharini unadumishwa.

    Ufaransa- Rais Macron anasema Ufaransa na Uingereza wataandaa kongamano ambalo lengo lake litakuwa “kurejesha uhuru katika mlango bahari wa Hormuz katika siku zijazo”

    Aidha Uingereza kupitia Waziri mkuu Keir Starmer, imesema haiungi mkono “uzuiaji wa eneo hilo la bahari.”

    Pia unaweza kusoma :

  11. “Sitaki kujibizana na Trump, simuogopi”- Papa Leo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Papa Leo amesema “ataendelea kupaza sauti” dhidi ya vita vya Marekani nchini Iran vilivyoanzishwa na Rais Trump pamoja na sera zake za uhamiaji.

    Trump alikuwa amekashifu kiongozi huyo wa dini ya Katoliki kuwa “dhaifu katika masuala ya sera za kigeni na uhalifu” na kisha baadaye kuwaambia waandishi wa habari kuwa yeye “sio shabiki wake.”

    Papa Leo amemjibu Trump kwa kusema hana nia ya kujibizana naye ila ataendelea kuzungumza dhidi ya vita vinavyoendelea.

    Papa amekuwa mkosoaji mkubwa wa vita vya Iran akisema “havikubaliki” na kumtaka Trump kuja na njia mbadala ya kumaliza vita hivyo.

    Kulingana na Trump, Papa Leo alichaguliwa kuwa papa kwa kuwa ni raia wa Marekani na kudai kuwa “kama singekuwa ikulu ya White House, Leo hangekuwa Vatican.”

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Papa Leo ambaye yuko katika ziara ya siku 11 bara Afrika, alisema kuwa yeye si mwanasiasa ila ni mjumbe wa kueneza amani duniani.

    “Siogopi utawala wa Trump, au siogopi kueneza injili ambalo ndilo wajibu wangu na jukumu la kanisa.” Aliwaambia wanahabari .

    “Sitaki kujibizana na Trump, kuna watu wengi wanakufa duniani bila hatia, na nadhani ni wakati wa mtu kujitokeza na kupaza sauti na kusema kuna njia bora ya kutatua hili.” Aliongezea Papa Leo.

    Pia Unaweza kusoma:

  12. Meli nne zaonekana zikipita katika mlango bahari wa Hormuz

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    BBC Verify imekuwa ikifuatilia meli ambazo zinapita katika mlango bahari wa Hormuz, baada ya idara inayosimamia jeshi la Marekani Centcom, kutangaza kuwa wataifunga mlango huo wa bahari na kuzuia meli zote zinazoingia na kutoka bandari ya Iran.

    Tangu Centcom kutoa taarifa hiyo usiku wa jana, meli nne zimeonekana zikipita mlango huo wa bahari kulingana na data iliyotolewa na shirika la ufuatiliaji la MarineTraffic.

    Meli hizo, zote nne ni za kubeba mafuta au gesi,ila hazijatambuliwa kama zinamilikiwa na Iran, au zinatoka au kuingia katika bandari ya Iran.

    Centcom imetangaza kuwa manowari mawili USS Frank Peterson Jr na USS Michael Murphy, ziko karibu na eneo hilo na zitatumika kuondoa mabomu ya bahari yaliyokuwa yameekwa na jeshi la Revolutionary Guard la Iran.

    BBC Verify, inaendelea kufuatilia meli zinazopita katika mlango huo wa bahari huku makataa ya Marekani yakikaribia kutamatika.

    Pia unaweza kusoma :

  13. Watu kadhaa wahofiwa kuuawa Nigeria

    Members of Nigeria's armed forces (file picture)

    Chanzo cha picha, AP Photo/Sunday Alamba

    Raia kadhaa wanaripotiwa kuuawa baada ya ndege za Jeshi la Nigeria kufanya mashambulizi ya angani katika kijii kimoja kaskazini mashariki mwa nchi hiyo siku ya Jumamosi.

    Kuna taarifa za kukinzana kuhusu idadi kamili ya watu waliouawa katika shambulizi hilo huku baadhi ya vyanzo vikiripoti kuwa zaidi ya watu 200 huenda waliuawa.

    Eneo hilo liko mpakani kati ya majimbo ya Yobe na Borno ambako kundi la waasi la Boko Haram limekuwa likifanya uasi kwa muda mrefu.

    Jeshi la Nigeria limesema lililenga maeneo yaliyo na magaidi lakini limeongeza kuwa litachunguza kilichojiri.

    Kaskazini-mashariki mwa Nigeria kumeshuhudia matukio ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni ambapo operesheni za anga za kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali.

    Opereshine hizo zime zimewalenga kimakosa raia, ikiwa ni pamoja na vijijini, kambi za watu waliokimbia makazi na masoko.

    Soma zaidi:

  14. Vita vya Iran: Bei ya mafuta yapanda zaidi ya $100

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Bei ya Mafuta ghafi imeongezeka tena na kupindukia dola mia moja baada ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran kufeli kufikia makubaliano kuvimaliza vita vya Mashariki ya Kati.

    Bei ya Mafuta imekuwa ikipanda na kushuka tangu vita vya Iran kuzuka mwishoni mwa mwezi Februari na shughuli za usafiriki kuathirika katika Mlango Bahari wa Hormuz ambapo asilimia 20 ya Mafuta na gesi hupitia.

    Bei ya mafuta ilishuka chini ya dola 100 Jumatano iliyopita baada ya Washington na Tehran kufikia masharti ya kusitisha mapigano kwa wiki mbili ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Mlango huo wa bahari unategemewa kwa usafirishaji wa mafuta duniani, umekuwa kielelezo muhimu cha vita vya Iran baada ya Tehran kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel kwa kutishia kushambulia meli zinazojaribu kuitumia.

    Usafirishaji wa bidhaa kwenye njia hiyo ya Bahari umevurugwa kwa kiasi kikubwa tangu mzozo uanze tarehe 28 Februari, ingawa baadhi ya nchi kama India na Malaysia zimejkubaliana na Iran meli zao kupitia njia hiyo

    Kufungwa kwa Hormuz kumesababisha bei ya mafuta kuongezeka kote duniani.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Iran bado inataka silaha ya nyuklia, Trump anasema

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump anasema Iran bado inataka kuwa silaha ya nyuklia na alieleza nia hiyo wakati wa mkutano mjini Islamabad. "

    Bado wanataka kuwa na sila haio, na waliliweka wazi hilo usiku uliopita. Iran kamwe haitakuwa na silaha ya nyuklia."

    Trump tayari amesema mazungumzo ya moja kwa moja na Iran yalitibuka kwa sababu Tehran "haikuwa tayari kuachana na malengo yake ya nyuklia".

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi hapo awali alisema pande hizo mbili ziko "zinakaribia" kufikia makubaliano lakini Iran ilikabiliwa na " visa vya kubadilisha misimama hapa na pale".

    Soma zaidi:

  16. Péter Magyar ashinda uchaguzi wa Hungary kwa kishindo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Peter Magyar ameshinda uchaguzi mkuu wa Hungary,huku chama chake kikipata theluthi mbili ya viti vya ubunge katika uchaguzi ambao unamuondoa madarakani Waziri Mkuu Victor Orban aliyeliongoza taifa hilo kwa miaka 16.

    Bwana Magyar ameuambia umati mkubwa wa wafuasi mjini Budapest kuwa Hungary inataka tena kuwa taifa la Ulaya na kuongeza kuwa wamefanikiwa kuleta muujiza katika historia ya Hungary kwa kushinda uchaguzi huo kwa kishindo.

    Waziri Mkuu huyo ajaye wa Hungary ameahidi kipindi cha kukabidhiana madaraka kitakuwa cha amani.Viongozi kadhaa wa nchi za Umoja wa Ulaya wamempongeza Magyar kwa ushindi huo.

  17. Trump amshambulia Papa Leo juu ya Iran

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Donald Trump amemkosoa vikali Papa Leo XIV kwenye mitandao ya kijamii baada ya kiongozi wa kwanza wa Marekani wa Kanisa Katoliki Duniani kulaani tishio la rais wa Marekani dhidi ya Iran.

    Katika chapisho refu kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, rais huyo wa Marekani aliandi Papa "ni mbaya kwa Sera ya Kigeni".

    "Simtaki Papa ambaye anadhani ni sawa kwa Iran kuwa na Silaha ya Nyuklia," Trump alisema.

    Akiorodhesha malalamiko mengine dhidi ya Papa, Trump aliandika kwamba Papa ''hana nguvu kushughulikia uhalifu na silaha za nyuklia''.

    Trump pia alidai kuwa papa huyo alichaguliwa "kwa sababu alikuwa Mmarekani, na walidhani hiyo ndiyo ingekuwa njia bora ya kukabiliana na Rais Donald J Trump".

    "Kama singelikuwa Ikulu ya White House, Leo hangekuwa Vatican.".

    Maoni ya Trump dhidi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, ambaye - aanajulikana kwa kukisia matamshi yake - ameibuka kama mkosoaji mkubwa wa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Wiki iliyopita Papa Leo alisema tishio la Bw Trump la "ataiangamiza Iran" isipofikia makubaliano ya kumaliza vita ''halikubaliki''.

    Papa pia aliongeza kusema: "Kuna suala la sheria ya kimataifa, lakini zaidi ya yote, ni suala la kimaadili."

  18. Marekani kudhibiti kijeshi bandari za Iran kuanzia leo

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Marekani linasema litaanza kuzingira bandari za Iran siku ya Jumatatu, lakini "haitazuia" meli zinazopita kwenye Mlango wa bahari wa Hormuz zinazosafiri kwenda au kutoka nchi nyingine.

    Haya ndio matukio ya hivi punde kwa ufupi:

    • Kamandi Kuu ya Marekani imesema kuwa itaanza kuiza meli zinazoingia na kutoka katika bandari za Iran saa 10:00 ET (14:00 GMT) siku ya Jumatatu.
    • Rais wa Marekani Donald Trump anasema agizo lake ni la kujibu hayua ya Iran "kukataa makusudi" kufungua tena Mlango wa bahari wa Hormuz. Pia anaonya Jeshi la Wanamaji la Marekani "litawaangamiza Wairani wowote watakaowashambulia na watazuia meli yoyote itakayolipa ushuru wa usafiri kwenda Iran.
    • Bei ya Mafuta ghafi imeongezeka tena na kupindukia dola mia moja baada ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran kufeli kufikia makubaliano kuvimaliza vita vya Mashariki ya Kati. Bei ya Mafuta imekuwa ikipanda na kushuka tangu vita vya Iran kuzuka mwishoni mwa mwezi Februari na shughuli za usafiriki kuathirika katika Mlango Bahari wa Hormuz ambapo asilimia 20 ya Mafuta na gesi hupitia.
    • Trump anasema mazungumzo ya moja kwa moja na Iran mjini Islamabad yalifeli kwa sababu "Iran haiko tayari kuachana na malengo yake ya nyuklia"
    • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi anasema Tehran ilishiriki mazungumzo hayo kwa "imani njema" huku spika wa bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika akiongeza kuwa nchi yake haitatishika baada ya Rais Donald Trump kusema Jeshi la Majini la Marekani litaanza mara moja operesheni ya kuzuia Meli kupita Katika Mlango Bahari wa Hormuz

    Pia unaweza kusoma:

  19. Karibu kwa Matangazo ya Moja kwa mojaleo Jumatatu 13.04.2026