Polisi Kenya wasema maandamano ya kupinga ongezeko la bei za mafuta yalikiuka sheria

Chanzo cha picha, Getty Images
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Nairobi, Issah Mohamud, amesema maandamano yaliyoshuhudiwa sambamba na mgomo wa sekta ya usafiri yalikiuka sheria kwa kuwa hayakutanguliwa na taarifa rasmi kwa polisi.
Akizungumza na wanahabari, Mohamud amesema maandamano hayo hayakuwa ya amani, akidai waandamanaji waliweka vizuizi barabarani na kuvuruga shughuli za kawaida za wananchi.
“Maandamano hayakuwa ya amani, waliweka vizuizi barabarani na kusumbua raia na abiria wengine. Hali hii ilitatiza biashara na kulemaza uchumi kwa sababu imeathiri familia nyingi,” amesema Issah Mohamud.
Ameongeza kuwa polisi walifanikiwa kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika, licha ya baadhi ya waandamanaji kudai kuwa walikuwa wakilalamikia kile walichokiita dhuluma.
“Ninawarai Wakenya wote kutokubali kurubuniwa na wanasiasa au upande wowote,” ameongeza.
Aidha, amesema watu 225 wamekamatwa kufuatia matukio hayo na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Soma zaidi:















