Moja kwa moja , Trump aituhumu Iran kwa kuongeza mashambulizi ya droni na makombora
Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Iran imerusha ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi, ndani ya wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote
Tetesi za usajili Ulaya: Manchester United yamtaka Ivan Toney
Rais Ruto akutana na Rais Tshisekedi
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula
Mlango wa Hormuz utafunguliwa iwapo Marekani itatekeleza ahadi zake - Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Msemaji
wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Iran, Esmail Baghaei, amesema
kuwa iwapo Marekani itatekeleza ahadi zake, usalama utarejea katika Mlango
Bahari wa Hormuz na maeneo
jirani kwa muda mfupi iwezekanavyo.
Akizungumza
katika mkutano wake wa kila wiki na wanahabari, Baghaei alisema masharti ya
Iran ni kuondolewa kwa vikwazo anavyovitaja kuwa haramu na kusitishwa kwa
mzingiro wa baharini.
Baghaei
amesisitiza kuwa iwapo Marekani
itatekeleza ahadi zake, usalama utarejea katika Mlango Bahari wa Hormuz na eneo
hilo kwa muda mfupi iwezekanavyo.
Alipoulizwa
kuhusu uwezekano wa kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, alisema Tehran inaweza kuchukua
hatua haraka sana.
Trump aunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni ya Nvidia
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Jensen Huang na Donald Trump
Rais
wa Marekani Donald Trump ameunga mkono kurejea kwa Jensen Huang katika kampuni
ya Marekani ya kutengeneza chipu
za kompyuta, Nvidia.
Katika
ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump
alisema: "Natumai bodi ya wakurugenzi ya Nvidia itamrejesha Jensen Huang.
Huo utakuwa uamuzi bora kwa kampuni hiyo na Marekani."
Matamshi
hayo yanajiri baada ya Jensen Huang
kujiuzulu kutoka
wadhifa wake wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Nvidia mapema mwezi huu.
Kuondoka
kwa Huang kulifuatia utata kuhusu maisha yake binafsi, uliohusisha madai ya
kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na mwanamke anayedaiwa kuwa jasusi wa China.
Nvidia
ni mojawapo ya kampuni zinazoongoza
duniani katika utengenezaji wa chipu za kisasa zinazotumika katika teknolojia ya akili unde (AI).
AFCON 2027: Viwanja sita vyateuliwa kuandaa mechi Kenya, Tanzania na Uganda
Chanzo cha picha, online
Viwanja
sita vimeteuliwa kuandaa mechi za fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka ujao, ambazo zitaandaliwa kwa pamoja nchini Kenya, Tanzania na Uganda.
Viwanja
vitakavyotumika kwa mashindano hayo vilitangazwa wakati wa mkutano wa
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita nchini
Nigeria.
Mjini Nairobi, mechi
zitachezwa katika Uwanja mpya wa Talanta wenye uwezo wa kuchukua watazamaji elfu 60,000, ambao unatarajiwa
kufunguliwa mwezi Januari.
Tanzania
itakuwa na viwanja vitatu vitakavyotumika katika miji ya Arusha, Dar es Salaam
na Zanzibar.
Uganda
itatumia Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Kampala pamoja na Uwanja mpya wa
Hoima City, ambao timu ya taifa ya Uganda imekuwa ikiutumia katika mechi zake
za hivi karibuni za kimataifa.
Uwanja
utakaotumika kuandaa fainali ya mashindano hayo ya timu 24, yatakayofanyika
kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, bado haujaamuliwa.
Fainali
za mwisho za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zilizofanyika Morocco kuanzia
Desemba 2025 hadi Januari 2026, zilichezwa katika viwanja tisa vilivyoko katika
miji sita.
Mataifa yashindwa kufikia makubaliano katika mkutano wa COP31
Chanzo cha picha, Reuters
Nchi
mbalimbali zimeshindwa kufikia makubaliano mapya muhimu ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi,
kufuatia mivutano kuhusu matumizi ya nishati ya kisukuku na ufadhili katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi
ya COP31 nchini Uturuki.
Mazungumzo
hayo yaliyopaswa kukamilika siku ya Ijumaa
ila yaliendelea hadi Jumapili huku wanaoshiriki wakijaribu kufikia
mwafaka, na hivyo kuwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi uliochukua
muda mrefu zaidi katika historia.
Hata
hivyo, mapendekezo ya mwisho
hayakukubalika na Umoja wa Ulaya, mataifa ya visiwa vya Pasifiki na nchi
nyingine kwa sababu hayakutaja moja kwa moja matumizi ya nishati ya kisukuku,
ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko la joto duniani.
Wakati
huohuo, nchi nyingi maskini zilipinga kutokuwepo kwa ahadi zozote za wazi za
kifedha kutoka kwa mataifa tajiri za kuzisaidia kukabiliana na athari za
ongezeko la joto duniani.
Mara
ya mwisho makubaliano makuu ya kisiasa katika mkutano wa COP kushindwa kufikiwa
kwa aina hii ilikuwa mwaka 2009 mjini
Copenhagen, Denmark.
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ambaye huu ulikuwa mkutano wake wa
mwisho wa COP kabla ya kuondoka madarakani, alisema amesikitishwa sana na
matokeo hayo.
Aliyashutumu
makundi yenye ushawishi mkubwa katika sekta ya nishati ya kisukuku, akisema
yanatumia mbinu zinazofanana na zile za kampuni kubwa za tumbaku.
Alisema
makundi hayo yanapotosha sayansi, kuchelewesha sera, kuzuia hatua za
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujikusanyia faida kubwa huku watu
kote duniani wakilipa gharama.
Trump aituhumu Iran kwa kuongeza mashambulizi ya droni
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump
Rais
wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Iran imerusha ndege zisizo na rubani na
makombora mengi zaidi, ndani
ya wiki moja iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha zaidi
ya mwaka mmoja tangu vita kuanza.
Trump
hakutaja ripoti wala chanzo chochote cha takwimu kuthibitisha madai yake, lakini alihusisha kuongezeka kwa
mashambulizi hayo na ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani.
"Kwanza,
nilisema kuwa iwapo chama cha Democratic kingeshinda, masoko ya hisa
yangeshuka, jambo ambalo limetokea. Pili, nilisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran, ambayo hadi sasa imewaua waandamanaji 81,000, ingeongeza mashambulizi
yake, jambo ambalo pia limetokea."
Rais
huyo wa Marekani
aliongezea kuwa,
"Iran
imefyatua ndege zisizo na rubani na makombora mengi zaidi katika wiki moja
iliyopita kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha zaidi ya mwaka
mmoja. Msijali, yote yamenaswa na kudunguliwa, bila kusababisha uharibifu
wowote."
Mvulana wa miaka saba aokolewa baada ya saa 14 chini ya vifusi Ukraine
Chanzo cha picha, Ukraine State Emergency Service
Mvulana
mwenye umri wa miaka saba ameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo la makazi
lililoporomoka katika mji wa Dymer, baada ya kunaswa humo kwa saa 14 kufuatia
mashambulizi ya usiku ya Urusi katika eneo la Kyiv, yaliyosababisha vifo vya
watu tisa, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.
Shambulizi
hilo lilitokea mapema Jumapili. Mkuu wa utawala wa eneo la Kyiv, Tymur
Tkachenko, alisema pia mwanamke mwenye umri wa miaka 79 aliokolewa akiwa hai
kutoka kwenye jengo hilo lililoporomoka.
Rais
wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amesema watu watatu waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika
shambulizi tofauti lililotokea katika mji wa Vyshneve, pia katika eneo la Kyiv,hapo jana. Shambulizi hilo lililenga duka
la bidhaa za vyakula.
Mamlaka
za Ukraine zimesema mvulana aliyeokolewa katika mji wa Dymer anaendelea vizuri
kiafya na alikimbizwa hospitalini.
Meli ya Urusi yashambuliwa kwa droni katika bandari ya Libya
Chanzo cha picha, Reuters
Serikali
ya Libya imesema mlipuko uliotokea ndani ya meli ya Urusi iliyokuwa imetia
nanga katika kituo cha wanamaji kilichoko Benghazi,ulisababishwa na shambulizi
linaloshukiwa kutekelezwa na ndege isiyo na rubani.
Mlipuko
huo ulitokea mapema Jumapili wakati meli hiyo ilipowasili bandarini kwa ajili ya kuongeza mafuta na kupokea bidhaa kabla ya kuendelea na safari yake
ya kurejea Urusi.
Taarifa
ya serikali hiyo imesema hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Hadi kufikia sasa, Moscow haijatoa tamko lolote kuhusu shambulizi hilo.
Baadaye
hapo jana, Wizara ya
Afya ya Libya ilisema kuwa imepokea
watu waliojeruhiwa kutoka katika meli nyingine ya kibiashara ambayo pia
ililengwa katika shambulizi lililotokea karibu na pwani ya Benghazi.
Wizara
hiyo ilisema majeraha ya
waliojeruhiwa yalikuwa madogo na hali zao za afya zilikuwa imara.
Ujumbe
wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ulieleza wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi
hayo, huku ukitaka uchunguzi wa haraka, huru na wa wazi kufanyika.
"Libya
haiwezi kumudu, wala hairuhusiwi kuwa uwanja wa mapambano ya migogoro ya
kigeni," Umoja wa Mataifa uliandika kwenye mtandao
wa X
Video
zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa kijiografia na
kitengo cha BBC Verify zinaonyesha meli iliyoshambuliwa ikiwa imezingirwa na
moto na moshi.
Picha
za setilaiti kutoka kampuni ya Planet Labs PBC pia zinaonyesha meli ikiwa
inawaka moto katika bandari ya Benghazi.
Serikali
ya Umoja wa Kitaifa (GNS) inayotawala mashariki mwa Libya ilisema meli hiyo ya
Urusi, ambayo haikutajwa jina wala kutambuliwa rasmi, ilikuwa ikitumia bandari
ya Benghazi chini ya makubaliano yaliyopo ya usafiri wa baharini.
Tetesi za usajili Ulaya: Manchester United yamtaka Ivan Toney
Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester United inajiandaa kumsajili mshambuliaji wa Al-Ahli na timu ya taifa ya England, Ivan Toney, katika dirisha dogo la usajili la Januari.
Hata hivyo, klabu nyingine za Ligi Kuu England pia zinamfuatilia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30. (
Teamtalk)
Arsenal na Chelsea zinaendelea kumfuatilia kwa muda mrefu kocha wa Como, Cesc Fabregas, kama mmoja wa warithi wa kiti cha ukocha wa timu zao katika siku zijazo. Fabregas aliwahi kuzichezea klabu zote mbili za London.
(Football Insider)
Beki wa Nigeria, Calvin Bassey, anahusishwa na uwezekano wa kujiunga na Manchester United. Hata hivyo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 amesema yuko kwenye mazungumzo na Fulham kuhusu kuongeza mkataba wake.
(Standard)
Kiungo wa Liverpool na timu ya taifa ya Argentina, Alexis Mac Allister, mwenye umri wa miaka 27, anatamani kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Anfield. Mazungumzo kati yake na klabu hiyo yameripotiwa kushika kasi.
(Football Insider)
Arsenal na Liverpool zina nia ya muda mrefu ya kumsajili kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Jamal Musiala, mwenye umri wa miaka 23.
Klabu hizo zinaweza kujaribu kumnasa kutokana na kutokuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake Bayern Munich. (Talksport)
Paris Saint-Germain inaweza kuongeza kasi ya jitihada za kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi, mwenye umri wa miaka 20, baada ya mshambuliaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Desire Doue, 21, kupata jeraha kubwa la goti.
(Teamtalk)
Kipa wa Schalke 04, Loris Karius, amehusishwa na uwezekano wa kujiunga na Bayern Munich.
Hata hivyo, kipa huyo wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 33 amesema hajafanya mazungumzo na mtu yeyote kuhusu uwezekano wa kuhamia klabu nyingine.
(Sky Sports Germany)
AC Milan inaelekea kumpa kipaumbele mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Endrick, mwenye umri wa miaka 20, badala ya kujaribu kumsajili Nicolo Tresoldi, mshambuliaji wa Club Brugge mwenye umri wa miaka 22 ambaye pia ni mchezaji wa timu za vijana za Ujerumani. (Gazzetta dello Sport)
Rais William Ruto na Tshisekedi wakubaliana kuimarisha uhusiano wa kikanda
Chanzo cha picha, @WilliamRuto
Rais William Ruto na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, wamekubaliana kushirikiana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yalifikiwa hapo jana wakati wa Mkutano wa Kisiasa wa Ngazi ya Juu wa Nchi Nne uliofanyika mjini Oyo, Congo.
Mkutano huo uliongozwa na Rais Denis Sassou N’Guesso wa Jamhuri ya Congo, huku Rais wa Baraza la Mawaziri la Togo, Faure Essozimna Gnassingbé, ambaye pia ni mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mzozo wa mashariki mwa DRC, akihudumu kama mpatanishi.
Kuhusu uhusiano wa kidiplomasia, viongozi hao walikubaliana kushirikiana kurejesha uwakilishi wa kidiplomasia katika ngazi ya mabalozi, kuanzisha tena mashauriano ya mara kwa mara ya kisiasa na kuendeleza shughuli za Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Kenya na DRC.
Viongozi hao wawili pia waliahidi kuimarisha ushirikiano katika masuala ya amani na usalama wa kikanda, pamoja na kuimarisha muungano wa kikanda kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Chanzo cha picha, @WilliamRuto
Chanzo cha picha, @WilliamRuto
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatatu ya leo