Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yalipiza kisasi kwa washirika wa Marekani baada ya meli zake za mafuta kuharibiwa

Iran imeanza kulipiza kisasi dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba, baada ya Marekani kuharibu meli tano za mafuta za Iran.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Mkenya akamatwa kwa matamshi ya chuki dhidi ya Warundi

    Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutoka Buru Buru wamemkamata Mkenya mwenye umri wa miaka 32 kwa tuhuma za kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Warundi wanaoishi na kufanya kazi nchini Kenya.

    DCI imesema Kevin Odiwuor Otieno, maarufu kama Engineer Kevin, alitoa matamshi hayo katika mkutano wa Bunge la Mwananchi uliofanyika Jacaranda Grounds, Kayole. Matamshi hayo yalirekodiwa na kusambazwa mitandaoni, na kusababisha uchunguzi kuanzishwa.

    Uchunguzi wa awali umebaini kuwa matamshi hayo yalilenga raia wa Burundi wanaoishi Kenya na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

    Anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatano, Septemba 9, akikabiliwa na shtaka la matamshi ya chuki chini ya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, pamoja na mashtaka mengine yatakayoibuka kutokana na uchunguzi.

    DCI imesema uhuru wa kujieleza haulindi matamshi ya chuki, uchochezi wa kikabila au wito wa vurugu, na kwamba kulenga watu kwa misingi ya utaifa au kabila hakutavumiliwa.

    “DCI inawakumbusha wananchi kwamba, ingawa uhuru wa kujieleza unalindwa na Katiba, hauhusishi matamshi ya chuki, uchochezi wa kikabila au kuhimiza vurugu. Kenya ni taifa lenye watu wa jamii na mataifa mbalimbali, wakiwemo raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini,” DCI ilisema.

    “Kuwalenga watu binafsi au jamii kwa misingi ya utaifa au kabila, hasa pale ambapo vitendo hivyo vinalenga kuchochea chuki, uhasama au vurugu, hakutavumiliwa.”

    DCI pia imewaonya wananchi dhidi ya kujichukulia sheria mkononi au kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa umma.

  2. Marekani yaweka vikwazo dhidi ya mashirika ya ndege ya Iran

    Marekani imeweka vikwazo dhidi ya mashirika yote ya ndege ya Iran ambayo hayakuwa tayari yamewekewa vikwazo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Tehran.

    Hazina ya Marekani imesema vikwazo hivyo vinawalenga watu na kampuni 36 zinazosaidia sekta ya usafiri wa anga ya Iran, ambayo Washington inaituhumu kutumika kusafirisha silaha, wanajeshi na mizigo haramu.

    Katibu wa Hazina wa Marekani aliongeza: “Leo tunatimiza ahadi hiyo kwa kuiwekea vikwazo kampuni zinazoendelea kuiunga mkono Mahan Air.”

    Walengwa hao ni pamoja na mashirika 27 ya ndege ya Iran na kampuni katika nchi kama Falme za Kiarabu, Uturuki, Malaysia na Kazakhstan.

    Afisa wa Hazina ya Marekani amesema hatua hiyo inalenga kuiondoa karibu sekta nzima ya usafiri wa anga ya Iran kwenye mfumo wa biashara wa kimataifa.

    Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema kampuni au watu wanaofanya biashara na mashirika hayo ya ndege ya Iran wanaweza pia kukabiliwa na kutengwa na mfumo wa kifedha wa kimataifa.

    “Kupitia Operesheni Economic Outcast, tuliahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wanaotoa msaada wa kifedha kwa serikali ya Iran,” Bessent alisema Jumanne katika taarifa.

    Vikwazo hivyo pia vinawalenga watoa huduma za mizigo na mawakala wa mauzo wanaohudumia safari za kimataifa za Mahan Air, shirika la ndege la Iran ambalo Marekani inalishutumu kwa kusaidia shughuli za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).

    Iran imekuwa ikikabiliwa na vikwazo kwa muda mrefu, hali ambayo imezuia uwezo wake wa kununua ndege, vipuri na huduma za matengenezo.

  3. Takriban Warundi 600 wazuiliwa mpakani Kenya na Tanzania

    Takriban Warundi 600 wanaorejea nchini Burundi kutoka Kenya wamezuiliwa katika mpaka wa Isebania, kwa sababu hawana hati za kusafiria.

    Mkuu wa chama cha Waburundi wanaoishi Kenya, Alexis Ntinanirwa, ameiambia BBC Gahuzamiryango kuwa watu hao walikuwa kwenye magari mbalimbali, lakini maafisa wa uhamiaji waliwazuia kuvuka mpaka katika upande wa Sirari, Tanzania.

    Amesema Ubalozi wa Burundi nchini Kenya unafahamu hali hiyo na unaendesha mazungumzo na serikali za Kenya na Tanzania, ili kuruhusu Warundi hao kuendelea na safari bila kulazimika kurejea Nairobi kuchukua hati za kusafiria.

    Kwa sasa, amesema, wako katika uwanja wa mpira mpakani wakisubiri uamuzi.

    Bw. Ntinanirwa amesema shirika lao, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Burundi nchini Kenya, pia linafanya mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Shirika la Msalaba Mwekundu na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), ili kuwapatia msaada wa haraka, ukiwemo chakula na malazi.

    Ameongeza kuwa upatikanaji wa magari ya kuwasafirisha Warundi wanaotaka kurejea nchini humo ni changamoto nyingine inayoshughulikiwa.

    Hali hiyo inajiri huku mamia ya Warundi wakiwa wamekuwa wakikusanyika kwa siku kadhaa katika Ubalozi wa Burundi jijini Nairobi, wakitafuta hati za kusafiria ili kurejea nyumbani.

    Wanasema wanahofia matamshi ya Rais wa Kenya, William Ruto, kuhusu wafanyabiashara wadogo wa kigeni.

    Serikali ya Kenya imewapa raia wa kigeni siku 90 kukamilisha taratibu zinazohitajika ili kuishi, kufanya kazi na biashara nchini humo. Pia imesema hakuna mtu au kundi linaloruhusiwa kuwatisha, kuwanyanyasa au kuwazuia wageni kuendelea na shughuli zao.

    Hata hivyo, baadhi ya Warundi wameiambia BBC kuwa bado wanataka kurejea nyumbani kwa sababu hawaamini kuwa watalindwa.

    Ingawa Burundi, Kenya na Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wasafiri wanaovuka mipaka wanatakiwa kuwasilisha pasipoti au hati nyingine halali ya kusafiria.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Tetesi za Soka Ulaya Jumatano: Liverpool yamfuatilia Thiaw

    Liverpool na Manchester United zinaendelea kumfuatilia beki wa Ujerumani, Malick Thiaw, mwenye umri wa miaka 25, lakini Newcastle haina mpango wa kumuuza. . (Caught Offside)

    Winga wa Sunderland, Chemsdine Talbi, mwenye umri wa miaka 21, yuko mbioni kujiunga na klabu ya Al Ittihad ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

    Fulham inatarajiwa kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba wa beki wake, Calvin Bassey, mwenye umri wa miaka 26, anayewindwa na Inter Milan.

    Winga wa Bournemouth, Rayan, mwenye umri wa miaka 20, ana kipengele cha kuvunja mkataba chenye thamani ya pauni milioni 130, kitakachoanza kutumika katika dirisha la usajili la majira ya joto 2027. (David Ornstein via the Athletic - subscription required)

    Newcastle itampa kiungo Joe Willock, mwenye umri wa miaka 27, mkataba mpya iwapo ataendelea kuonyesha kiwango kizuri chini ya kocha Matthias Jaissle. (Football Insider)

    Kiungo wa zamani wa Real Madrid, James Rodriguez, mwenye umri wa miaka 35, yuko kwenye mazungumzo ya kujiunga na Avellino ya Serie B, inayofundishwa na beki wa zamani wa Italia, Alessandro Nesta.(Marca)

    Chelsea iko tayari kuwasilisha ofa kwa kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye umri wa miaka 23, katika dirisha la usajili la Januari(Teamtalk)

  5. Iran yalipiza kisasi kwa washirika wa Marekani baada ya meli zake za mafuta kuharibiwa

    Iran imerusha makombora ya balistiki dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani karibu na Al Azraq nchini Jordan, kwa mujibu wa taarifa ya Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, iliyonukuliwa na vyombo vya habari vya serikali.

    Vyombo vya habari vya Iran pia vimechapisha video vinavyodai kuonyesha makombora ya Iran yakirushwa kuelekea Jordan. Kamandi Kuu ya Marekani, CENTCOM, haijatoa maelezo kuhusu madai hayo.

    Mashambulizi hayo yanakuja baada ya CENTCOM kusema imeharibu meli tano za mafuta za Iran, Kaviz, Charminar, Horizon 1, Riesco na Derya, katika Ghuba ya Oman na karibu na Kisiwa cha Kharg.

    CENTCOM imesema iliwataka wafanyakazi wa meli hizo kuondoka kabla ya kuzishambulia na kuzifanya zishindwe kufanya kazi.

    Jumamosi, CENTCOM ilisema pia iliharibu meli tatu za mafuta za Iran baada ya Walinzi wa Mapinduzi kujaribu kushambulia meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani na meli ya kivita yenye makombora.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Iran itaendelea kupoteza meli za mafuta kila inapojaribu kushambulia meli za kivita za Marekani.

  6. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 9/09/ 2026.