Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ameishutumu Iran kwa kuendeleza mpango wa
kutengeneza silaha za kemikali, lakini akasisitiza kuwa Tehran bado haijafikia
uwezo wa kuzitumia kuishambulia
Israel.
Katika
taarifa iliyochapishwa na chama cha Likud kupitia mtandao wa Telegram, Katz amesema Iran imeanza kutengeneza
silaha za kemikali lakini bado haina uwezo wa kuzitumia kuishambulia Israel.
"Hatupaswi
kuruhusu hali hii kuendelea,"alisema Katz.
Matamshi
ya Katz yanajiri siku chache baada ya kituo cha televisheni cha CNN kuripoti,
kikirejelea taarifa za kijasusi za Marekani, kwamba Iran imekuwa ikiandaa mipango ya kuwalenga
maafisa katika utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kwa kulipua kile
kinachojulikana kama “bomu chafu” au dirty
bomb, mjini Washington DC.
CNN
ilinukuu vyanzo ambavyo
hawakuvitaja majina,
vikisema mipango hiyo ya Iran ni ya
tahadhari, lakini haimaanishi kwamba shambulio linakaribia kutekelezwa.
Waziri huyo wa Ulinzi alidokeza uwezekano
wa Israel kuishambulia Iran akisema hawatasubiri kushambuliwa kwanza.
“Jeshi linaweza kuamrishwa kuchukua hatua mapema ili
kuzuia tishio hilo iwapo itabainika kuwa Iran inapanga kuishambulia Israel.”
Kauli
hizo zinajiri wakati Israel inakabiliwa
na changamoto za kisiasa, baada ya Waziri Mkuu wa mpito Benjamin Netanyahu na
mpinzani wake mkuu Gadi Eisenkot kushindwa kupata wingi wa viti katika uchaguzi mkuu uliofanyika
mwezi uliopita.
Rais
wa Israel Isaac Herzog alimpa Eisenkot jukumu la kujaribu kuunda serikali, huku
Netanyahu akizidisha matamshi yake kuhusu tishio la Iran na kusisitiza umuhimu
wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayojumuisha chama chake cha Likud.
Ripoti
zingine zimeelezea kuwa Netanyahu amekuwa akimhimiza Rais wa Marekani Donald Trump, kuanzisha tena vita dhidi ya Iran.