Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kutana na Rais wa China Xi Jinping
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid
Urusi iko tayari kuendelea kuipatia China nishati, asema Putin
Chanzo cha picha, AP
Baada ya hotuba ya rais wa China, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa Urusi iko tayari kuendelea kusambaza nishati kwa China.
Amesema biashara kati ya mataifa hayo mawili inalindwa dhidi ya shinikizo la nje na mwenendo hasi wa masoko ya dunia.
Kwa mujibu wa Putin, Urusi na China zimejizatiti kuendeleza sera huru za mambo ya nje na zitaendelea kuwa na nafasi katika kuimarisha utulivu wa kimataifa.
Urusi na China zaonekana kukosoa hatua za kijeshi za Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Hoja kadhaa zimejitokeza katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Urusi na China, kama ilivyotangazwa na Kremlin, kuhusu “uhusiano wa kina wa ujirani mwema, urafiki na ushirikiano.”
Taarifa hiyo imekosoa aina mbalimbali za vitisho vya kijeshi duniani, na inaonekana kurejelea hatua za Marekani nchini Iran na Venezuela katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Xi Jinping na Vladimir Putin wametoa wito wa kupinga “mashambulizi ya kijeshi ya moja kwa moja dhidi ya mataifa mengine, matumizi ya mazungumzo yasiyo ya kweli kuandaa mashambulizi hayo, mauaji ya viongozi wa nchi huru, kuvuruga hali ya kisiasa ya ndani ya mataifa hayo na kubadili tawala, pamoja na kuwateka viongozi wa kitaifa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.”
Viongozi hao wawili wamesema hatua kama hizo “zinakiuka kwa kiasi kikubwa madhumuni na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na mahusiano ya kimataifa, na kusababisha uharibifu usioweza kurekebishwa kwa misingi ya mfumo wa dunia ulioanzishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia.”
Xi na Putin wanaonekana kujiweka zaidi kama walinzi wa mfumo mpya wa kimataifa, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu mwelekeo wa mfumo wa sasa wa dunia wakati wa muhula wa pili wa Rais wa Marekani Donald Trump.
Wanandoa wa Uingereza waliofungwa Iran waanza kususia kula gerezani
Chanzo cha picha, HANDOUT
Familia ya wanandoa wa Uingereza waliofungwa nchini Iran baada ya kushutumiwa kwa ujasusi imesema wawili hao wameanza kususia kula.
Lindsay Foreman na Craig Foreman walikamatwa walipokuwa wakivuka Iran kwa pikipiki mnamo Januari 2025, na baadaye walihukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani.
Wakati huo huo, raia wa Iran mwenye ukaazi wa kudumu nchini Marekani ameachiwa huru na kurejea Marekani baada ya kuzuiliwa kwa miaka kumi nchini Iran.
Shahab Dalili alikuwa ameshtakiwa kwa kushirikiana na serikali hasimu.
Iran yaonya vita vitaenea nje ya Mashariki ya Kati iwapo itashambuliwa tena
Chanzo cha picha, TASNIM
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran IRGC limetoa taarifa likionya kuwa iwapo Marekani na Israel wataishambulia Iran tena, vita vitaenea nje ya eneo la Mashariki ya Kati.
Taarifa hiyo ya kijeshi ya Iran imetolewa kujibu vitisho vya mashambulizi mapya vilivyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na baadhi ya maafisa wa Israel, waliodai kuwa hatua mpya dhidi ya Iran inaweza kusababisha vita kuenea katika maeneo mengi duniani.
Jeshi hilo limesema mashambulizi yoyote dhidi ya Iran yatakabiliwa na “majibu makali.”
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kupitia mtandao wa X kuwa Iran imejifunza mengi kutokana na vita vya karibuni na sasa ina uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi.
Katika ujumbe wake mwingine, amesema Iran imefanikiwa kuangusha ndege ya kivita ya Marekani aina ya F 35, akidai hatua hiyo imeonyesha uwezo mpya wa vikosi vya Iran.
“Kwa sababu ya mafunzo tuliyopata na maarifa tuliyojifunza, Marekani itakumbana na mshangao mwingine,” ameongeza.
Kauli hiyo imejiri siku moja baada ya Rais Trump kusema alikuwa amesitisha mpango mkubwa wa mashambulizi dhidi ya Iran kufuatia ombi kutoka kwa viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Uingereza yaondoa vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi
Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali
ya Uingereza imeondoa baadhi
ya vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi,huku bei ya mafuta ikipanda nchini humo.
Agizo hilo limeanza kutekelezwa hii leo,
na inaashiria hofu inayoongezeka kuhusu upatikanaji wa mafuta kutokana na kuzuizi kilichowekwa katika Mlango
bahari wa
Hormuz tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Vikwazo
dhidi usafirishaji wa gesi ya asili ya
Urusi iliyoyeyushwa (LNG) pia vimeondolewa.
Hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Marekani hivi majuzi ilikosolewa vikali.
Bei za mafuta ya ndege barani Ulaya zimeongezeka mara mbili Zaidi baada ya vita kuanza, huku bei ya mafuta katika vituo za mafuta zikipanda.
Mashirika
kadhaa ya ndege nchini Uingereza na duniani kote yamehairisha safari zake na kuongeza bei za tiketi
kutokana na kupanda kwa bei
mafuta ya ndege.
Baada ya miaka 127, Bournemouth kucheza michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza
Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya kutoka sare ushindi nyumbani dhidi ya Manchester City waliopata bao la kusawazisha la dakika za jioni kupitia Erling Haaland, Bournemouth bado wameandika historia kubwa kwa kufuzu michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo.
Sare ya bao 1-1 dhidi ya City katika Uwanja wa Vitality usiku wa Jumanne imeihakikishia Bournemouth nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League msimu ujao.
Hata hivyo, bado kuna uwezekano kwa Bournemouth kufuzu hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya kulingana na matokeo ya mechi za mwisho za msimu.
Iwapo Aston Villa wataifunga Freiburg katika fainali ya Europa League itakayochezwa Jumatano usiku, Bournemouth kuna uwezekano ku kupata nafasi hiyo.
Villa wakitwaa ubingwa huo na kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa EPL, watapata tiketi ya moja kwa moja ya Ligi ya mabingwa League kama mabingwa wa Europa League.
Hivyo itafanya nafasi ya ziada ya timu ya Ligi kuu England (EPL) kwenda kwa timu itakayomaliza nafasi ya sita, jambo ambalo linaweza kuinufaisha Bournemouth.
Ili hilo litokee, Aston Villa wanapaswa kupoteza dhidi ya Manchester City huku Liverpool wakishinda nyumbani dhidi ya Brentford.
Kwa upande wa Bournemouth, watakuwa na uhakika wa kumaliza nafasi ya sita iwapo wataepuka kupoteza dhidi ya Nottingham Forest au Brighton wakashindwa kuifunga Manchester United.
Bado kuna uwezekano mwingine mdogo wa Bournemouth kufuzu Ligi ya mabingwa Ulaya ikiwa Liverpool watapoteza kwa kipigo kikubwa katika mchezo wao wa mwisho huku Bournemouth wakishinda kwa mabao mengi.
Kwa mfano, Liverpool wakifungwa mabao 3-0 na Bournemouth kushinda 4-0, tofauti ya mabao inaweza kuibeba Bournemouth.
Pia njia ya kipekee zaidi inaweza kutokea ikiwa Liverpool wakifungwa 1-0 na Bournemouth kushinda 5-0.
Katika mazingira hayo, timu hizo zinaweza kuwa sawa kwa kila kitu hadi kuhitaji mechi ya mchujo maalum ya mwisho wa msimu kuamua nani afuzu ligi ya mabingwa.
Wakati Arsenal tayari wametwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22, bado kuna ushindani mkubwa katika michezo ya mwisho ya msimu huku nafasi za kufuzu mashindano ya Ulaya pamoja na vita vya kushuka daraja vikiwa bado havijaamuliwa.
Katika vita vya kushuka daraja, West Ham wanahitaji ushindi dhidi ya Leeds United ili kujiweka kwenye nafasi ya kuendelea kubaki EPL.
Tottenham pia wako kwenye presha kubwa huku wakihitaji ushindi dhidi ya Everton ili kuhakikisha hawashuki daraja.
Chelsea, Brighton, Brentford na Sunderland nazo bado zinapambana kuwania nafasi za michuano ya Ulaya kabla ya pazia la msimu kufungwa rasmi Jumapili hii.
Beijing na Moscow zinafaa kushirikiana zaidi, Xi amwambia Putin
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Rais Putin na Xi
Katika
hotuba yake, Rais Xi Jinping
wa China, amemwambia Rais wa
Urusi Vladimir Putin, kwamba nchi hizo mbili zinapaswa kusaidiana katika maendeleo na
kufufua uchumi wa mataifa hayo.
Putin naye
katika katika hotuba yake, amesema uhusiano
kati ya Urusi na China ni wa viwango
vya juu na unaonyesha “mwenendo mzuri” kati ya mataifa hayo mawili.
Putin aliisifia taifa lake kuwa “muuzaji
wa nishati anayeaminika” licha ya mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
China na Urusi pia wameongeza muda wa miaka mitano kwa mkataba walionao wa kushirikiana kibiashara na kijeshi.
Viongozi hao wawili pia wamejadili vita Mashariki ya Kati, Rais Xi akisema kuwa imefikia wakati muhimu wa kusitisha mashambulizi na kupatikana kwa amani.
Putin amemwalika Rais Xi
Jinping kutembelea Urusi mwaka
ujao, akisisitiza kuwa uhusiano kati ya Beijing na Moscow ndiyo “unachangia utulivu wa dunia.”
Xi
alikuwa Urusi mara ya mwisho mwezi Mei mwaka uliopita.
Rais Trump atishia kuishambulia Iran, iwapo makubaliano hayataafikiwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump
Rais
wa Marekani Donald Trump amesema kuwa alikuwa amebakisha saa moja tu, kabla ya
kuidhinisha shambulio jipya dhidi ya Iran, kisha akabadili uamuzi huo, baada ya kupokea ombi kutoka kwa mataifa ya Ghuba asitishe mashambulizi, huku akionya kuwa Marekani inaweza kuanzisha
mashambulizi mapya
dhidi ya Iran siku chache zijazo.
Trump amesisitiza
kuwa viongozi wa Iran “wanatakiwa
kuafikia makubaliano kwa haraka,” na kuongezea kuwa shambulio jipya la Marekani
linaweza kufanyika siku chache zijazo iwapo
hakutakuwa na makubaliano yaliyoafikiwa.
“Ninamaanisha
ndani ya siku mbili au tatu, labda Ijumaa au Jumamosi au Jumapili, au mwanzoni
mwa wiki ijayo, kwa sababu hatuwezi kuiruhusu Iran kuwa
na silaha ya nyuklia.”
Trump
pia alisema kuwa Rais wa China Xi Jinping, aliahidi kutoipa jeshi la Iran silaha yoyote.
Jeshi la Iran nalo limejibu semi za Trump
na kusema pia wako tayari kurejea kutekeleza mashambulizi.
Waziri wa Israel Bezalel Smotrich asema mwendesha mashtaka wa ICC anataka akamatwe
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Picha ya Bezalel Smotrich
Waziri wa Fedha kutoka mrengo wa kulia nchini Israel, Bezalel
Smotrich, amesema amepewa taarifa kwamba waranti ya kukamatwa
kwake imetolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.
Smotrich
hakusema ni mashtaka gani
anayokabiliwa nayo, lakini alieleza hatua hiyo kuwa “tangazo la vita” na kuinyooshea lawama mamlaka
ya Palestina.
Waranti
ya mtu kukamatwa na mahakama ya ICC huwa suala la siri na lazima iidhinishwe na
majaji wa mahakama hiyo.
Mahakama
hiyo aidha imekanusha kutoa waranti ya kukamatwa kwa viongozi watano wa Israel.
Smotrich
ambaye ana mamlaka makubwa juu ya sera za Israel katika eneo linalokaliwa
kimambavu la Ukingo wa Magharibi, aliagiza kubomolewa kwa Kijiji maarufu cha
Waaplestina cha Khan al-Ahmar karibu na Jericho.
Afisa mmoja wa Mamlaka ya Palestina amelaani agizo hilo na kulitaja kama “hatua hatari ya kuongeza mvutano”.
Mwaka 2018, Mahakama Kuu ya Israel iliidhinisha
amri ya kuwafurusha wakazi wa Khan al-Ahmar, lakini amri hiyo haijatekelezwa baada ya mahakama ya
ICC kutoa onyo kuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.
Watu 19 wauawa katika mashambulizi ya anga Lebanon
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Moshi unafuka kutoka kwa majengo yaliyolengwa kusini mwa Lebanon
Mashambulizi ya angani yaliyotekelezwa na Israel, imewauwa takriban watu
19 kusini mwa Lebanon, kulingana na wizara ya afya ya taifa hilo.
Kumi kati ya waliouawa ni watoto watatu na wanawake watatu ambao
walifariki katika shambulio moja nyumbani kwao, katika mji wa Dier Qanoun.
Lebanon ilianza kushambuliwa na Israel tarehe 2 mwezi Machi, baada ya
kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, kuishambulia Israel, kama hatua
ya kulipiza kisasi kifo cha aliyekuwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei.
Mashambulizi haya yanajiri siku chache tu, baada ya mataifa hayo mawili
kukubaliana kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa siku 45, ili kutoa muda kwa
mazungumzo kufanyika.
Licha ya makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, Israel na kundi la
Hezbollah wamekuwa wakishambuliana.
Ghana kuikabili Ivory Coast katika mechi za kufuzu Afcon 2027
Chanzo cha picha, Getty Images
Ghana wamepangwa pamoja na Ivory Coast katika kundi ambalo linaonekana kuwa gumu kwenye mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027.
Black Stars hawakuwa kwenye chungu cha kwanza cha timu zilizopanda daraja kwenye droo hiyo, baada ya kushuka kwenye viwango vya dunia kufuatia kushindwa kufuzu kwa mashindano yaliyopita yaliyofanyika Morocco mwezi Disemba na Januari.
Mabingwa hao wawili wa Afrika Magharibi watakutana katika Kundi C, ambako pia watacheza dhidi ya Gambia, waliotikisa kwa kufika robo fainali ya Afcon 2021 kwenye ushiriki wao wa kwanza, pamoja na Somalia.
“Kwa nini kila mara sisi? Hili ni kundi gumu,” alisema mchezaji wa zamani wa Ivory Coast, Max-Alain Gradel, ambaye aliisaidia timu ya Elephants kutwaa ubingwa nyumbani mwaka 2022 na alikuwa mmoja wa wasaidizi kwenye droo iliyofanyika Cairo.
“Lakini tutafanya kila tuwezalo kufuzu. Nina imani na timu hivyo hakuna tatizo.”
Kenya, Tanzania na Uganda zitakuwa wenyeji wa pamoja wa Afcon ijayo, itakayofanyika kuanzia tarehe 19 Juni hadi 17 Julai 2027.
Timu 48 zinazowania kufuzu kwa fainali zimegawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja, ambapo timu mbili za juu kutoka kila kundi zitafuzu baada ya raundi sita za mechi.
Hata hivyo, mambo yanakuwa magumu zaidi kwa sababu wenyeji watatu tayari wamehakikishiwa nafasi kwenye mashindano hayo, hivyo ni timu moja tu nyingine kutoka kwenye makundi yao itakayopata tiketi ya kufuzu.
Nigeria, Afrika Kusini na Tunisia zina nafasi ndogo ya kufanya makosa baada ya kupangwa pamoja na mmoja wa wenyeji hao watatu.
Kenya itacheza dhidi ya Eritrea, ambao wanarejea kwenye mechi za kufuzu Afcon kwa mara ya kwanza tangu mchujo wa mashindano ya 2008, pamoja na Guinea na Afrika Kusini katika Kundi A.
Kwingineko, mabingwa wa kihistoria wa Afcon wenye mataji saba, Misri, wamepangwa pamoja na Angola, Malawi na Sudani Kusini.
Raundi nne za kwanza za kufuzu zitachezwa mwezi Septemba, Oktoba na Novemba mwaka huu, huku mechi mbili za mwisho zikitarajiwa kuchezwa mwezi Machi mwaka ujao.
Rais
wa Urusi, Vladimir Putin, yuko mjini Beijing
kwa ziara ya kitaifa ambapo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa China, Xi Jinping, hii leo.
Putin, aliwasili China usiku wa kuamkia leo, na anatarajiwa kujadili “masuala
muhimu” yanayohusu Urusi na
China,kulingana na taarifa iliyotolewa na ikulu
ya Kremlin.
Ziara ya Putin, ambayo
ndiyo safari yake ya kwanza nje ya taifa lake mwaka huu wa 2026, imejiri siku chache tu
baada ya ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump,
nchini China, ambapo walijadili
na Rais Xi masuala mbalimbali ya kibiashara ikiwemo vita vya Iran.
Wizara
ya Mambo ya Kigeni ya China imesema ziara ya Putin
inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wa mataifa hayo mawili.