Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Ujerumani yasema kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani ni jambo lililotabirika, Trump aonya kuhusu kupunguza zaidi vikosi vyake

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani amesema kuwa uamuzi wa Marekani kuondoa wanajeshi 5,000 kutoka nchini humo ulikuwa “unatabirika,” huku muungano wa kijeshi wa NATO ukisema kuwa unatafuta ufafanuzi kutoka Washington.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Ashtakiwa kwa mauaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya mtoto wa miaka mitano

    Mwanaume mmoja ameshtakiwa kwa mauaji na makosa mawili ya unyanyasaji wa kingono kufuatia kifo cha msichana wa miaka mitano nchini Australia.

    Mwili wa msichana huyo, anayejulikana kama Kumanjayi Little Baby, jina la bandia alilopewa na familia yake kwa sababu za kitamaduni baada ya kifo chake ulipatikana Alhamisi baada ya siku kadhaa za msako mkubwa wa polisi.

    Jefferson Lewis, mwenye umri wa miaka 47, alishtakiwa kwa mauaji yake Jumamosi usiku na anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne katika mji wa Darwin.

    Watu watano wamekamatwa kufuatia ghasia za vurugu zilizotokea Alice Springs baada ya kifo cha mtoto huyo.

    Kamishna wa Polisi wa Northern Territory, Martin Dole, alitangaza mashtaka dhidi ya Lewis Jumapili asubuhi.

    “Bado hili ni tukio linaloumiza sana, na mawazo yetu yako pamoja na familia ya Kumanjayi, wapendwa wake na jamii pana iliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na matukio haya,” alisema.

    Dole aliomba jamii iheshimu mchakato wa kisheria.

    Inaripotiwa kuwa Jefferson Lewis alishambuliwa katika mji wa Alice Springs kabla ya kukamatwa Alhamisi.

    Unaweza kusoma;

  2. Meli ya mafuta yatekwa nyara karibu na pwani ya Yemen na kuelekea Somalia

    Maharamia wa Kisomali wameiteka nyara meli ya kubeba mafuta karibu na pwani ya Yemen, kulingana na maafisa kadhaa wa usalama wa Somalia waliozungumza na BBC.

    Walinda pwani wa Yemen awali walisema kuwa meli hiyo, MT Eureka, ilikuwa imetekwa nyara na ilikuwa inaelekea Somalia. Vyanzo vilisema ilitekwa na maharamia katika Ghuba ya Aden, karibu na bandari ya Qana.

    Maharamia hao waliondoka katika eneo la pwani la mbali karibu na mji wa Qandala, uliopo kwenye Ghuba ya Aden, kulingana na maafisa watatu wa usalama kutoka eneo la Puntland waliozungumza na BBC.

    Tukio hili ni la pili la kutekwa kwa meli ya mafuta katika eneo hilo ndani ya kipindi cha siku 10, kufuatia kutekwa kwa meli ya Honor 25 na maharamia wa Kisomali tarehe 22 Aprili.

    Meli ya Honor 25 ilikuwa imebeba mapipa 18,500 ya mafuta yaliyokuwa yakielekea Mogadishu.

    MT Eureka ilikuwa inapeperusha bendera ya taifa la Afrika Magharibi la Togo kabla ya kutekwa, na ilivamiwa na watu wenye silaha saa 5:00 asubuhi kwa saa za huko (03:00 BST), afisa wa usalama aliiambia BBC.

    Kwa sasa meli hiyo inasafiri katika Ghuba ya Aden kati ya Yemen na Somalia.

    Katika tukio jingine tofauti, United Kingdom Maritime Trade Operations (UKMTO) iliripoti Ijumaa kuwa “watu wenye silaha” waliokuwa kwenye boti ndogo walikaribia meli ya mizigo karibu na Al-Mukala, Yemen.

    Unaweza kusoma;

  3. Ujerumani yasema kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani ni jambo lililotabirika,Trump aonya kuhusu kupunguza zaidi vikosi vyake

    Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, amesema kuwa uamuzi wa Marekani kuondoa wanajeshi 5,000 kutoka nchini humo ulikuwa “unatarajiwa”, huku muungano wa kijeshi wa NATO ukisema unatafuta ufafanuzi zaidi kutoka Washington.

    Akizungumza na shirika la habari la DPA, Pistorius alisisitiza kuwa “uwepo wa wanajeshi wa Marekani barani Ulaya, na hasa nchini Ujerumani, ni kwa manufaa yetu na pia ni kwa manufaa ya Marekani”.

    Wakati huo huo, msemaji wa NATO, Allison Hart, alisema kuwa muungano huo “unafanya kazi na Marekani kupata maelezo ya uamuzi huo”.

    Alipoulizwa kuhusu kuondolewa kwa wanajeshi hao, Rais wa Marekani Donald Trump alisema: “Tutapunguza kwa kiwango kikubwa, na tutapunguza zaidi ya hao 5,000.” Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.

    Hatua hiyo ya Washington imekuja baada ya Trump kumkosoa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz kwa kauli yake kwamba Marekani “imedhalilishwa” na wajumbe wa Iran katika vita vinavyoendelea.

    Kwa sasa, uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Ujerumani unazidi wanajeshi 36,000 walioko kazini, ukiwa ndio mkubwa zaidi barani Ulaya, ukilinganishwa na takribani wanajeshi 12,000 walioko Italia na 10,000 walioko Uingereza.

  4. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo