Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Israel yasema imefanya mashambulizi ya anga yaliyolenga maeneo ya magharibi na katikati ya Iran

Hakukuwa na maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu idadi ya walioumia au waliouawa, wala maeneo halisi yaliyolengwa katika mashambulizi hayo.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Je mahakama kumsafisha Rigathi Gachagua?

    Na Laillah Mohammed

    BBC Swahili, Nairobi

    Jumatatu Juni 8 ni siku muhimu kwa aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua almaarufu Riggy G, huku Mahakama Kuu ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu iwapo kuondolewa kwake madarakani kupitia kura ya kutokuwa na imani naye, kulifuata katiba ya Kenya au la.

    Majaji Eric Ogolla, Anthony Mrima na Fred Mugambi watatoa uamuzi baada ya miezi kadhaa ya kusikiliza kesi hiyo yenye mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Kenya.

    Gachagua aliondolewa rasmi madarakani Oktoba 17 mwaka 2024, baada ya bunge la taifa kupiga kura ya kumuondoa kwa zaidi ya wabunge 280 kuunga mkono hoja hiyo, kabla Seneti nayo kuidhinisha hatua hiyo.

    Alikabiliwa na mashtaka matano makuu yakiwemo ukiukaji wa katiba, matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi, utakatishaji fedha, utovu wa nidhamu kazini na kuendesha siasa za ukabila.

    Miongoni mwa kauli zilizozua mjadala mkubwa ni ile aliyosema kuwa “wadau waliopiga kura ndio watanufaika zaidi serikalini,” kauli ambayo wakosoaji wake waliitafsiri kuwa serikali ya Kenya Kwanza ilikuwa ikibagua maeneo ambayo hayakumpigia kura Rais William Ruto.

    Katika kesi yake, Gachagua amedai kuwa kuondolewa kwake madarakani kulikuwa mpango wa kisiasa uliopangwa baada ya uhusiano wake na Rais Ruto kuzorota ndani ya serikali ya Kenya Kwanza.

    Pia aliiambia mahakama kuwa Bunge la Taifa na Seneti hazikumpa nafasi yakutosha kujitetea, akisema siku mbili pekee za kujiandaa zilikuwa chache mno kwa kesi nzito kama hiyo.

    Aidha, mawakili wake waliiambia mahakama kwamba Seneti iliendelea na kesi hiyo hata baada ya Gachagua kulazwa hospitalini, huku Spika wa Seneti Amason Kingi akikataa ombi la kuahirisha vikao hadi.

    Uamuzi wa leo unaweza kubadilisha kabisa siasa za Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

    Kama mahakama itakubaliana na Riggy G basi kiongozi huyo wa chama cha DCP atakuwa na nafasi ya kuwania tena uongozi katika uchaguzi mkuu mwakani.

    Lakini Ikiwa mahakama itatupilia mbali ombi la Gashagua, basi atabakia kuwa ‘King Maker’ kwani sheria za uchaguzi hazimruhusu kiongozi aliyeondolewa madarakani kupitia ‘Impeachment’ kuwania tena kiti cha uongozi au iwapo tu wakati wa uchaguzi awe bado mahakamani na hajafikia mahakama ya upeo.

    Je, mahakama itabatilisha kura ya kutokuwa na imani na Rigathi Gachagua au itaacha uamuzi wa Bunge na Seneti usimame?

    Unaweza kusoma;

  2. Rais wa Afrika Kusini atangaza msako mkali dhidi ya wahamiaji haramu

    Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amehutubia taifa na kutangaza hatua kadhaa mpya za kukabiliana na uhamiaji haramu, wakati mvutano ukiongezeka kutokana na maandamano ya kupinga wageni na malalamiko kuhusu ukosefu mkubwa wa ajira.

    Hatua hizo ni pamoja na kuwafunga jela waajiri wanaowaajiri wafanyakazi wasio na vibali halali, kuanzisha mahakama maalum ili kuharakisha uhamisho wa wahamiaji wasio na vibali, na pia kuweka rejesta yenye taarifa za kibaiometriki “kwa kila mtu nchini” ili kuzuia wizi wa utambulisho.

    Hata hivyo, pia alionya wananchi wa Afrika Kusini wasijichukulie sheria mikononi mwao.

    Katika wiki chache zilizopita, mataifa kadhaa ya Afrika yamekuwa yakiratibu uhamisho wa baadhi ya raia wao kutokana na hofu ya vurugu kuongezeka.

    Makundi yanayopinga wahamiaji yanataka wahamiaji wasio na nyaraka kuondoka nchini na yameweka tarehe ya mwisho kuwa 30 Juni.

    Wiki iliyopita, mamia ya wahamiaji wa Kiafrika walikimbia makazi yao katika eneo la Overberg, Mkoa wa Western Cape, baada ya taarifa za vitisho vya nyumba kwa nyumba, pamoja na vifo vya raia wawili wa Msumbiji huko Mossel Bay.

    Wengi walikimbilia katika kumbi za jamii, ufukweni au milimani. Baadhi wameamua kurudi makwao, na mwishoni mwa wiki kundi jingine la takribani watu 140 lilipanda mabasi kwenda Malawi na Msumbiji.

    Mjini Durban, wageni wamekuwa wakipiga kambi nje ya ofisi ya Wizara ya mambo ya ndani kwa wiki kadhaa, wakisema wana hofu ya maisha yao.

    Unaweza kusoma;

  3. Maandamano yafanyika Tehran

    Tunapata baadhi ya picha sasa za maandamano yanayoiunga mkono serikali yanayoendelea Tehran, kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye viunga vya kusini mwa Beirut.

    Wengi wa waandamanaji kwenye picha wamebeba bendera za Iran na Hezbollah, kundi la kisiasa na kijeshi linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon.

  4. Bei ya mafuta yapanda baada ya Iran kurusha makombora dhidi ya Israel

    Bei ya mafuta imepanda Jumatatu asubuhi barani Asia baada ya Iran kurusha makombora dhidi ya Israel kwa mara ya kwanza tangu kufikiwa kwa makubaliano ya usitishaji vita kati ya nchi hizo na Marekani mwezi Aprili.

    Bei ya kimataifa ya mafuta ghafi ilipanda kwa 2.6% hadi $95.50 (£71.60) kwa pipa, wakati mafuta yasiyosafishwa ya Marekani yalipanda kwa 2.5% hadi $92.75.

    Bei za nishati zimekuwa na mabadiliko makubwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano Aprili yalipokubaliwa.

    Bei zimepanda kwa karibu $95 katika wiki iliyopita huku wafanyabiashara wakipima athari za muda mrefu za vita dhidi ya mtiririko wa nishati duniani.

  5. Ripoti za vifo na majeruhi kutokana na tetemeko Ufilipino bado zinathibitishwa

    Kumekuwa na ripoti za vifo kutokana na tetemeko Ufilipino, ingawa bado hazijathibitishwa rasmi.

    Mamlaka zinaendelea kuthibitisha takribanivifo vitano vilivyoripotiwa, kulingana na shirika la habari Reuters.

    Afisa mmoja wa polisi ameiambia AFP kwamba mtu mmoja amethibitishwa kufariki na wengine wanne wamejeruhiwa.

    Diego Mariano, afisa wa taarifa kutoka wakala wa kitaifa wa majanga wa Ufilipino, amesema kuwa ripoti za vifo na majeruhi zinafuatiliwa kwa karibu.

    Pia kuna taarifa za uharibifu mkubwa katika miundombinu mbalimbali.

    Ameonya wananchi kuepuka kurudi ndani ya nyumba zao au majengo mengine, hasa yale yanayoonesha dalili za uharibifu.

    Unaweza kusoma;

  6. Trump asema Netanyahu hatakuwa na jinsi, isipokuwa kukubali yatakayoafikiwa

    Trump amesema kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu “hatakuwa na chaguo lingine” isipokuwa kukubali makubaliano yoyote ambayo Marekani itafikia na Iran.

    Akizungumza na Financial Times kupitia simu, Trump alisema: “Yeye hatakuwa na jinsi. Mimi ndiye ninayeamua. Mimi ndiye ninayeamua kila kitu. Yeye (Netanyahu) si anayeamua.”

    Trump pia aliiambia Axios hapo awali kwamba atamuomba Netanyahu asiendelee kulipiza kisasi dhidi ya Iran baada ya mashambulizi ya hivi karibuni, ili kuhakikisha pande hizo tatu zinaweza kufikia makubaliano.

    Kwa mujibu wa Financial Times, Trump alisema mashambulizi ya hivi karibuni hayajabadilisha chochote kuhusu mchakato wa makubaliano.

    “Tutaona jinsi itakavyomalizika,” alisema Trump.

    Unaweza kusoma;

  7. Tetemeko kubwa la ardhi limekumba eneo la kusini mwa Ufilipino

    Tetemeko kubwa la ardhi limetokea kusini mwa Ufilipino saa majira ya saa moja na dk 37 kwa saa za eneo hilo.

    Kwa sasa ukubwa halisi na kina cha tetemeko hilo bado havijathibitishwa kikamilifu.

    Kulingana na Taasisi ya Ufilipino ya Volkeno na Matetemeko ya Ardhi (Phivolcs), tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 7.0 na kina cha kilomita 10 (maili 6.2).

    Hata hivyo, Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani (USGS) limeripoti ukubwa wa 7.8 na kina cha kilomita 35, huku Kituo cha Utafiti wa Jiolojia cha Ujerumani kikiripoti ukubwa wa 7.8 na kina cha kilomita 50.

    Nchi kadhaa za eneo hilo, zikiwemo Ufilipino, Indonesia na Japani, zimetangaza tahadhari za tsunami.

    Unaweza kusoma;

  8. Israel imesema imefanya mashambulizi ya anga yaliyolenga maeneo ya magharibi na katikati ya Iran

    Israel imesema imefanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya magharibi na katikati ya Iran.

    “Dakika chache zilizopita, Jeshi la Anga la Israel lilishambulia maeneo ya kijeshi yanayomilikiwa na utawala wa kigaidi wa Iran katika maeneo ya magharibi na katikati ya Iran,” Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kupitia Telegram.

    Hakukuwa na maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu idadi ya walioumia au waliouawa, wala maeneo halisi yaliyolengwa katika mashambulizi.

    Katika hatua nyingine, Televisheni ya taifa ya Iran sasa inaripoti milipuko katika miji mitatu baada ya Israel kusema jeshi lake la anga limefanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi katikati na magharibi mwa Iran.

    “Milipuko kadhaa imeonekana kusikika Tehran, Tabriz na Isfahan,” televisheni ya taifa imeandika kupitia Telegram.

    Milipuko pia imeripotiwa kusikika karibu na mji wa kati wa Karaj.

    Taarifa hizi zinakuja wakati hali ya tahadhari ikiendelea kuongezeka kutokana na mfululizo wa mashambulizi kati ya Israel na Iran, huku maelezo zaidi yakitarajiwa kutolewa.

    Unaweza kusoma;

  9. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu.