Je, Trump amesitisha mpango wa kupeleka makombora nchini Ujerumani?

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akighadhabishwa na mataifa ya Ulaya kukataa kumuunga mkono katika vita alivyoanzisha nchini Iran.
Trump ameamua kujibu uamuzi huo wa Ulaya na Ujerumani kwa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani wapatao takriban elfu tano kwa muda wa miezi sita hadi kumi na mbili zijazo nchini humo.
Kujibu hatua ya Trump, kansela wa Ujerumani Friedrich Merz's alitoa taarifa akikashifu vita vya Iran, na hatua ya Trump kutangaza kupunguza idadi ya wanajeshi wake nchini humo na kutishia kuwaongezea vikwazo vya ushuru haswa katika sekta ya magari.
Kando na wanajeshi elfu tano, Trump ametangaza kuwapunguza wanajeshi hao kwa idadi kubwa zaidi.
Haikuwa jambo la kushangaza kwa Ujerumani
Ingawa serikali ya Ujerumani ilionyesha utulivu wake kuhusu tangazo la Trump,Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius alisema kuwa hatua ya Marekani ilikuwa inatarajiwa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Johann Wadephul alisema kuwa hata kabla ya utawala wa Trump, Marekani ilikuwa inataka kuangazia sana eneo la Pacific na China, kwa hivyo walikuwa wanakagua upya vikosi vyao vilivyoko nje ya nchi.
"Hii sio siri, tulikuwa tumejiandaa kwa hili, tumekuwa tukijadili hili na Nato"alisema Wadephul.
Jambo pekee lililoshtua Ujerumani ni tamko la Trump kuwa wamesitisha mpango wa kuwapa makombora yenye masafa marefu.
Hatua ya Trump inazua maswali
Kulingana na mkataba ulioafikiwa kati ya Ujerumani na Marekani miaka miwili iliyopita, Marekani ilitakiwa kuipa Ulaya makombora na mifumo mingine ya ulinzi ili kujilinda dhidi ya Urusi, ifikiapo mwaka wa 2026.
Mkataba huo uliotiwa saini na rais wa kipindi hicho Joe Biden, makombora aina ya Tomahawk, yenye uwezo wa nyuklia na, na ulinzi wa angani wa SM-6, makombora yenye kasi aina ya Dark Eagle yalifaa kupelekwa nchini Ujerumani, ili kuonyesha kujitolea kwa Marekani kama mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya Nato.

Chanzo cha picha, Reuters
Ila taarifa kuwa Trump amesitisha hatua hiyo, imezua wasiwasi nchini Ujerumani.
Hatua ya Trump imechukuliwa kama "kuitunuku" Urusi na kuwaacha washirika wa Ulaya katika hatari.
Maswali yameibuka iwapo Trump aliafikia uamuzi huo baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Urusi Vladimir Putin wiki iliyopita.
Urusi ilikashifu vikali mkataba huo miaka miwili iliyopita na kutishia kuwa miji mikuu ya Ulaya italengwa iwapo watapokea silaha hizo kutoka Marekani.
Wataalam wa ulinzi waonya kuhusu udhaifu uliopo
Wataalam wa ulinzi wanaonya kuwa iwapo Trump atahairisha mpango huo, italeta udhaifu katika ulinzi wa Nato, na wanashauri njia mbadala kuafikiwa hivi karibuni.
Christian Molling,mtaalam wa ulinzi, anaelezea umuhimu wa makombora ya masafa marefu yaliyopangwa kupelekwa nchini Ujerumani, "Makombora hayo yana uwezo wa kukabiliana na shambulio lolote la Urusi dhidi ya taifa lolote la Ulaya kabla hata halijafika kwenye mipaka ya NATO."
Nico Lange, mtaalamu wa sera za usalama alisema kuwa Kremlin imepeleka makombora ya masafa marefu katika eneo la Kaliningrad, lililoko kati ya Poland na Lithuania, na kusema kuwa makombora hayo ni tishio kwa Ulaya,
"Bila makombora ya Tomahawk kutoka Marekani, kuzuia mashambulizi itakuwa vigumu"
Mtaalamu mwingine wa ulinzi kutoka Ujerumani, Carlo Masala, pia alionya kwamba hatua ya hivi karibuni ya Trump "itadhoofisha uwezo wa kawaida wa kuzuia mashambulizi wa NATO."
Pingamizi kutoka Bunge la Marekani.
Bunge la Marekani pia limekosoa uamuzi wa Trump wa kuwaondoa wanajeshi nchini Ujerumani.
Katika taarifa ya pamoja, mwenyekiti wa chama cha Republican wa Kamati za Huduma za Kijeshi za Seneti na Baraza la Wawakilishi, Roger Wicker na Mike Rogers, walieleza wasiwasi mkubwa kuhusu uamuzi wa utawala wa Trump wa kuwaondoa wanajeshi kutoka Ujerumani.
Viongozi hao walisema kuwa kambi za kijeshi nchini Ujerumani zimekuwa zikitumika bila matatizo katika operesheni dhidi ya Iran.
Wicker na Rogers walionya katika taarifa yao ya pamoja kuwa,
"Kupunguza mapema uwepo wa kijeshi wa Marekani barani Ulaya kunaweza kudhoofisha uwezo wa kuzuia mashambulizi na kutuma ujumbe usio sahihi kwa Vladimir Putin."
Je, Trump anachochea mvutano ili kupata fursa nzuri ya kujadiliana?
Bado haijajulikana ni wanajeshi wangapi kati ya takriban 40,000 walioko Ujerumani ambao Trump atawaondoa, au kama ataachana kabisa na mpango wa kupeleka makombora ya masafa marefu nchini Ujerumani.
Duru za kidiplomasia mjini Berlin, zinaashiria kuwa hatua ya Trump huenda inalenga kuimarisha nafasi yake katika mazungumzo.
Shinikizo kwa Merz linaongezeka
Uamuzi wa Trump wa kuondoa wanajeshi kutoka Ujerumani, pamoja na tishio lake la kutoza ushuru wa ziada wa asilimia 25 kwa magari na malori yanayoagizwa kutoka Umoja wa Ulaya, unaonekana kulenga moja kwa moja sekta ya magari ya Ujerumani.
Sekta ya magari ya Ujerumani inapitia wakati mgumu kutokana na kupanda kwa gharama ya mafuta na ushindani kutoka China.
Tishio la viwanda kadhaa kufungwa na watu kupoteza ajira inazidi kuongeza shinikizo kwa kansela Merz ambaye yuko karibu kutimiza mwaka mmoja madarakani.
Kura za maoni nchini Ujerumani zinaonyesha kuwa uungwaji mkono kwa serikali umepungua.

Chanzo cha picha, Focke Strangmann/Getty Images
Sekta ya magari ya Ujerumani inasemaje?
Marekani na Umoja wa Ulaya waliafikia makubaliano ya kibiashara mwaka uliopita.
Hata hivyo, mchakato wa kuidhinisha mkataba huo katika Bunge la Ulaya ulicheleweshwa mara mbili, kufuatia tishio la Trump la kuitwaa kisiwa cha Greenland.
Utawala wa Trump unaishutumu umoja wa ulaya kwa kutofuata makubaliano yaliyofikiwa.














