Dunia inazidi kutajirika, lakini kwa nini vijana hawana furaha?

Chanzo cha picha, Getty Images
Dunia inazidi kutajirika, teknolojia inazidi kuimarika, na fursa mbalimbali zimejitokeza. Ila kwa wakati huo huo, watu wengi wanazidi kusema kuwa hawana furaha.
Professa Ira Bedzov, kutoka chuo kikuu cha udaktari cha Emory anasema hili limekuwa fumbo.
Swali ni, mbona watu hawana furaha wakati huu ambapo dunia inastawi?
Ukiangalia takwimu, kizazi cha sasa kinaishi maisha bora kuliko cha awali. Kuna elimu, dawa na ufahamu umeongezeka. Teknolojia imebadilisha maisha ya wengi.
Sasa unaweza kupiga simu kutumia njia ya video kutoka bara moja hadi nyingine, kuna vitabu vya kusoma mtandaoni na elimu inapatikana kote duniani. Hii haikuwepo miaka 20 iliyopita.
Licha ya kukuwa kwa uchumi na maendeleo ya teknoljia, fahamu ya kuhisi kutosheka inapungua kila siku.
Fumbo la mafanikio
Kulingana na tafiti za hivi karibuni za kimataifa, viwango vya kuridhika na maisha nchini Marekani vimepungua ikilinganishwa na miaka michache iliyopita, na idadi kubwa ya watu wanasema hawaridhiki au hawana furaha.
Hali hii inaonekana zaidi kwa vijana wa kizazi cha Gen Z na millennials.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la Global Development Survey, makundi haya ndiyo yenye viwango vya chini zaidi vya ustawi wa kisaikolojia .
Vijana wengi wanasema kwamba maisha yao hayana maana kubwa kwao, na kwamba kazi zao hazina mchango wowote au lengo madhubuti.
Millennials ambao ni wakubwa kiumri wana hali iliyo bora, ingawa nao pia wanazidi kuhisi shinikizo la kazi, majukumu ya kifedha, na changamoto za kifamilia.
Kizazi cha Generation X pamoja na kizazi kilichozaliwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia kinaonekana kuridhika zaidi na maisha kwa ujumla.
Hata hivyo, kulingana na Ira Bedzov, watu kwenye kundi hili bado wana furaha kiasi kidogo zaidi ikilinganishwa na watu wa umri sawa waliokuwa miaka 10 hadi 20 iliyopita.
Mwelekeo huu umekuwa mkubwa kiasi kwamba mwaka 2023, mshauri wa afya wa serikali ya Marekani, Vivek Murthy, alieleza kwamba upweke na kujitenga kutoka kwa jamii ni tatizo la kiafya la limefikia kuwa janga la kitaifa.
Lakini swali ni je, kwa nini watu wanazidi kupoteza furaha kadri utajiri unavyoongezeka?
Mtego wa kujilinganisha
Sababu moja ya hali hii ni kujilinganisha na watu wengine katika kijamii.
Katika historia ya binadamu, watu hujilinganisha na wale wanaowafahamu binafsi kama majirani, marafiki, na wafanyakazi wenzao.
Hata hivyo, mitandao ya kijamii imebadilisha kila kitu.
Sasa tunaona mamia ya hadithi za mafanikio kutoka sehemu mbalimbali za dunia kila siku.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu kuonyesha wakisafari, mafanikio, mahusiano mazuri, maisha yenye kuvutia yanajumuisha machapisho ya mitandao ya kijamii , ambayo watu huamua kuonyesha dunia.
Kijana anayeyaona machapisho kama hayo kila siku anaweza kwa urahisi kuanza kuhisi kwamba maisha yake si ya kuvutia au hajafanikiwa vya kutosha, hata kama kwa uhalisia mambo yako sawa kwa upande wake.
Utafiti unaonyesha kuwa hali hii imechochea kuongezeka kwa wasiwasi na sonona miongoni mwa vijana, kwa sababu hali yao ya kujithamini inazidi kutegemea jinsi wengine,hata watu wasiowajua wanavyowaona mtandaoni.
Furaha imekuwa kama maigizo
Siku hizi, mafanikio yanazidi kuonekana kama kitu kinachopaswa kuonyeshwa kwa wengine.
Unapofungua mitandao ya kijamii, unakutana na machapisho yaliyojaa hadithi za mafanikio mapya, ushindi wa kikazi, safari mbalimbali za kitalii, na mahusiano yenye furaha.

Chanzo cha picha, Getty Images
Badala ya kuishi na watu wanaowapenda, watu huanza kutafuta shughuli za kushiriki na kujumuika na watu wengine.
Hii imechochea hamu ya kutaka kutambulika kuwa nimepata mafanikio.
Watu wengi hudhania baada ya mafanikio, furaha itakuja moja kwa moja.
Lakini mara nyingi matokeo huwa tofauti. Mtu anapofikia malengo yake, anagundua kuwa bado hana furaha aliyokuwa akiihitaji, na hapo ndipo anaanza kukata tamaa tena.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndoto ya kufanikiwa na uhalisia
Vijana wengi wanakumbana na pengo linalozidi kukua kati ya picha yao ya maisha yenye mafanikio yanavyofaa kuwa na uhalisia wa maisha yao.
Taswira ya ndoto mara nyingi hujumuisha mambo kama elimu ya hadhi ya juu, kazi nzuri, taaluma yenye mafanikio, kusafiri, vitu vya kupendeza, na maisha yenye shughuli nyingi.
Hata hivyo, uhalisia mara nyingi hujumuisha utaratibu wa kila siku, msongo wa mawazo, na kutokuwa na uhakika.
Furaha haitokani tu na mafanikio makubwa,mara nyingi hujitokeza katika nyakati za kawaida za maisha kama vile kazini , katika mahusiano, katika miradi ya pamoja na familia au marafiki, ila si tu mambo yanayoonekana kuvutia kwenye mitandao ya kijamii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati pesa haileti furaha
Ukuaji wa kipato cha mtu huboresha maisha. Huleta usalama, starehe, na fursa mpya.
Lakini baada ya kiwango fulani cha utajiri, pesa huacha kuwa na athari kubwa sana kwenye furaha. Mambo mengine huwa muhimu zaidi:
Mahusiano thabiti ya kijamii
Hisia ya kuwa na uhuru binafsi
Kujihisi kuwa sehemu ya jamii
Mahusiano ya karibu na familia au marafiki
Mambo haya ndiyo huamua jinsi mtu anavyotathmini maisha yake.
Kwa nini kujizuia hakufanyi kazi?
Suluhisho ni rahisi, unahitaji tu kupunguza muda wa kutumia mitandao ya kijamii.
Lakini kulingana na Ira Bedzov, hii mara nyingi hii huwa haifanyi kazi.
Mara nyingi mtu anapoambiwa "usifanye hivi," hamu ya kufanya jambo hilo huongezeka.
Kutokana na hilo, kanuni ya "punguza matumizi ya simu" mara nyingi huwa na matokeo kinyume.
Kwa hivyo, ni muhimu kuelewa kwa nini watu huanza kutumia mitandao ya kijamii kwa kurudia rudia.
Hii huchangiwa sana na uchovu, upweke, au hitaji la kuwasiliana na wengine.
Ukipata njia nyingine ya kukidhi mahitaji haya, tabia yako hubadilika polepole.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na Ira Bedzov, watu wanapaswa kuacha kujilinganisha na watu wengine katika jamii na kuimarisha uhusiano wao wa kijamii
Wakati mwingine, ili kuwa na furaha zaidi, watu wanahitaji kuzingatia zaidi jinsi ya kuishi vizuri na kile walicho nacho tayari, badala ya kutaka mafanikio mapya kila wakati.













