Oparesheni ya Marekani dhidi ya Iran yasitishwa kwa ombi la Pakistan, Je Iran kuishambulia UAE kumeiweka Pakistan katika njia panda?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa operesheni ya kijeshi iliyozinduliwa dhidi ya Iran ili kurejesha usalama wa safari za meli katika Mlango bahari wa Hormuz, imesitishwa, baada ya Pakistan kuwaomba wafanye hivyo.
Mazungumzo ya kupata amani kati ya Marekani na Iran yamekwama tangu kusitishwa kwa mapigano.
Wakati jeshi la Marekani ililenga boti za Iran, Falme za Kiarabu ilitangaza kufanikiwa kudungua makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kiwanda cha mafuta cha Fujairah.
Pakistan ambayo imekuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran, kwa sasa inakumbana na changamoto katika kudumisha usitishaji mapigano na kujaribu kuzishawishi nchi hizo mbili kuafikia makubaliano.
Pakistan imelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Falme za Kiarabu, ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kutatua migogoro kupitia njia ya diplomasia.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa X na Waziri Mkuu wa Pakistan siku ya Jumanne, alielezea uwepo wa ushirikiano na Rais wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan.
Waziri huyo mkuu wa Pakistan alilaani vikali mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyolenga miundombinu katika Falme za Kiarabu.
Bila kuitaja Iran, kiongozi huyo alisema kuwa
"Pakistan inasimama pamoja na ndugu na dada zake wa Emirati, pamoja na serikali ya Falme za Kiarabu, katika kipindi hiki kigumu."

Chanzo cha picha, Telegram
Waziri mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif aliongezea kuwa,
"Pakistan inahimiza pande zote kuheshimu usitishaji mapigano katika hali zote, ili amani ya kudumu iweze kupatikana kupitia mazungumzo na diplomasia"
Taarifa ya Pakistan, ilitolewa wakati kumekuwa na hofu ya mashambulizi kurejea tena, baada ya Iran kulenga kituo cha mafuta cha Fujairah kilichoko Falme za Kiarabu.
Je, shambulio hili jipya dhidi ya Falme za Kiarabu inaleta changamoto kwa Pakistan na pia linaathiri juhudi zake za upatanishi? Je, usitishaji mapigano uko hatarini? Na je, Pakistan inaweza kuishinikiza Iran kutoishambulia Falme za Kiarabu?
BBC imezungumza na wataalamu ili kupata majibu ya maswali haya.
"Pakistan inajaribu kusawazisha mahusiano na nchi zote ambazo ni rafiki."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Imran Ali, aliyekuwa balozi wa Pakistan nchini Oman, anasema kuwa kudumisha uwiano katika nchi rafiki ni kazi ngumu sana.
Akizungumza na BBC News Urdu, Imran Ali alisema kuwa Pakistan ilikuwa tayari "inatembelea kwenye kamba nyembamba" hata kabla ya vita kuanza, ikijaribu kusawazisha mahusiano yake na Saudi Arabia na Iran.
Aliongezea kuwa "vita viko karibu kuanza tena, na ikiwa vita vitaanza tena, Pakistan inaweza tu kuwaambia pande zote kwamba vita havina manufaa yoyote."
"Pakistan haiwezi tena kuzishawishi nchi hizi, zinapaswa kujishawishi zenyewe. Pakistan ilifanya juhudi kubwa kushawishi usitishaji mapigano baada ya kuzikutanisha nchi hizo mbili ana kwa ana."
Mchambuzi wa masuala ya ulinzi, Hassan Askari, anasema kuwa mahusiano kati ya Iran na Falme za Kiarabu yanazidi kudorora na kwamba mkataba huo wa usitishaji mapigano uko hatarini. Anaeleza kuwa Falme za Kiarabu imeashiria uwezekano wa kujibu mashambulizi.
Akizungumza na BBC News Urdu, alisema kuwa vita vilimalizika kutokana na juhudi za Pakistan, na kwamba pale ambapo makubaliano yanakiukwa, hali hiyo inaongeza matatizo na changamoto kwa Pakistan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, Pakistan inaweza kusitisha mashambulizi dhidi ya Falme za Kiarabu?
Imran Ali anasema kuwa mkakati wa vita wa Iran uko wazi, kila mara Iran inapokuwa na mgogoro na Marekani, inalenga nchi za Ghuba.
"Iran inaona kuwa Falme za Kiarabu inaipa Marekani uungwaji mkono wa kimaadili, hivyo inaona ni halali kuishambulia. Hata hivyo, Pakistan haitaki Iran kushambulia Falme za Kiarabu."
Anaongezea kuwa mapendekezo ambayo Iran iliwasilisha siku chache zilizopita ya kumaliza vita yalikuwa hatua kubwa na yangeweza kusaidia nchi hizo mbili kusonga mbele.
"Pakistan haina mamlaka ya kisheria ya kulazimisha nchi hizi mbili kuheshimu makubaliano. Inaweza tu kujaribu, na itaendelea kufanya hivyo kama mpatanishi."

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, Pakistan itasalia kuwa mpatanishi mkuu?
Imran Ali, anasema kuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, anasema Pakistan ndiyo mpatanishi, lakini wakati huohuo pia amezuru Urusi na China.
Kulingana naye, kama Pakistan itaendelea kuwa mpatanishi mkuu au la, si jambo muhimu sana kwa sasa. Kilicho muhimu ni vita kumalizika na Mlango bahari wa Hormuz kufunguliwa, hata kama nchi nyingine pia zitajiunga katika upatanishi.
Anaongezea kuwa "kama kungekuwa na duru ya pili ya mazungumzo nchini Pakistan, matatizo mengi yangeepukika."
Hassan Askari, anasema kuwa Pakistan kulaani mashambulizi dhidi ya Falme za Kiarabu bila kuitaja nchi yoyote, haikuharibu mahusiano yake na nchi yoyote katika suala hilo. Wakati Marekani na Israel zilipoishambulia Iran, Pakistan pia ililaani mashambulizi hayo bila kutaja nchi yoyote.













